Social Icons

Saturday 10 May 2014

Boko Haram yaua watu wengine 300

Kundi la Boko Haram nchini Nigeria limeuwa watu wengine zaidi ya 300 kaskazini mwa nchi, na nchi zaidi zenye nguvu duniani, zikiwemo Marekani na China zimejiunga na juhudi za kuwatafuta wasichana waliochukuliwa mateka.

Mojawap ya maeneo yaliyoshambuliwa na Boko Haram katika mji wa Maiduguri

Mojawap ya maeneo yaliyoshambuliwa na Boko Haram katika mji wa Maiduguri

Juhudi hizo zinafanyika wakati ambapo kundi hilo pia limewaua mamia ya watu wengine kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, wiki hii. Huku kukiwa na hasira kutoka duniani kote, Marekani, Uingereza na Ufaransa, zinapeleka timu za wataalamu kuisaidia Nigeria katika juhudi za kuwakomboa wasichana hao.

China imeahidi kutoa taarifa zozote muhimu zitakazopatikana kwenye picha za satelaiti zake na idara za kijasusi kwa serikali ya Nigeria. Rais Barack Obama wa Marekani, amesema kitendo hicho kinasikitisha na kwamba timu ya watalamu wa kijeshi imepelekwa Nigeria kutoa msaada.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron amelaani vikali utekaji nyara huo uliofanywa na Boko Haram, Aprili 14.

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria

Cameron amesema timu ndogo ya wataalamu wa mipango na uratibu itakwenda nchini Nigeria mapema iwezekanavyo.

Jana (07.05.2014) Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan ameukubali msaada huo uliotolewa na mataifa hayo ya Magharibi. Serikali ya Rais Jonathan imekosolewa vikali na wanaharakati pamoja na wazazi wa wasichana hao, jinsi inavyolishughulikia suala hilo. Jana polisi wa Nigeria waliahidi kutoa Dola laki tatu kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana wanafunzi hao wa kike.

Watu 300 wauawa

Hata hivyo, wakati juhudi za kuwaokoa wasichana hao zikiendelea, imeripotiwa kuwa wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu wamewaua watu 300 nchini Nigeria kwenye mji ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Cameroon. Kundi la Boko Haram limesema kuwa liliwafyatulia raia risasi kiholela wakati wakijaribu kuukimbia moto uliowashwa kwa makusudi kwenye mji wa Gamboru Ngala, katika jimbo la Borno.

Inaaminika kuwa watu hao waliokuwa na silaha, walilivamia eneo hilo na kulichoma moto. Seneta wa eneo hilo, Ahmed Zannah, amesema kiasi watu 300 wameuawa katika shambulio hilo lililotokea baada ya wanajeshi wa serikali kuondolewa katika eneo hilo na kupelekwa karibu na mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri, katika harakati za kuwakomboa wasichana wanaoshikiliwa mateka.

Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau

Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau

Zannah amesema hali hiyo imesababisha eneo la Gamboru Ngala kutokuwa na ulinzi wa kutosha. Jeshi la Cameroon limeimarisha ulinzi kwenye eneo la Fotokol, lililoko kwenye mpaka na Nigeria.

Siku ya Jumanne, wasichana wengine wanane walitekwa nyara na watu wenye silaha katika kijiji cha Warabe, kaskazini-mashariki mwa Nigeria. Akizungumza katika mkanda wa video siku ya Jumatatu, kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, alisema wasichana hao wanashikiliwa kama watumwa kwa ajili ya kuuzwa.

Juhudi za kuwakomboa wasichana hao zinafanyika wakati ambapo Kongamano la Kimataifa kuhusu Uchumi wa Afrika, likiwa limefunguliwa rasmi jana, kwenye mji mkuu wa Nigeria, Abuja. Rais Jonathan amesema ana matumaini kwamba kongamano hilo litaonyesha maendeleo ya uchumi wa Nigeria.

Chanzo: dw.de


No comments:

 
 
Blogger Templates