MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu Hassan (CCM), amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa bunge hilo.
Uchaguzi huo ulifanyika jana, ikiwa ni siku moja baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo ambapo Mbunge wa Urambo Magharibi, Samuel Sitta, alichaguliwa.
Ushindi wa Samia ulionekana dhahiri kabla ya upigaji kura, kwani mpinzani wake, Amina Abdallah Amour, alijitokeza dakika za mwisho, hivyo hakutoa ushindani mkubwa.
Katika uchaguzi wa jana, Samia ambaye ni Waziri wa Nchi Masuala ya Muungano, Mbunge wa Makunduchi, alishinda kwa kupata kura 390 kati ya kura 523 zilizopingwa dhidi ya mpinzani wake, Amina Abadallah Amour aliyepata kura 126. Kura saba ziliharibika.
Akizungumza baada ya ushindi, Samia alisema atazitumia busara za Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho, kuendesha bunge hilo kwa ufanisi.
Samia alimpongeza Sitta kwa ushindi alioupata juzi na kuahidi kushirikiana naye katika kuhakikisha Watanzania wanapata Katiba mpya wanayotarajia.
Awali wakati wa kuomba kura, Amina alitoa mpya akisema ameachika katika ndoa.
Akijieleza mbele ya wajumbe na kuomba kura alisema: “Waheshimiwa wajumbe mimi ni mama wa watoto watano na kwa bahati mbaya nimeachika.” Hivyo kufanya ukumbi mzima kuangua vicheko.
Hata hivyo, maelezo yake nusura yaibue vurugu wakati wa kuulizwa maswali pale mjumbe mmoja alipotaka ufafanuzi wa kuachika kwake, jambo lililowafanya wajumbe wengi wanawake kuinuka na kupiga kelele, wakidai swali hilo halihusiani na uchaguzi.
Kelele za wajumbe zilimwinua Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho, na kulikataa swali hilo na kutoa nafasi kwa mjumbe mwingine kuuliza swali. Mgombea mwingine, Samia Suluhu Hassan wa CCM alikumbana na swali la mtego lililomtaka ataje mambo mawili aliyojifunza kutoka kwa Mwenyekiti wa muda.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete leo saa nne asubuhi atawaapisha Katibu wa Bunge na Naibu wake, katika Ikulu ndogo ya mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho, baadaye saa kumi jioni Katibu wa Bunge atawaapisha Mwenyekiti wa kudumu na makamu wake, kisha mwenyekiti huyo ataanza kuwaapisha wajumbe wengine.
No comments:
Post a Comment