Ukraine imeripoti kuongezeka kwa magari ya kijeshi katika rasi ya Crimea inayozitenganisha Urusi na Ukraine huku muingilio wa kijeshi wa Urusi ukilaaniwa vikali na nchi za magharibi na kuathiri masoko ya kifedha
Msemaji wa askari wa kulinda mipaka wa Ukraine amesema meli za kivita za Urusi zimeonekana zikiingia na kuzunguka bandari ya mji wa Sevastopol ambako Urusi ina kambi ya jeshi la majini na kuongeza kuwa majeshi ya Urusi yamekatiza mawasiliano ya simu katika baadhi ya maeneo.
Tangu Jumamosi baada ya bunge la Urusi kuidhinisha matumzi ya nguvu za kijeshi katika eneo la Crimea na maeneo mengine ya Ukraine ili kulinda kile ilichokiita maslahi ya Urusi na raia wake,kumekuwa na hali ya taharuki kati ya Urusi na Ukraine na kuzua mihemko barani Ulaya.
Uingereza imesema inatiwa wasiwasi mno na uwezekano wa serikali ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kupeleka majeshi yake katika sehemu nyingine nchini Ukraine mbali na Crimea na kumuonya Putin kuwa Urusi itagharamika pakubwa ikifanya hivyo.
Nchi za magharibi zina wasiwasi
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema muingilio huo wa kijeshi uliofanywa na Urusi nchini Ukraine ndiyo mzozo mkubwa zaidi kuwahi kuikumba Ulaya katika karne hii.
Nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani zimelaani hatua hiyo ya Urusi na kutishia kuichukulia hatua ambazo zitakuwa na athari kubwa kwa Urusi kama kuiwekea vikwazo vya kiuchumi,kuitenga katika safu ya kidiplomasia na kuichukulia hatua za kiulinzi iwapo haitabadilisha mkondo wa mambo yalivyo hivi sasa.
Tayari nchi saba zilizostawi zaidi kiviwanda zimetangaza kujiondoa kutoka mazungumzo ya kuandaa mkutano wa nchi nane zenye nguvu zaidi kiviwandaG8 ikiwemo Urusi ambayo ilipaswa kuwa mwenyeji wa mkutano huo uliokuwa ufanyike mjini Sochi mwezi Juni mwaka huu ili kupinga hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Urusi dhidi ya Ukraine.
Putin hatetemeshwi na vitisho
Licha ya vitisho hivyo vyote kutoka kwa nchi za magharibi na Ukraine yenyewe,Rais Putin haonekani kutetereka au kubadili nia yake ya kuendelea kutuma vikosi vya wanajeshi katika eneo la Crimea.Hii leo wanajeshi wa Urusi wamezizingira kambi kadhaa za kijeshi katika eneo hilo.Urusi ina wanajeshi zaidi ya 6,000 katika eneo hilo.
Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk ameliagiza jeshi la nchi hiyo kuwa katika hali ya tahadhari kuu na kuonya kuwa nchi yake iko karibu kutumbukia katika janga na kuwaomba washirika wake kuisaidia Ukraine.
Na huku Urusi ikionekana kutengwa,waziri wa mambo ya nchi hiyo Sergei Lavrov amesema China inakubaliana nayo kuhusiana na yanayojiri Ukraine.Lavrov aliyesema hayo baada ya kuzungumza na mwenzake wa China Wang Yi kwa njia simu.
Mzozo huo umesababisha masoko ya fedha barani Ulaya kuporomoka huku bei za mafuta na dhahabu zikipanda.Wawekezaji wakuu Urusi wamekumbilia kuuza hisa zao wakihofia kuwa Urusi huenda ikawekewa vikwazo vya kiuchumi.
Na wajumbe wa shirika la fedha la kimataifa IMF wanatarajiwa kuwasili mjini Kiev hii leo kuanza mazungumzo na serikali ya Ukraine kuangazia jinsi ya kuisaidia kiuchumi.Ukraine inahitaji kiasi ya dola bilioni 35 ili kuepuka kufilisika.
Chanzo:- dw.de
No comments:
Post a Comment