BENCHI la Ufundi la Simba limewahakikishia namba wachezaji wanne, lakini likaweka wazi kwamba ugomvi wao mkubwa na wachezaji ni ulevi, starehe za wanawake na kuchati kwenye mitandao ya kijamii hadi usiku wa manane.
Kocha wa Mkuu wa Simba, Abdallah Kibaden, jana Ijumaa aliwataja wachezaji Abel Dhaira, Jonas Mkude, Joseph Owino na Betram Mwombeki ambao wana uhakika wa namba katika kikosi hicho.
“Wachezaji wengine wa nje wamesajiliwa kwa gharama kubwa huwezi kuwaweka benchi ni lazima wacheze, Mkude kwa kiwango chake cha sasa huwezi kumweka benchi, hata Mwombeki,” alisema.
Kibadeni alisema kwamba amekuwa akizozana na baadhi ya wachezaji kutokana na tabia zao za kupenda anasa na kujisahau kwenye utendaji. “Wachezaji wakipata pesa wanataka watumie watakavyo, wawe na wanawake watatu watatu, walewe, wachati mpaka usiku wa manane ndiyo kazi ya kina Humoud (Abdulhalim), sasa mimi ikifika saa nne nazima taa nawaambia walale hicho wao hawakitaki, wananivizia nimelala wanawasha taa wanaendelea na mambo yao.”
“Kujua mpira isiwe sababu ya kusumbua watu, kuna wachezaji hawajitambui ni lazima tuwaelimishe mfano Singano (Ramadhani) ni darasa la saba, mpira una muda wake asipofanya kitu cha maana leo siku za mbeleni ataishije,’’ alisema Kibaden na kuongeza: “Ni lazima umuelimishe umepata pesa weka benki achana na starehe, baba yako umemnunulia nini mpaka utumie pesa kwa mambo ya wanawake ndiyo ninachofanya sasa hiyo wachezaji hawataki.
“Kuna mshambuliaji nimempa mechi saba, hajafunga goli hata moja sasa mimi mnataka nifanyaje? Ni lazima akae benchi, Simba tuna wachezaji 36 anayefanya vizuri ndio anayeingia kambini kujiandaa na mechi iliyopo mbele yetu, ambaye kiwango kimeshuka anaachwa ajipange kuhakikisha anarudisha kiwango chake,” alisema.
“Mchezaji kama Edo Christopher, yule ni mjukuu wangu kabisa nashangaa watu wanasema simpendi, nagombana naye alishuka kiwango nikamrudisha timu B, sasa amewafunika wote amerudi,” alisema Kibadeni ambaye usiku wa kuamkia leo Jumamosi ametimiza miaka 64.
Chanzo ;- Mwanaspot

No comments:
Post a Comment