Social Icons

Sunday, 13 October 2013

NIDHAMU YA CHUJI YAMSTUA MEXIME


KOCHA wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime amesema kama angekuwa na kazi ya kutoa tuzo za mchezaji mwenye nidhamu bora angempa kiungo wa Yanga, Athuman Iddi ‘Chuji’.

Maxime alisema: “Ni kitu kizuri kuona mchezaji kama Chuji akiwa na nidhamu ya hali ya juu anapocheza kwani wachezaji wengi wa sasa hawajali suala la nidhamu, ningekuwa mtoaji tuzo lazima ningempa Chuji tuzo ya nidhamu, kama kocha kwa kweli ni kitu kizuri ambacho nimekiona kwake na cha kuigwa na wachezaji wengine.”

“Kwa kipindi kirefu sasa nimeona nidhamu yake ikimbeba na kumfanya acheze soka kwa muda mrefu bila kuchoka na hata kuadhibiwa, zamani kidogo nilipokuwa nikichezea Mtibwa Sugar, Chuji mara kwa mara alikuwa akihusika sana kwenye mambo ya utovu wa nidhamu lakini sasa kabadilika mpaka namwona kama si yeye aliyekuwa mpenda fujo na kama mmiliki wa kadi za njano na nyekundu anapocheza,” alisema Maxime.

Naye Chuji alisema,”Nidhamu ndiyo suala kubwa ambalo napenda kulitoa kwa wachezaji wadogo ambao pengine hawana uzoefu mkubwa kwenye soka. Kwa sasa sisi ndiyo wachezaji wenye umri mkubwa kwenye ligi hivyo tunatakiwa kuwa mfano wa kuigwa.”

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema: “Chuji huwa tunapenda kumuiga, amekuwa mstari wa mbele kuonyesha njia kwetu hasa kwa kutuhamasisha kufanya mambo mazuri.”

Chanzo:- Mwanaspot

No comments:

 
 
Blogger Templates