Social Icons

Friday, 18 April 2014

Hii nimeikuta jamii forums: Seif Sharif Hamad ndiye aliyeiba hati ya kuvunja muungano kwa Rais Jumbe na kumpelekea Nyerere


Chaguo la Nyerere la mrithi wa Kawawa lilishutua wengi. Edward Moringe Sokoine, ambaye kabla ya kuteuliwa, alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hakuwa mmoja wa wanafunzi au wafuasi wa Mwalimu; wala hakuwa na jina kwenye duru za siasa kabla ya uhuru. Uteuzi wa Sokoine kwa nafasi ya Waziri Mkuu nusura uvunje Muungano wa Tanzania. Kwa nini?

Rais Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais, aliyechukua wadhifa huo kufuatia kifo cha Mzee Abeid Amani Karume, mwaka 1972; tofauti na Karume, alipania kuimarisha kwa vitendo Muungano kwa kuwa karibu kiutendaji na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Nyerere.

Tena tofauti na Karume, Jumbe aliweza kumwakilisha Nyerere nje ya nchi mara nyingi; alitembea nchi nzima akitoa hotuba ndefu kutetea Muungano na hatimaye kuridhia kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU kuunda CCM, jambo ambalo lisingewezekana enzi za Karume.

Kwa sababu hii, Jumbe alianza kujihesabu kama mrithi halali wa Nyerere asiyeepukika kwa kiti cha Rais wa Tanzania. Jumbe akatumia muda mwingi kwa shughuli za Muungano na kumwakilisha Rais nje; akaitelekeza Zanzibar kwa matarajio ya kuukwaa urais wa Jamhuri ya Muungano.

Nao utendaji kazi wa Sokoine ulianza kujionyesha muda mfupi tu baada ya kuteuliwa. Alijipambanua kama mtekelezaji na mfuatiliaji mzuri wa maamuzi ya Serikali, mkweli na mwenye kujali watu; hasa Wanyonge. Hakupenda kuonea wala kuonewa.

Kwa sababu hii, alipendwa na wengi, hasa watu wa tabaka la chini; kiasi kwamba katika kipindi kifupi Taifa liliimba na kushangilia jina na sifa zake. Nyerere akafurahi na kumweka moyoni.

Habari zikavuja kwamba tayari Mwalimu Nyerere alikuwa amemweka Sokoine moyoni na katika kitabu chake kuwa mrithi wake mtarajiwa baada ya kung’atuka. Naye Jumbe akanusa upepo; uhasama ukaanza kati ya viongozi hao wawili.

Hatua ya kwanza ya Jumbe ilikuwa ni kuhoji mfumo wa uhalali wa Muungano na Sheria iliyouanzisha. Nayo Redio Zanzibar ikadaka haraka wimbo wa Jumbe, kwa kutangaza maneno ya kashfa dhidi ya Muungano kupitia kipindi kilichojulikana kama “Kiroboto Tapes”, au Kanda za Kiroboto.

Na katika Sherehe za Mapinduzi mjini Unguja, Januari 12, 1984 ambazo Mwalimu alihudhuria, Jumbe aliendeleza uchokozi wake wa kuhoji Muungano na kuwataka Wazanzibari watulie wakati akishughulikia suala hilo. Akasema ikibidi angelifikisha kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba ili kupata ufumbuzi.

Hatua nyingine aliyochukua ni ya kumrejesha kwao Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mheshimiwa Damian Lubuva; na badala yake akamteua Al-Haji Bashir Kwaw Swanzy, raia wa Ghana, na rafiki wa Jumbe tangu 1958.

Kisha Jumbe alimwagiza Swanzy kuandaa Hati kupeleka Mahakama ya Kikatiba kuhoji mfumo na uhalali wa Muungano.

Na baada ya hati hiyo kuwa tayari na kuwekwa mezani kwa Jumbe ili aitie sahihi, ilipotea katika mazingira ya kutatanisha, na kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere. Duru zinadai kuwa ni Seif Sharif Hamad aliyepora hati hiyo na kuipeleka kwa Mwalimu.

Mwalimu akachemka, akaitisha kikao cha dharura cha NEC mjini Dodoma ambako Jumbe aliitwa kujibu tuhuma za kutaka kuvunja Muungano. Na baada ya kukiri kuandaa hati hiyo, alivuliwa nyadhifa zote za Chama na Serikali na ikatangazwa “Hali ya kuchafuka kwa hali ya hewa ya Kisiasa Visiwani”.

Mchangiaji wa kwanza:

Ndio ni kweli seif sharif hamad alimchoma jumbe kwa nyerere ,na lengo lake ni kwamba alitegemea kwamba atapewa urais wa zanzibar lakini hakupewa .cha ajabu ni kwamba sasa hivi seif anapiga kelele za kuvunja muungano .but why he didn't support jumbe at that time?well the answer is the guy is a fraud anapenda madaraka .siku zote katika kugombea urais wa zanzibar kwa tiketi ya cuf hamruhusu mtu yoyote kuchukua form .

Mchangiaji wa pili:

..sijui kama wengi wenu mlikuwepo au mnakumbuka mtafaruku wa kisiasa uliosababisha kujiuzulu kwa Makamu wa Raisi wa Muungano na Raisi wa Zanzibar Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi.


..nakumbuka mtafaruku huo ulipelekea mpaka Raisi wa Msumbiji wakati ule, Field Marshal. Samora Moises Machel, kuja Tanzania na kuhutubia Halmashauri Kuu ya CCM.


..Mzee Ali Hassan Mwinyi alichukua nafasi ya Aboud Jumbe -- inasemekana alipendekezwa na Sheikh Thabit Kombo Jecha. Maalim Seif Shariff Hamad aliteuliwa Waziri Kiongozi kuchukua nafasi ya Brigadier.Ramadhani Haji Faki.


..nimeipata makala hii toka gazeti la Raia Mwema, na kuna madai na tetesi kwamba Maalim Seif Sharriff alihusika na kuchomoa toka ofisini kwa Raisi wa Zanzibar makala kesi ya kikatiba dhidi ya serikali ya Muungano.

Mchangiaji wa tatu:

Kilichomponza Jumbe ni udhaifu wake mwenyewe pale aliporuhusu Faki na genge lake kumzidi nguvu. Nakumbuka Jumbe hali ilimuwia ngumu huko akaamua kuja bara na kukaa Musoma Desemba 1983 yote pale Musoma Hotel. Alirejea kwao siku ya sherehe za mapinduzi 1984. Ilikuwa kero hata kwa mzee Mwingira (RC wa Mara wakati huo) kwani pengine kwa hasira za mwalimu, hata gari la ikulu kwa siku zote hizo hakupewa, akawa anatumia la RC.

Hotuba aliyoitoa mwalimu siku ya sherehe za mapinduzi 1984 inaeleza kwa ufasaha kuchukizwa kwake na udhaifu huo wa Jumbe!


                                                              Na Basahama blog

No comments:

 
 
Blogger Templates