RASIMU ya Pili ya Katiba Mpya ya Tanzania iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete, mwanzoni mwa wiki hii, imependekeza mapinduzi makubwa katika maadili ya viongozi wa umma na namna uchaguzi wa nafasi za kisiasa za dola utakavyokuwa ukiendeshwa hapa nchini.
Ingawa si lazima mapendekezo yote ya rasimu hiyo kupitishwa na Bunge la Katiba na katika kura ya maoni baadaye; mengi ya mapendekezo hayo yametokana na kilio cha muda mrefu cha wapenda maadili ambao walikuwa wakiona namna miiko ya uongozi ilivyokuwa ikikiukwa katika miaka ya karibuni.
Katika ibara ya 15 ya rasimu hiyo, inapendekezwa kwamba viongozi wa umma wapigwe marufuku kupokea zawadi zozote zenye thamani na kwamba zawadi zote wanazopewa zinatakiwa ziwe mali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliwahi kupokea zawadi ya bonge la dhahabu kutoka mojawapo ya migodi iliyofunguliwa hapa nchini katika miaka ya nyuma; zawadi ambayo aliipokea kama yeye binafsi.
Miezi miwili iliyopita, wakati akiwa ziarani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Kikwete alipewa pia zawadi ya pande la dhahabu lakini yeye hakuichukua moja kwa moja, aliikubali na kuigawa.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya rasimu hiyo ya pili iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, sasa kunatakiwa kuwepo kwa utaratibu maalumu wa namna viongozi wanavyopaswa kupokea zawadi.
Ibara hiyo ya 15 inasema; “Kiongozi wa Umma wakati anatekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi itakuwa ni mali ya Serikali ya Jamhuri na atatakiwa kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara inayohusika,” inasema ibara hiyo.
Kwa ufafanuzi, ibara hiyo inaeleza kwamba wakati wa kuwasilisha zawadi hiyo, mpewa zawadi ni lazima aeleze ni zawadi gani iliyotolewa, thamani ya zawadi hiyo, sababu za kutolewa kwa zawadi hiyo na mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
Ibara ya 16 ya mapendekezo yaliyo katika rasimu hiyo inapendekeza kupigwa marufuku kwa viongozi wa umma kuwa na akaunti katika nchi za nje isipokuwa kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu.
Mapendekezo haya yanakuja katika kipindi ambacho taifa liko kwenye mjadala mzito kuhusu mabilioni ya fedha ambayo yanadaiwa kuhifadhiwa katika nchi mbalimbali za kigeni; huku baadhi ya viongozi wa umma wakituhumiwa kuwa miongoni mwa wenye fedha hizo.
Rasimu hiyo inakwenda mbali zaidi kwa kupendekeza viongozi wa umma kutoomba au kupewa mkopo au riba katika namna ambayo inashusha hadhi ya utumishi wa umma.
Katika Mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilieleza Bunge kwamba yeye ni “fundi wa kukopa”, akisema katika miaka michache iliyopita amechukua mikopo katika benki tofauti hapa nchini.
Urais wa Muungano
Wakati katika utaratibu wa sasa mshindi wa uchaguzi wa Rais ni yule aliyepata kura nyingi kuliko wagombea wenzake, rasimu ya pili inapendekeza kwamba ni lazima mgombea apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa.
Kama ikitokea hakuna mshindi aliyepata alama hizo, rasimu inapendekeza uchaguzi urudiwe katika kipindi cha siku 60 tangu kumalizika kwa uchaguzi wa kwanza na watakaoshindana ni wagombea wawili walioshika nafasi mbili za juu.
Mapinduzi yaliyopendekezwa katika rasimu hii ni yale ya kuruhusu matokeo ya Uchaguzi wa Rais kupingwa mahakamani, tofauti na ilivyo sasa, na mahakama iliyopewa nguvu ya kusikiliza kesi hiyo ni Mahakama ya Juu (Supreme Court).
Kama Mahakama ya Juu itathibitisha kwamba mshindi hakushinda kihalali, uchaguzi huo utarudiwa katika kipindi cha siku 60.
Pia, rasimu hiyo inaeleza kwamba mshindi wa kiti cha urais hataapishwa kushika wadhifa huo katika kipindi cha chini ya siku 30 tangu kutangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi au Mahakama ya Juu.
Rasimu hii ya pili inapendekeza pia kwamba mawaziri wataokuwa wakitumika katika Serikali ya Muungano wasiwe wabunge na kwamba watumike hadi muda wa saa 24 kabla ya kuapishwa kwa rais mpya –Isipokuwa kama wataachishwa mapema kwa sababu zinazofahamika.
Chanzo:- Raia Mwema
No comments:
Post a Comment