Social Icons

Sunday, 22 September 2013

KATIBA MPYA ILIKWAMA TOKA MWANZO.


MATUKIO ya vurugu, kauli kinzani na hata mgawanyiko wa ndani na nje wa chama na vyama kuhusu Katiba mpya, sasa umezaa mpasuko mkubwa ambao kama hautazibwa, unaweza kuzima ndoto ya kupatikana kwa chombo hicho kabla ya mwaka 2015.


Wakati mvutano baina ya vyama vya upinzani na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ukishudiwa sasa kutokana na hatua ya Bunge kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, ndani ya vyama vya siasa nako kumeonekana kuwapo kwa mgawanyiko wa kimtazamo, hasa kuhusu kipengele cha serikali tatu, kilivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

Kabla ya uelekeo wa upepo wa sasa ambao umechukua sura ya upinzani wa vyama vya upinzani (Chadema, CUF na NCCR Mageuzi) Vs Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndani ya vyama vya CCM, Chadema na CUF tayari kulikuwa na mgawanyiko uliotokana na kuwapo kwa mitizamo tofauti kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya na pia kipengele hicho cha serikali tatu. 

Wakati CCM na CUF wakivurugwa na kipengele cha serikali tatu, Chadema wao walikuwa wakikabiliwa na mtihani wa mwakilishi wao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesigwa Baregu, ambaye aligomea agizo la chama chake lililomtaka ajiengue katika Tume hiyo kutokana na kutoridhishwa na mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya. 

Kwa upande wa CCM, wakati Mwenyekiti wa Chama hicho, Jakaya Kikwete akiwataka wanachama wake wajiandae kisaikolojia kuhusu suala la muundo wa serikali tatu, Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, amekuwa akisisitiza sera yao ya kuamini katika mfumo wa serikali mbili.

Vivyo hivyo kwa Chama cha Wananchi (CUF), wakati Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, akiunga mkono mfumo wa serikali tatu, licha ya kusisitiza kama ni msimamo wa pamoja wa chama, lakini zipo taarifa zinazodai kuwa baadhi ya viongozi wenzake wa upande wa Zanzibar wamekuwa wakishinikiza mfumo wa serikali ya mkataba.

Ni kwa mwenendo huo na mpasuko unaoonekana sasa, ndio ambao umewafanya baadhi ya wachambuzi waanze kupata shaka ya kusainiwa kwa muswada wakati ambapo Watanzania wakiwa tayari wamegawanywa na wanasiasa.

Kinachojitokeza sasa si kigeni, kwani mwaka 2011, kabla ya Rais Jakaya Kikwete hajasaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ambao ulifungua awamu wa pili ya kuanza mchakato wa kuandika Rasimu ya Katiba mpya, alijikuta akikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa Chadema, kabla ya kupatikana kwa muafaka baada ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza.

DK BANA, BAREGU: BUSARA ITUMIKE 

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, aliliambia MTANZANIA Jumapili kwamba Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba urudishwe bungeni ili ujadiliwe upya, kwa muktadha wa kuondoa dosari ambazo zimesababisha mvurugano wa mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Anasema, kinachotakiwa sasa ni kupitisha muswada unaowaunganisha Watanzania na si ule ambao unaonesha kuwatenganisha.

“Ni bahati mbaya sasa kwa Bunge kupitisha Muswada ambao unawagawa Watanzania, hivyo busara itumike ili kuondoa dosari iliyopo,” alisema Profesa Baregu. 

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, anasema kinachotokea sasa katika mchakato wa Katiba mpya ni mkanganyiko hai ambao kwa namna moja au nyingine ni lazima usababishe mpasuko.

Akifafanua hoja hiyo, Dk. Bana anasema kwa ulipofikia mchakato wa Katiba Mpya, hakuna budi busara kutumika ili kuepusha matatizo zaidi ambayo dalili zake zinaonekana kwa sasa.

“Huu ni mnyukano hai, na siku zote masuala ya mchakato lazima watu mvutane, lakini cha muhimu hapa ni busara, CCM wasitake kung’ang’ania mambo ya miaka ya 1960, watu wanahitaji mababadiliko, hivyo msimamo wao unaibua hisia ya kipi kitaendelea ndani ya Bunge la Katiba.

Kuhusu muungano wa vyama vya upinzani, anasema: “Huu muungano wa viongozi wa upinzani uwe wa kuwanufaisha Watanzania na isiwe kwa maslahi yao binafsi...hata hivyo muungano huo ni mchezo wa kitoto kwa sababu hautabadilisha chochote, kwa kuwa taratibu zote za muswada unaopigiwa kelele umepitishwa kwa mujibu wa kisheria”.

Chanzo:- Mtanzania.


No comments:

 
 
Blogger Templates