Social Icons

Monday, 19 May 2014

Dr Slaa ataka Ukawa iungwe mkono



Arusha. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amewataka Watanzania kuungana na kutetea Rasimu ya Katiba Mpya.

Kadhalika, amewataka wananchi kuiunga mkono Ukawa katika harakati za kuleta mageuzi yenye tija kwa Watanzania.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Uwanja wa Kilombero, Samunge jana akiwa sambamba na viongozi wa CUF na NCCR Mageuzi, Dk Slaa alisema kujadili bungeni rasimu nyingine tofauti na iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni makosa.

“Msikubali tena mabilioni ya fedha zenu kuendelea kutumika kuwalipa wabunge ambao hawajadili mawazo yenu,“ alisema.

Alisema ni hatari kwa Taifa iwapo viongozi wa juu serikalini watapuuza maoni ya wengi.

“Viongozi wajifunze mambo yaliyotokea Kaskazini mwa Afrika. Tusipuuze maoni ya wengi ni hatari kwa nchi,” alisema.

Alisema Ukawa hawatarudi bungeni hadi Serikali ya CCM ikubali kujadili mawazo yaliyopendekezwa kwenye Tume ya Marekebisho ya Katiba.

“Waache lugha ya matusi na kejeli, tunataka tujadili kile ambacho wananchi wengi wamependekeza,” alisema Dk Slaa. Akifafanua muundo wa Serikali, Slaa alisema uamuzi wa kuwa na muundo wa serikali tatu ni mawazo ya wengi na unapaswa kuheshimiwa.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates