Kinana alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Kijiji cha Mwasengela, wilayani Meatu na wilayani Itilima mkoani Simiyu, ambavyo vimepakana na Pori la akiba Maswa, ambapo wananchi wake walilalamikia hatua ya kupigwa na kukamatwa kwa mifugo yao na askari wa wanyamapori.
Kinana alisema kutokana na hali hiyo, ni lazima Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kumaliza migogoro hiyo kabla ya damu kumwagika na kuleta maafa kwa Taifa.
Alisema maeneo mengi yamekuwa na malalamiko ya wananchi dhidi ya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya hifadhi za Taifa, bila kutoa kipaumbele kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na kulisha mifugo yao.
Alisema kuwa ni lazima mawaziri husika wa Wizara za Maliasili na Utalii pamoja na Ardhi, watumie busara ya kufikia katika maeneo hayo ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro hii.
“Haiwezekani hata kidogo, mipaka hii iliwekwa kwa ajili ya wanyama mwaka 1940, wakati huo Watanzania walikuwa milioni sita tu. Sasa tupo milioni 45 hatuwezi kuendelea na sheria hizi ambazo ni wazi zinaonekana ni kandamizi dhidi ya wananchi wake.
“Kila mahali kumekuwa na migogoro ya aina hii na hata kufikia hatua ya askari kuua raia, kwa sababu wameingiza mifugo kwenye hifadhi huku wengine wakitozwa fedha bila hata kukatiwa stakabadhi za malipo.
“Nimekwenda Morogoro, Njombe, Mikumi, Kilosa na Wanging’ombe kote huko ni malalamiko kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi hata huko Arusha na Tanga, pia kuna migogoro ya aina hiyo na maeneo mengine mengi.
“Kuna haja ya mawaziri hawa na popote walipo wanisikilize kwa agizo hili kuwa wasikae kimya hadi watakapoona damu inamwagika ndio waanze kutafuta ufumbuzi wake, ila waanze sasa,” alisema Kinana.
Aliongeza kuwa ni kweli Tanzania inataka kutunza rasilimali za Taifa ikiwemo wanyama, ila ni lazima Serikali itambue kuwa binadamu nao ni muhimu kupewa kipaumbele na Serikali itumie busara ili kumaliza matatizo hayo.
Alisema hakuna sababu ya kuendelea na sheria ambazo zimewekwa tangu wakati wa ukoloni, kwa ajili ya kulinda wanyama na hifadhi zake na badala yake sheria hizo zinaweza kuangaliwa upya kwa maslahi ya Taifa na kizazi cha sasa na vijavyo.
Awali akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mwasengela, mmoja wa wanakijiji aliyefahamika kwa jina la Zunzu Ndaturu kwa niaba ya wenzake, alisema kuwa askari wa Pori la akiba la Maswa wamekuwa wakikamata mifugo ya wananchi na kuwatoza Sh milioni 1.5, huku mifugo mingine ikifa kwa njaa kutokana na manyanyaso hayo.
Akizungumzia utekelezaji wa ilani ya CCM kwa wananchi wa Kata hiyo, Mbunge wa Kisesa, Luaga Mpina, alisema amefurahishwa na kasi ya maendeleo kwani ujenzi wa vituo vya afya, miundombinu ya barabara, umeme na maji vinatekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Chanzo :- Mtanzania
No comments:
Post a Comment