Waasi wanaotaka kujitenga wameendelea kupiga kile wanachokiita kura ya maoni mashariki mwa Ukraine wakati mapigano yakizuka upya katika mzozo unaotishia kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuigawa nchi hiyo.
Mataifa ya magharibi yenye kuiunga mkono serikali ya Ukraine katika mzozo wake na waasi wanaoiunga mkono Urusi wamesisitiza kwamba hicho kinachoitwa kura ya maoni iliopigwa Jumapili (11.05.2014) kuhusu mamlaka ya kujitawala kwa majimbo ya Donetsk na Lugansk sio halali na haitotambuliwa.
Mapigano ya hapa na pale yamezuka upya mapema leo hii wakati waasi wenye silaha nzito walipojaribu kuudhibiti tena mnara wa TV ulioko kwenye vitongoji vya mji wenye vurugu wa Slavyansk.Kulikuwa pia na hali kubwa ya mvutano katika maeneo mengine.
Katika miji zaidi ya kumi na mbili ambayo inashikiliwa na waasi, wapiga kura walipiga misururu kwa utulivu kupiga kura zao. Wengi walipiga kura ya "ndio " kwa suala lililowauliza unapendelea kuwa na uhuru kwa Jamhuri ya Watu wa Donetsk ? Hali ilikuwa hivyo pia katika jimbo la jirani la Lugansk.
Kura ya ndio
Wakaazi wakiwa katika misururu ya kupiga kura katika mji wa Mariupol mashariki ya Ukaraine. (11.05.2014)
"Nataka kuwa huru kutoka kwa kila mtu."amesema hayo mfanyakazi wa viwandani Nikolai Cherepin wakati alipopiga kura yake ya "ndio" katika mji wa Mariupol ulioko kwenye jimbo la Donetsk.Ameongeza kusema " Yugoslavia ilivunjika na hivi sasa wanaishi vizuri."
Zhenya Denyesh mwanafunzi wa miaka 20 ambaye alikuwa mtu wa pili kupiga kura yake katika jengo la chuo kikuu la ghorofa tatu amekaririwa akisema " Sote tunataka kuishi kwenye nchi yetu wenyewe."
Alipoulizwa kitafuatia nini baada ya kura hiyo iliyoandaliwa kwa haraka na waasi katika kipindi cha wiki chache tu amejibu " Itakuwa bado ni vita".
Katika mji wa Mariupol ambapo wiki iliopita kulikuwa na mapigano makali,maafisa wamesema kulikuwa na vituo vinane tu vya kupigia kura kwa ajili ya watu nusu milioni ambapo misururu ya wapiga kura ilikuwa mirefu sana.
Msemaji wa "Jamhuri ya Donetsk" Kiril Rudenko amesema idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura hiyo kufikia mchana katika mji mkuu huo wa jimbo wenye wakaazi nusu milioni moja ilikuwa asilimia 30 ambayo ni kubwa kuliko waliokuwa wameitegemeaAmeongeza kusema kwamba hakuna tukio la vurugu lililoripotiwa wakati wa kura hiyo.
Haina taathira ya kisheria
Lakini baadhi ya wakaazi wa mashariki ya Ukraine hawaungi mkono kura hiyo inayowahusu watu milioni saba wanaoishi katika majimbo mawili kati ya watu milioni 46 wa Ukraine.
Mkaazi mmoja wa Donetsk, Anatoli Kozlovsky amesikika akilalama kwamba "Ni hatua isio halali inayotekelezwa na kundi la watu wasiojulikana ambao wameyanyakuwa majengo ya serikali na kuzunguka na silaha mkononi
Serikali ya Ukraine pia ilikuwa na matamshi makali.
Wizara yake ya mambo ya nje imesema katika taarifa kwamba wandaaji wa uhalifu huo wa kipuuzi wamekiuka katiba na sheria ya Ukraine.
Taarifa hiyo imeongeza kusema kura hiyo"imechochewa, imeandaliwa na kugharamiwa na serikali ya Urusi" na kuitangaza kuwa "haitokuwa na taathira ya kisheria kwa mamlaka ya dola ya Ukraine."
Mkuu wa Utumishi katika ofisi ya rais Sergiy Pashinskiy amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kiev kwamba hiyo sio kura ya maoni bali ni jaribio la aibu la magaidi na wauaji kuwatumia wananchi wa mikoa ya Donetsk na Lugansk kuficha uhalifu wao.
Marekani na Umoja wa Ulaya pia zimetilia mkazo msimamo wao kwamba kura hiyo ya maoni sio halali.Zina wasi wasi kwamba eneo la mashariki litakalokuwa limejitenga linaweza kuvuruga mipango ya kufanyika kwa uchaguzi wa rais wa nchi nzima hapo Mei 25 ambao unaonekana kuwa muhimu katika kurudisha utulivu nchini humo.
Kuunda taasisi na jeshi lao
Kiongozi wa waasi katika jimbo la Donetsk amesema itaunda taasisi zake zenyewe za taifa na itawachukulia wanajeshi wa serikali walioko katika jimbo hilo kuwa wanalikalia kwa mabavu jimbo hilo mara tu baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kile wanachokiita kura ya maoni ya Jumapili.
Shirika la habari la Urusi Interfax limemkariri Denis Pushilin kiongozi wa jimbo lililojitangaza kuwa Jamhuri ya Donetsk akisema " Vikosi vyote vya kijeshi katika ardhi yetu vitachukuliwa kuwa sio halali na kutangazwa kuwa wanaikalia ardhi kwa mabavu mara tu baada ya kutangazwa rasmi kwa matokeo ya kura hiyo ya maoni.
Rais Vladimir Putin wa Urusi amejitenganisha hadharani na kura hiyo ya maoni na kutowa wito wa kuahirishwa ambao umepuuzwwa na waasi.
Lakini Marekani na Umoja wa Ulaya bado wanaona kuna mkono wa Putin katika machafuko yanayotokea mashariki ya Ukraine tokea mwezi wa Aprili na zinaamini kwamba anataka kurudia kufanya kile kilichopelekea Urusi kulinyakuwa jimbo la Crimea hapo mwezi wa Machi.
Iwapo uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika katika kipindi cha wiki mbili zijazo utachafuliwa ,Marekani na Ulaya zimeonya kwamba zitaweka vikwazo vitakvyoleta athari kwa sekta kubwa ya uchumi wa Urusi.
Chanzo: dw.de
No comments:
Post a Comment