Urusi imeviondowa vikosi vyake mpakani na Ukraine na kuihakikishia Marekani kwamba haitoivamia Ukraine hatua ambayo inakuja wakati Marekani na Umoja wa Ulaya zikiiwekea vikwazo vipya Urusi kutokana na dhima yake Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu (katikati) akitembelea kambi ya kikosi cha wanamaji cha Urusi kilioko mashariki mwa Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema vikosi vya Urusi ambavyo vilikuwa vikifanya mazoezi ya kijeshi karibu na mpaka wa Ukraine vimeondolewa.
Shoigu ametowa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake ya simu na waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel. Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Adimeri John Kirby amesema katika taarifa kwamba mawaziri hao wawili wamejadili masuala mbali mbali kuhusiana na hali ya Ukraine ambapo Hagel alisisitiza kupatiwa ufafanuzi juu ya dhamira za Urusi mashariki ya Ukraine.
Hagel ametowa wito wa kukomeshwa kwa ushawishi wa Urusi ndani ya Ukraine unaoidhoofisha nchi hiyo na kuonya kwamba kuendelea kwa vitendo vya uchokozi kutazidi kuitenga Urusi na kuepelekea shinikizo zaidi la kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.
Suala la wakaguzi wa OSCE
Vyacheslav Ponomaryov meya wa kujitagazia wa mji wa Slaviansk aliyesimama (kulia) akiwatambulisha wakaguzi wa OSCE kwa waandishi wa habari.
Hagel pia ameitaka Urusi kusaidia kuachiliwa kwa wakaguzi saba wa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya OSCE wanaoshikiliwa mashariki ya Ukraine.
Aliyejitangatza kuwa meya wa mji wa Slaviansk unaoshikiliwa na wanaharakati wanaotaka kujitenga mashariki ya Ukraine Vyacheslav Ponomaryov ameliambia shirila la habari la Urusi Interfax kwamba kuwekwa kwa marufuku ya viza na kuzuiliwa kwa mali dhidi ya Denis Pushlin kiongozi wa jimbo lililojitangaza kuwa Jamhuri ya Donetsk na Andrei Purgin kiongozi mwengine wa mashariki ya Ukraine hakutoleta tija ya kufanyika mazungumzo ya kuwaachilia wakaguzi hao wa OSCE.
Amesema atakubali kuzungumzia juu ya kuachiliwa kwa wakaguzi hao wa kijeshi na mataifa ya magharibi iwapo tu Umoja wa Ulaya utaachana na mpango wa kuiwekea vikwazo waasi wa Ukraine.
Vikwazo dhidi ya Urusi
General Walery Gerasimow Mkuu wa Majeshi ya Urusi (kulia) katika mkutano na Rais Vladimir Putin wa Urusi (katikati) na Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu (kushoto).
Hapo jana Marekani imetangaza kuwawekea vikwazo maafisa saba wa serikali ya Urusi na makampuni 17 yenye uhusiano wa karibu na Rais Vladimir Putin wa Urusi,wakati wa Umoja wa Ulaya umetangaza leo hii kwamba inaweka marufuku ya viza na kuzuwiya mali dhidi ya maafisa tisa wa serikali ya Urusi na viongozi sita wa wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi nchini Ukraine.
Watu mashuhuri walioko kwenye orodha hiyo ya vikwazo ni pamoja na Dmitry Kozak naibu waziri mkuu ambaye anashughulikia suala la kujumuisha jimbo la Crimea nchini Urusi,Valery Gesasimov mkuu wa majeshi ya Urusi na Igor Sergun mkuu wa shirika la siri la kijasusi la kijeshi nchini Urusi.Katika orodha hiyo pia yumo Oleg Belaventsev mwakilishi binafsi wa Rais Putin kwa Crimea.
Serikali ya Urusi imeapa kwamba itachukuwa hatua kali kukabaliana na vikwazo viliyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo.Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov amesema kwamba serikali ya Urusi imechukizwa na hatua ya serikali ya Marekani ambayo inaonyesha kwamba nchi hiyo haifahamu kabisa hali halisi ya kile kinachotokea Ukraine.
No comments:
Post a Comment