Social Icons

Friday, 20 September 2013

KINANA: CCM HAITAKUBALI KUBURUZWA.


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema kamwe chama hicho hakitakubali kuburuzwa na watu ambao wamekataliwa na wananchi. Alisema kutokana na hali hiyo, CCM pamoja na Serikali, wamejipanga kukataa hali hiyo ndani na nje ya Bunge kwa kuhakikisha wanafanya kazi kila kona ya kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza ahadi.

Kinana alitoa kauli hiyo jana, katika Kijiji cha Iganganulwa, Kata ya Dutwa, wilayani Bariadi.

Alisema kutokana na hila na vitimbi vinavyofanywa na vyama vya upinzani, ni wazi Watanzania watatoa salamu wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Alisema Tanzania ina chama kimoja cha siasa, ambacho ni CCM, huku vyama vilivyobaki 18 ni walalamikaji wa kila kukicha kupitia vyombo vya habari, badala ya kuwahudumia wananchi katika majimbo yao ya uchaguzi.

“Ninasema wazi mchana kweupe, CCM haiko tayari na wala haitakubali kuburuzwa na vyama ambavyo vimekataliwa na wananchi kupitia masanduku ya kura.

“Hivi vyama, vimekuwa ni vya ‘press’ (mikutano ya waandishi wa habari) kila kukicha Dar es Salaam na vimekosa ajenda ya kufanya na badala yake, vimekaa kutengeneza uongo na fitna, ila watambue kuwa salamu zao watazipata mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Kinana.

Alisema kutokana na tabia hiyo, anaamini mwaka 2015 itakuwa msiba kwa vyama vya upinzani na katu wasitegemee kupewa madaraka na wananchi ambao wamechoka na vitimbi vyao vya kuharibu umoja wa kitaifa.

Katika hatua nyingine, Kinana amemsafisha Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, kwa kusema ni kiongozi mchapakazi.

Kauli hiyo, ilisababisha shangwe na nderemo kutoka kwa wananchi waliokusanyika, huku akiwataka wasidanganyike kuchagua mtu mwingine.

Alisema hakatazi mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea ubunge kufanya hiyo, ila lazima wana CCM wawe makini na watu wanaotaka uongozi kwa kuwapima kwa maneno na vitendo vyao kabla ya kufanya uamuzi.

Kwa upande wake, Chenge alisema katika kipindi cha uongozi wake, jimbo hilo limefanikiwa kuunganisha mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa shule za sekondari.

Chanzo:- Mtanzania.

No comments:

 
 
Blogger Templates