Ni baada ya wanajeshi kugoma kutii ‘sheria bila shuruti’
MAPAMBANO makali yaliyohusisha risasi za moto yamezuka baina ya polisi na askari wa Jeshi la Ulinzi Tanzania (JWTZ) na kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja na mwingine kujeruhiwa vibaya.
Tukio hilo lilitokea saa 4.30 usiku wa kuamkia jana eneo la Kwa Mrombo, nje kidogo ya jiji la Arusha huku mashuhuda wakidai kuwa lilisababishwa na mwanajeshi mmoja kuporwa mfuko uliokuwa na sare zake.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Jumanne Hamisi, alisema mwanajeshi huyo aliyeporwa (jina lake halikupatikana mara moja), alikuwa kwenye bodaboda akitokea jeshini Monduli; alipofika eneo hilo kibaka mmoja alimpora mfuko uliokuwa na sare za jeshi, ndipo alipopiga simu na kuwaita wenzake waliokuwa kiraia.
“Wenzake walipofika eneo hilo, walianza kutembeza kipigo kikali kwa kila raia aliyekuwapo pale wakiwataka wamtaje kibaka aliyempora mwenzao. Nao wananchi wakawapigia simu polisi. Askari polisi waliwasili na kuwasihi wanajeshi waache vurugu, hawakutii.
"Wanajeshi kadhaa wakwavamia polisi na kuwapokonya bunduki zao, ndipo askari wengine walipoamua kupiga risasi hewani kabla ya kuwalenga wanajeshi waliopora bunduki," alisema shuhuda huyo.
Inasemekana kuwa purukushani kati ya polisi, wanajeshi na raia zilidumu kwa saa nzima hadi pale risasi ilipompata mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni mwanajeshi, aliyefariki papo hapo, na mwingine kujeruhiwa vibaya.
Maofisa wa chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, walithibitisha kupokea maiti ya Joram Myakule (24), mkazi wa Kwa Morombo, mzaliwa wa Kigoma wakati alijeruhiwa hajatambulika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini alidai maelezo zaidi yatatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Hadi tunakwenda mitamboni, Mulongo alikuwa hajapatikana kwani simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokewa, akidaiwa kutingwa na majukum ya kikazi.
Chanzo:- Raia mwema
No comments:
Post a Comment