Social Icons

Saturday 12 October 2013

DR. MAHANGA, MEYA SLAA WAVUTANA.


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga amembeza Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa kwa hatua yake ya kumshambulia kupitia vyombo vya habari akibainisha kuwa busara yake ni ndogo kama umri wake.

Dk Mahanga alimbeza Silaa juzi, wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya kuhojiwa ambapo alibainisha zaidi kuwa, busara na umri alionao vinamwongoza asilumbane na viongozi wenzake kwenye vyombo vya habari.

“Mimi nina miaka 58 yeye ana miaka 31, busara zetu ni tofauti sana hata kwenye malumbano, ingawa mimi nina cheo kidogo kwenye chama ukilinganisha na yeye, mimi ni mbunge tu CCM, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama, wakati yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,” alisema Dk Mahanga.

Alisisitiza kuwa busara aliyonayo meya huyo ndiyo iliyomfanya amfananishe na Punda ndani ya Baraza la Madiwani waliokuwapo kwenye kikao hicho na waandishi wa habari waliohudhuria.

Kwa upande wake, Meya Silaa alibainisha kuwa tuhuma dhidi ya Dk Mahanga zilitolewa ndani ya Kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 11 la Aprili 16, mwaka 2004, kanuni za kudumu za halmashauri hiyo sehemu ya (iii) 24 inakataza suala lililojadiliwa kwenye kikao hicho kuhojiwa nje ya hapo na chombo chochote ikiwamo mahakama.

“Kanuni hiyo inaeleza kutakuwa na uhuru wa kutoa mawazo wakati wa majadiliano katika mikutano ya halmashauri na uhuru huo hautaweza kuhojiwa katika mahakama yoyote au popote nje ya mkutano wa halmashauri,” Silaa alinukuu kanuni hiyo.

Oktoba 3, mwaka huu Meya Silaa, alikaririwa na vyombo vya habari akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Ilala,Dar es Salaam, akilaani vikali migogoro ya kisiasa isiyo na tija kwa wananchi ukiwamo uliosababishwa na barua iliyoandikwa na Mbunge wa Segerea ambaye ni Dk Mahanga.

Alidai kuwa barua hiyo ilisababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Gabriel Fuime kusimamishwa kazi bila kufuatwa taratibu za utumishi hivyo kutia doa utumishi wake wa muda mrefu.

Silaa alisisitiza kuwa, Dk Mahanga hakujali msaada wa Fuime ambaye aliutoa jimboni kwake wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010, badala yake kuna barua ya siri iliyoandikwa kwenda Tamisemi ikimtuhumu Fuime na Silaa wakidaiwa kuhusika na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.

Ilidaiwa kuwa kutokana na tuhuma hizo, Fuime alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake ambapo miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kushindwa kusimamia mapato ya halmashauri hiyo na ukodishaji unaotia shaka katika Soko la Samaki Feri.

Chanzo:- Mwananchi


No comments:

 
 
Blogger Templates