Social Icons

Saturday 12 October 2013

MEYA MSTAAFU ASHINDA KESI YA MAUAJI.

VILIO vya furaha jana vilitawala katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo na wenzake watatu kuachiwa huru katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa CCM Kata ya Isamilo, Bahati Stephan iliyokuwa ikiwakabili.

Akisoma hukumu hiyo ya shauri namba 79 la mwaka 2011, Jaji Aisheri Sumari alisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umeshindwa kumtia hatiani mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo, Jumanne Oscar ambaye alituhumiwa kutekeleza mauaji hayo kwa kumchoma Bahati kisu katika ziwa lake la kushoto.

Akisoma maelezo ya shahidi namba 16 na 18 ambao walikuwa ni askari polisi waliokabidhiana mtuhumiwa namba moja, alisema kuwa ushahidi wao ulikuwa na mkanganyiko hivyo kutoa faida kwa washitakiwa.

Jaji Sumari alisema kwa maelezo yao, shahidi namba 16 anasema kuwa alipelekwa mahabusu na shahidi namba 18 kumchukua mshitakiwa namba moja, kisha kmpeleka kwa RCO Muna kuchukuliwa maelezo.

Aliongeza kuwa shahidi namba 18 katika ushahidi wake alisema kuwa tangu alipomkabidhisha mtuhumiwa kwa OCD siku ya tukio, hajawahi kurudi wa kushughulika na kesi hiyo hadi alipokwenda kutoa ushahidi mahakamani.

“Mkanganyiko huo ulitakiwa kuondolewa na Malingumu ambaye mpaka sasa ni askari, lakini upande wa Jamhuri wameshindwa kushughulika na hilo, hivyo kushindwa kuamini maelezo ya ushahidi,” alisema.

Jaji Sumari alisema kuwa pande wa mashitaka haukutaka Malingumu kufika mahakamani kuthibitisha mtuhumiwa aliyekabidhiwa na shahidi namba 18 (Sostenas) kama ndiye mshitakiwa namba moja.

Alisema kuwa uwezekano wa kuwachanganya washitakiwa ni mkubwa kutokana na ushahidi uliotolewa na shahidi namba 16 na 18, kwa sababu kama mshitakiwa namba moja ndiye aliyekamatwa ziwani, haoni kwanini awe na majeraha wakati shahidi namba 7 na namba 2 walimkabidhi mtuhumiwa kwa askari bila majeraha yoyote.

Kufuatia maelezo hayo, Jaji Sumari alisema kuwa kuna mkanganyiko mkubwa upande wa mashahidi wa Jamhuri juu ya mtu aliyechukuliwa na polisi na mtuhumiwa aliyetolewa ziwani.

“Hapa kuna maswali mengi ya kujiuliza, kwanini upande wa Jamhuri hawakuita gwaride la utambuzi kwa sababu wananchi ndio waliomkamata mtuhumiwa ziwani na kumkabidhi kwa askari wakati kesi hiyo imechukua muda mrefu?” alihoji.

Alisema kuwa anakubaliana na hoja za wakili wa mshitakiwa wa kwanza, Stephan Magoiga kuwa ushahidi unaotolewa hapo ni utambuzi wa mahakamani na si eneo la tukio ambapo mahakama haiwezi kumtia hatiani mshitakiwa huyo.

Kuhusu upande wa utetezi wa washitakiwa, Jaji Sumari alisema kuwa mtuhumiwa namba moja ambaye alikuwa na kesi ya kujibu aliuchambua vizuri ushahidi uliotolewa na shahidi namba 16 na 18 na kudai kuwa umeonyesha wazi mkanganyiko kutokana na vielelezo vya nguo ambavyo alikuwa amevaa.

Alisema kuwa mashahidi hao walimtambua kwa suruali aliyokuwa amevaa aina ya jinzi ambapo kielelezo kilichofikishwa mahakamani ni cha suruali ya khaki ambayo ilikuwa na damu.

Kutokana na maelezo hayo, Jaji Sumari alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri kuwa hauwezi kuwatia hatiani washitakiwa wote wanne, hivyo akawaachia huru.

Chanzo:- Tanzania Daima.

No comments:

 
 
Blogger Templates