ASKARI Polisi wanne na wafanyabiashara wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka mawili ya unyang'anyi wa kutumia siraha, likiwemo la wizi wa zaidi ya Sh milioni 70.
Polisi hao na wafanyabiashara hao, ni E 6396 Coplo Rajabu (39), F 9414 PC Albanus (32), F 9412 PC Saimon (30) na F 9521 PC Selamani (36), Meneja wa Kampuni ya Mafuta GBP, Germano Chaba (30), mfanyabiashara Salum Musa (22) na Bahati Ahmed.
Washitakiwa hao kwa pamoja, walipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana mbele Hakimu Athumani Nyamlani na kusomewa shitaka na Wakili wa Serikali Mmasy Bondo.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba washitakiwa wote hao walitenda kosa hilo Februari 17, mwaka huu, katika eneo la Boko Basihaya, katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wakili Bondo, bila halali, washitakiwa hao kwa pamoja waliiba Sh 77,379,240 mali ya Kampuni ya Mafuta ya GBP Ltd, na kabla na baada ya kukamilisha wizi huo, waliwatishia kwa bastora na panga wafanyakazi wa Kampuni hiyo ili waweze kupata fedha hizo.
Wafanyakazi hao waliotishiwa na watuhumiwa hao, walitajwa mahakamani hapo kwamba ni pamoja na Joyce Paul, Dayana Sosthenes, Ebeneza Godfle na Peter Lawrance.
Washitakiwa hao walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashitaka ulidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe ya kuwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Nyamlani, aliwaambia washitakiwa hao kwamba kesi yao haina dhamana na hivyo watarudishwa rumande hadi Machi 28, mwaka huu, watakapokuja kusomewa maelezo ya dhamana.
Katika hatua nyingine, Polisi E6396 Coplo Rajabu Ugoro (39), F 9414 PC Albanus (32) na wafanyabiashara saba walipandishwa kizimbani mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi nyingine ya unyang'anyi wa kutumia silaha.
Wafanyabiashara hao ni Juma Ngwele (50), Salum Musa (22), Omary Juma (29), Charles Mbwelwa (37), Adam Mkombozi (44), Ally Salum ( 37) na Grald Matutu (36).
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo mbele ya Hakimu Benedictor Beda, kabla ya kusomewa shitaka lao na Wakili wa Serikali, Hilda Kato.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba washitakiwa hao walitenda kosa hilo Machi 9, mwaka huu, katika eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, Dra es Salaam.
Kwa mujibu wa Wakili Kato, washitakiwa hao kwa pamoja, waliiba seti ya televisheni aina ya Samsang yenye thamani ya Sh 800,000, CCTV Camera yenye thamani ya Sh milioni 2.0, Grand Mashine mbili zenye thamani ya Sh milioni moja na kifaa cha gari aina ya Toyota chenye thamani ya Sh 250,000, vyote vikiwa na thamani ya jumla ya Sh.milion 4,050,000, mali ya Hong Biang.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba kabla na baada ya kukamilisha wizi huo, watuhumiwa hao waliwatishia kwa bastola na panga Suza Juan na Nelson William ili waweze kupata vitu hivyo.
Wshitakiwa hao walikana kutenda kosa hilo ambapo upande wa mashitaka ulidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hakimu Beda aliwaeleza washitakiwa hao kwamba shitaka wanalokabiliwa nalo halina dhamana, hivyo watarudishwa rumande hadi Aprili 4, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Polisi wanne hao, watangazwa kufukuzwa kazi hivi karibuni na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kutokana na tuhuma hizo.
Chanzo:- Raia mwema
No comments:
Post a Comment