Wakati Tanzania ikitegemea kuanza kufaidika na madini ya urani, tayari kuna harufu ya ufisadi inayogubika kampuni za uchimbaji wa urani wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.
Akifafanua utafiti alioufanya kuhusu athari za uchimbaji madini ya urani nchini hivi karibuni jijini Dar es Salaam, mwanasheria wa mazingira Dk Lugemeleza Nshala anasema harufu hiyo inatokana na kampuni ya Mantra Resources Limited yenye leseni katika eneo la Mkuju River kujigawa katika kampuni mbili yaani ARMZ na Uranium One.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anabainisha kwamba shauri hilo lipo mahakamani na kwamba kumekuwapo uovu mwingi kwenye sekta ya madini.
“Ni kweli kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamepeleka suala hilo mahakamani, lakini mkataba wa kuchimba madini hayo ni mwingine kabisa. Nakubaliana na wewe pia kwamba kumekuwa na mikataba mibovu, sijui kuna watu wamekula, lakini Watanzania tuwe na mtazamo wa kuendelea siyo kuangalia nyuma.
“Huo ni mtazamo wa kizamani, tumekuwa na muda mwingi wa kujadili matatizo tu, tumekuwa waoga mno wa kuthubutu, haya matatizo popote yapo. Mfumo wa dunia kwa sasa ni uwekezaji, tuwekeze ndani na nje ya nchi ili kupata fedha na ajira,”anabainisha Profesa Muhongo.
Ukwepaji kodi
Dk Nshala anasema: “Oktoba 2010 Mantra Resources Limited ya Australia inayomiliki leseni ya Mkuju River iliingia kwenye utekelezaji wa mkataba na kampuni ya Atomredmetzoloto (ARMZ) ya Russia katika makubaliano yao na ARMZ ilitakiwa iwalipe Mantra dola 1.6 bilioni za Marekani ikiwa ni asilimia 100 ya kumiliki Mantra.
“Hivyo makubaliano ya kuuza hisa zake yalikuwa ni dola 8.00 za Australia kwa kila hisa, lakini kutokana na tetemeko lililotokea Fukushima Japan kwenye kinu chake cha nyuklia miezi minne baadaye, ARMZ wakataka kujitoa.
“Lakini baadaye wakaja na makubaliano mapya na Mantra hawakuwa na la kufanya ila kuingilia makubaliano ya kushusha bei ya dola za Australia 7.02 kwa kila hisa ambayo ni sawa na dola 1.04 bilioni za Marekani ya hisa zote. Hadi Juni 7, 2011 makubaliano yakafikiwa na ARMZ ikamilikishwa hisa zote.
“Mwaka huohuo, ARMZ ikaingia mkataba wa kununua hisa 51.4 za kampuni ya Uranium One ambayo ni kampuni tanzu ya Canadian uranium mining company,” anasema Dk Nshala.
Anaendelea kufafanua: “Hivyo kuhamishwa kwa Mantra Resources Limited kutoka ARMZ ili wadau wa awali kupata dola 1.04 bilioni za Marekani bila kulipa kodi ya mapato kwa Tanzania.
Chanzo :- Mwananchi
No comments:
Post a Comment