Social Icons

Saturday 12 October 2013

JK: MA-DC MUWE NA AJENDA.


RAIS Jakaya Kikwete, amewataka wakuu wa wilaya na wabunge kubuni mipango kazi na ajenda za kusimamia maendeleo kama namna ya uhakika zaidi ya kutoa uongozi kwa jitihada za wananchi kujiletea maendeleo.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na viongozi wa mkoa wa Pwani kwenye Hoteli ya Oceanic Bay mjini Bagamoyo wakati akikamilisha na kujumuisha ziara yake ya siku sita ya kukagua na kuzindua shughuli na miradi ya maendeleo katika mkoa huo.

Alisema ukosefu wa mipango ya kazi na ajenda ya utendaji unasababisha wakuu wa wilaya wengi kuendesha shughuli zao kwa matukio tu na kutegemea ratiba za ziara za wakubwa zao wa kazi.

Alisema anatamani kazi yake ingekuwa inampa uhuru wa kuingia wilayani na kukagua mipango kazi ya mkuu wa mkoa bila kujulikana kama ameingia katika wilaya hiyo.

“Maendeleo ya wananchi ndiyo shughuli yenu kubwa ya uongozi. Hivyo, ni lazima muwe na mipango kazi ya maendeleo ya wananchi. Na kwa sababu wakati mwingi hatuna mipango kazi ya shughuli za kila siku za maendeleo ya wananchi basi tunafikia hatua ya sisi viongozi kuanza kugombea mafaili.

“Kwa hakika, natamani kuwa ningekuwa na nafasi na uhuru wa kuchomoka bila kugundulika na kuingia katika wilaya kukagua mipango kazi ya mkuu wa wilaya bila kujulikana kama nimeingia katika wilaya hiyo.

Na kwa sababu wengi wetu hatuna mipangokazi na ajenda ya kazi ya maendeleo ya wananchi tunaishia katika kwenda na matukio, akifika Waziri Mkuu tunaingia katika ratiba yake, akifika fulani tunapata ajenda ya kazi,” alisema.

Rais Kikwete alisema endapo viongozi hawatakuwa na ajenda ya maendeleo hakuna jambo lolote la maana litafanyika.

“Bila nyie viongozi kuwa na ajenda ya maendeleo, hakuna jambo lolote la maenddeleo ambalo litafanyika na mtamaliza muda wenu na kuondoka madarakani bila kuacha lolote la kukumbukwa na wananchi,” alisema.

Chanzo:- Tanzania Daima.

No comments:

 
 
Blogger Templates