Social Icons

Saturday 12 October 2013

MAGUFULI AZIDI KUWEKWA KITANZINI.


WAMILIKI wa malori nchini wamesema kuwa serikali imepata hasara ya sh bilioni 20 hadi 30 kufuatia kusitishwa kwa huduma ya usafirishaji mizigo kwa madai ya kulinda barabara zisiharibike.

Mbali na hasara hiyo, wamiliki hao wamemuomba Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhakikisha wanamchukulia hatua za kinidhamu Waziri wa Ujenzi, John Magufuli kutokana na kupotosha suala hilo kwa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya wenzake, Azim Dewji ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya usafirishaji ya Simba alisema kuwa serikali imepoteza mapato hayo kutokana na uongo wa Magufuli.

Dewji alisema kuwa hasara waliyoipata wamiliki wa malori hayo ni kubwa na sasa wapo katika kufanya mahesabu ili kuibaini ikiwa ni pamoja na kumchukulia hatua za kisheria Dk. Magufuli kwa kumfungulia mashitaka.

“Serikali tu imepoteza zaidi ya sh bilioni 20 na mama lishe nao wameshindwa kufanya kazi zao huko bandarini. Ni ajabu kuwa na kiongozi anayetesa Watanzania kutokana na uongo wake,” alisema.

Dewji alisema kuwa wamiliki wa malori wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, na kwamba wametoa ajira kubwa kwa Watanzania.

Alisema kuwa kwa kipindi cha siku moja malori zaidi ya 1,000 yamekuwa yakifanya safari nchini na kuingiza fedha nyingi serikalini.

Dewji aliongeza kuwa ni muhimu Dk. Magufuli akatoa maneno yenye hekima na busara, na sio kutumia mabavu na kutoa kejeli dhidi ya Watanzania.

Alisema kuwa Magufuli amewadhalilisha kwa kudai kwamba wamekuwa wakitoa rushwa kwa wafanyakazi wa mizani jambo ambalo halina ukweli wowote.

“Hivi kama sio uongo na upotoshaji unaofanywa na kiongozi huyo ni nini? Ni mfanyabiashara gani aliye tayari kutoa rushwa ya fedha kwa vituo vya mizani zaidi ya 14 vilivyopo kati ya Dar es Salaam hadi Tunduma asiyeangalia faida?” alihoji.

Alishauri kuwa ni vyema waziri huyo akatumia vyombo vya dola kufanya uchunguzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu barabara kuliko kutoa kauli za ubabe na kupotosha.

Kwa mujibu wa Dewji, Waziri Magufuli amekuwa na chuki na wamiliki wa malori baada ya kubaini kuwa walikutana na Kamati ya Miundombinu kipindi cha Bunge na kueleza changamoto zinazowakabili.

Waziri Mkuu Pinda juzi aliagiza wamiliki wa malori kuyaruhusu yasafirishe mizigo kwa utaratibu wa zamani badala ya ule wa Magufuli wa kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2001.

Sheria hiyo inayataka malori yote yanayozidisha uzito uliopo ndani ya asilimia tano kupunguza mzigo, kupanga mzigo upya au kulipia uzito uliozidi mara nne ya tozo ya kawaida.

Chanzo:- Tanzania Daima.

No comments:

 
 
Blogger Templates