LUGHA ya Kichina imeanza kufundishwa rasmi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), lengo likiwa ni kuwasaidia wanafunzi na wafanyabiashara wanaosafiri kwenda China.
Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Yunus Mgaya, alieleza hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ufundishwaji wa lugha hiyo ambayo wameanza kufundisha kozi fupi kwa sasa lakini kwa siku zijazo watafundisha digrii.
“Kichina kitawasaidia wafanyabiashara wanaotoka nchini kwenda China kwenye shughuli za kibiashara pamoja na wanafunzi wa Kitanzania wanaopata ufadhili kwenda kusoma huko,” alisema.
Aliongeza kuwa ufundishaji wa somo hilo pia utasaidia katika soko la utalii kwa kuwa kuna ongezeko la watalii kutoka China.
Profesa Mgaya alisema UDSM kwa kushirikiana na serikali ya watu wa China wameanzisha kituo cha kufundisha lugha hiyo na utamaduni wa Kichina.
“Januari mwaka huu UDSM iliingia katika makubaliano na Chuo Kikuu kilichoko China; tumekubaliana nao kwa pamoja kuendesha kitengo cha kufundishia lugha ya Kichina,” alisema.
Alisema mpaka sasa kozi nne za lugha ya Kichina zimeshaendeshwa chuoni hapo, ambapo wanafunzi 68 wamenufaika na kwamba kituo hicho kitazinduliwa Jumatano ijayo chuoni hapo.
Chanzo:- Tanzania daima.
No comments:
Post a Comment