Social Icons

Monday, 17 March 2014

Asilimia 95.5 ya wakazi wa Crimea wataka kujiunga na Urusi

Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wakaazi wa Crimea wamepiga kura ya maoni ya kutaka kujitenga na Ukraine na kujiunga na Urusi, kura ambayo mataifa yenye nguvu duniani yameapa kutoitambua.

Wananchi wa Crimea wakipeperusha bendera

Wananchi wa Crimea wakipeperusha bendera

Maafisa wa uchaguzi wamesema kuwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa kubwa. Vyombo vya habari nchini Urusi, vikiwemo vya serikali, vimeripoti kuwa asilimia 93 ya wapiga kura wameunga mkono hatua ya kujitenga na Ukraine.

Kwa mujibu wa viongozi wa tume ya uchaguzi ya taifa, karibu nusu ya kura zimeshahesabiwa na asilimia 95.5 wamepiga kura ya kutaka kujiunga na Urusi.

Matokeo rasmi kutangazwa leo

Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa leo asubuhi (17.03.2014). Moja ya sababu ya kuwepo matokeo ya upande mmoja, inaweza kutokana na wapinzani kugomea kura hiyo ya maoni.

Waziri Mkuu wa Crimea, Sergei Aksyonov (Mbele), akishangilia baada ya matokeo kutangazwa

Waziri Mkuu wa Crimea, Sergei Aksyonov (Kati), akishangilia baada ya matokeo kutangazwa

Mapema jana mchana (16.03.2014), Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, iliahidi kuwa itachukua hatua dhidi ya Urusi kutokana na kura hiyo yenye utata, ambayo umoja huo na Marekani umesema siyo halali.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana leo Jumatatu, kuamua kama waweke vikwazo vitakavyohusisha marufuku ya kupatiwa visa viongozi wa Urusi pamoja na kuzuia mali zao.

Obama azungumza na Putin

Rais Vladmir Putin na Rais Barack Obama wakizungumza kwa simu

Rais Vladmir Putin na Rais Barack Obama wakizungumza kwa simu

Akizungumza kwa njia ya simu na Rais Vladmir Putin wa Urusi, baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Rais Barack Obama wa Marekani amesema kura hiyo ya maoni imefanyika chini ya shinikizo la Urusi baada ya kuivamia kijeshi Crimea na kwamba kamwe haitatambuliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na jumuiya ya kimataifa.

Rais Obama amesema Marekani na washirika wake wa Ulaya wanajiandaa kuchukua hatua kali dhidi ya Urusi, kutokana na kitendo chake hicho.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE

Chanzo:- dw.de

No comments:

 
 
Blogger Templates