Social Icons

Friday, 20 September 2013

MAMA ZITTO AWAFUNDA MBOWE, LIPUMBA NA MBATIA.


MAMA mzazi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), Shida Salum, ametoa siri nzito kwa viongozi wa vyama vya upinzani ambayo itawawezesha kuchukua dola kirahisi ifikapo 2015. Mama Zitto, alisema ikiwa vyama vya upinzani vitaendeleza muungano wao kama ulivyo sasa na kuweka dhamira ya dhati ya kutekeleza mahitaji muhimu, vitachukua dola kirahisi kutoka mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Mama Zitto, aliitoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam jana, mbele ya wenyeviti wa vyama vitatu vya upinzani, akiwamo Freeman Mbowe (CHADEMA), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR Mageuzi).

Viongozi hao, walikutana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kwa lengo la kuwaomba kuwaunga mkono na kumsihi Rais Jakaya Kikwete asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya kutokana na kuwa na kasoro nyingi.

Mama Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa viungo na mwanzilishi wa SHIVYAWATA, alisema kundi la walemavu limesahaulika ndani ya Serikali na linaishi katika mazingira hatari.

“Hakuna ubishi sisi walemavu tumesikitishwa na jinsi tulivyotengwa na mchakato huu wa Katiba mpya na badala yake tunajumuishwa kwa kuwekwa kwenye makundi maalumu.

“Walemavu tupo milioni 7.9 Tanzania Bara na Visiwani na kati ya hao, wapiga kura ni milioni tano, sasa kama mnataka kukamata dola hebu jaribuni kuzingatia mahitaji ya kila kundi na kuwafikia pale walipo.

Naye Rais wa Chama cha Kutetea Watu Wasio na Akili Timamu, Robert Bundala, alimpa Mbatia jukumu la kuhakikisha anamuondoa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kwenye wizara hiyo.

Alisema Serikali imetelekeza makundi ya watu wenye ulemavu kwa kushindwa kuwapa haki yao ya kupata elimu na mahitaji yao muhimu.

Pamoja na mambo mengi, walitoa masharti kwa viongozi wa vyama vitatu vya upinzani ili kuweza kushirikiana katika kuhakikisha dhamira na malengo yanatimia.

Chanzo:- Mtanzania.

No comments:

 
 
Blogger Templates