Social Icons

Saturday 12 October 2013

MWAKYEMBE AZITAKA BENKI KUISAIDIA BANDARI.


Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameziomba taasisi za kibenki nchini, kutoa huduma kila siku, ili kupunguza foleni ya meli zilizopo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe inatokana na kumalizika kwa mgomo wa malori uliodumu kwa zaidi ya siku tatu na kusababisha meli zaidi ya 27 kukwama katika foleni ya kushusha shehena.

Dk Mwakyembe alisema hayo jana wakati akiipokea meli kubwa yenye zaidi ya mitaa 250. Alisema ni vyema benki zikafanya kazi kila siku ili kuongeza ufanisi wa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Taasisi za kibenki tumeziomba kusogeza huduma hapa bandarini na wafanye kazi hadi mwishoni mwa wiki ili kuendelea kupunguza meli zinazosubiri kushusha mizigo. Watanzania tuache kulala tuko nyuma, tuchape kazi hata Jumapili tuisogeze mbele nchi yetu,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema kuwasili kwa meli hiyo kubwa kunafungua milango kwa meli zingine za aina hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Madeni Kipande, alisema wamefanya juhudi za makusudi kuileta meli hiyo yenye uwezo wa kubeba kontena zaidi ya 4,500 ili kuonyesha uwezo wa bandari hiyo katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema wanaendelea kuhakikisha kuwa bandari hiyo inapiga hatua zaidi kwa kutoa huduma bora na kwa ufanisi zaidi kwa kupunguza muda wa upakuaji wa mizigo kwa haraka zaidi.

“Tutafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha meli kuwa zilizopo katika foleni zinaondoka kwa wakati. Tmejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa bandari hii inaendelea kuwa bora,” alisema Kipande.

Kwa upande wake, Nahodha wa meli hiyo ambaye ni Mtanzania, Abdull Mwingamno, alisema kazi ya kuileta meli hiyo nchini kutoka Ruanda, Angola ilikuwa rahisi.

“Namshukuru Mungu kuwa nimeifikisha salama meli hii na najua kufika kwa meli hii nchini kwetu kutazifanya na meli kubwa zaidi ya hii kuja nchini kwetu,” alisema Mwingamno.

Chanzo:- Mwananchi.


No comments:

 
 
Blogger Templates