Dar es Salaam. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Kuga Mziray amewashauri wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni kuendeleza mchakato wa kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Ukawa ni Muunganiko wa Vyama vya Chadema, CUF, DP na NCCR-Mageuzi vilivyosusia na kutoka nje ya Bunge Jumatano wiki hii kwa kile walichokieleza kutokuridhishwa na mambo yanavyoendelea.
Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha APPT-Maendeleo alisema Katiba itapatikana ndani ya Bunge na siyo nje ya Bunge hilo kama ambavyo Ukawa wamefanya.
“Hakuna lolote watakalolifanya, hao Ukawa hawatafika popote na kinachoangaliwa hapa ni jinsi gani Wazanzibari watarejea bungeni ili kuipata theruthi mbili kutoka Zanzibar, kwani Bara hakuna shida,” alisema Mziray.
Alisema uamuzi wa Ukawa hauna tija kwa Watanzania kwani wanachohitaji ni kuona Katiba Mpya inapatikana na siyo kinyume chake,” alisema.
Mwenyekiti huyo ambaye chama chake hakiko Ukawa alisema, Wazanzibar wanaitumia Ukawa ili kupata muundo wa muungano wa serikali ya mkataba na siyo lolote.
Ukawa baada ya kutoka bungeni wemetangaza kuzunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara kuwaeleza wananchi kwa nini walitoka bungeni.
Hata hivyo mkutano wa Ukawa uliopangwa kufanyika Zanzibar wiki hii umepigwa marufuku na polisi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment