WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likiwa halijaamua namna gani ya kufanya uamuzi wake katika kupitisha ama kukataa vifungu vya Rasimu ya Katiba inayowasilishwa bungeni leo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, Raia Tanzania inaripoti vifungu 13 nyeti kwa umma endapo vitafanyiwa uamuzi kwa njia ya kura ya siri.
Madhara ya kura ya siri ni kwamba wananchi ambao wanawakilishwa ndani ya Bunge Maalumu hawawezi kujua mwakilishi wao ameamua nini katika maeneo mahsusi, lakini kura ya wazi, mwakilishi anajulikana alichoamua kama kinalinda maslahi ya anaowawakilisha ama la.
Kutokana na ubishi uliojitokeza bungeni miongoni mwa wabunge, kwamba ama Bunge hilo lifanye uamuzi wa kupitisha ibara za Katiba itakayopendekezwa kwa kura ya wazi ama siri, jopo la gazeti hili la Raia Tanzania, limefanya uchambuzi wa baadhi ya ibara za rasimu ya Katiba Mpya na kubaini baadhi ya ibara ambazo ni hatari kuamuliwa kwa njia ya kura za siri.
Ingawa ubishi wa awali kwa wabunge ulijikita zaidi katika uamuzi kuhusu muundo wa Jamhuri ya Muungano (sura ya sita ya Rasimu ya Katiba Mpya) ambayo inaweza kuamuliwa kwa kura ya siri au wazi, kuna ibara nyingine nyeti zinazoweza kunusurika tu endapo kura ya wazi itatumika, kinyume cha hapo, ibara hizo zinazogusa maslahi ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba zitahujumiwa kupitia ‘kichaka’ cha kura ya siri.
Ibara hizo ni 13; 14; 15; 16; 17; 18; 20; 21; 30; 31; 36; 42 na 125. Kwa mfano, ibara ya 31 inazungumzia kuhusu uhuru wa habari na vyombo ya habari, ni rahisi wajumbe kupiga kura ya siri dhidi ya ibara hiyo kwa kadiri ya mtazamo wao na wasijulikane mbele ya wadau wa tasnia ya habari na umma kwa ujumla, lakini kura ya wazi inaweza kuokoa kifungu hicho nyeti kwa taifa.
Ibara hiyo kifungu cha kwanza kinasema; “Kila mtu anao uhuru wa; (a)kutafuta, kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa na (b) kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine ya upashanaji wa habari bila kujali mipaka ya nchi (2)Vyombo vya habari vitakuwa huru na vitakuwa na;- (a) haki ya kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa wanazopata (b) wajibu wa: (i) kusambaza habari na taarifa kwa wananchi na (ii) kuheshimu na kulinda utu, heshima, uhuru na staha ya wananchi dhidi ya habari na taarifa wanazozitumia, wanazozitayarisha na kusisambaza.
Ibara hiyo ya 31 kifungu cha tatu kinasema; Serikali na taasisi zake, asasi za kiraia na watu binafsi watakuwa na wajibu wa kutoa habari kwa umma juu ya shughuli na utekelezaji wa shughuli zao na kifungu cha nne cha ibara hiyo kinasema; Bunge litatunga sheria kwa ajili ya (a) haki na uhuru wa vyombo vya habari na (b) habari na taarifa kwa madhumuni ya usalama wa taifa, amani, maadili ya umma, haki, staha na uhuru wa watu wengine.
Ibara nyingine inayoweza kuhujumiwa kwa kuamuliwa kwa kura ya siri ni 125 hasa kifungu chake cha pili kinachosema; Mtu hatakuwa na sifa za kugombea kuchaguliwa kuwa mbunge ikiwa (a) mtu huyo aliwahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano. Kifungu hiki moja kwa moja kinaingilia sehemu kubwa ya wabunge wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni wajumbe wa Bunge la Katiba, kwa maslahi yao tu, wanaweza kuhujumu kifungu hiki kupitia kura ya siri inayowalinda kutojulikana msimamo wao mbele ya umma.
Ibara ya 42 pia ni nyeti kwa taifa lakini inayoweka hali ngumu kwa watawala na wafanyabiashara katika sekta ya elimu, ibara hii inahusu haki ya elimu na kujifunza.
Ibara hiyo kifungu cha kwanza kinasema; “Kila mtu ana haki ya; (a) kupata fursa ya kupata elimu bora bila vikwazo; (b) kupata elimu bora ya msingi bila ya malipo na inayomtayarisha kikamilifu mwanafunzi ama kuendelea na elimu ya ngazi inayofuata au kuweka msingi wa kuanza kujitegemea; (c) kupata elimu bora inayotolewa nje ya utaratibu wa umma kwa gharama nafuu na (d) kupata fursa sawa ya kupata elimu ya juu ilimradi ana sifa stahiki kupata elimu hiyo bila ubaguzi wa aina yoyote.
Lakini ibara ya 16 inahusu akaunti nje ya nchi na mikopo ikisema kiongozi wa umma; (a) hatafungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu na (b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
Ibara nyingine nyeti zisizostahili kufanyiwa uamuzi wa kupitishwa kwa njia ya kura ya siri ni pamoja na zinazozungumzia dhamana ya uongozi wa umma, kanuni za uongozi wa umma na zawadi katika utumishi wa umma.
Ibara nyingine ni ya 16 inayolazimisha viongozi si tu kutangaza mali zao wakati wanaingia madarakani bali hata wanapoacha madaraka, pamoja na ibara ya 18 inayozungumzia mgongano wa maslahi kwa viongozi na ibara ya 19 inayohusu matumizi ya mali ya umma.
Nyingine ni ibara ya 21 kuhusu utii wa miiko ya uongozi wa umma, ibara ya 128 kuhusu kupoteza sifa za kuwa mbunge, ibara ya 129 kuhusu haki ya wapiga kura kumwajibisha mbunge pamoja na Ibara ya 152 kuhusu uhuru wa Mahakama.
No comments:
Post a Comment