Social Icons

Saturday, 17 May 2014

UKAWA WAKUTANA NA NGUVU YA UMMA MAFINGA

Baadhi ya mabango yanayopinga harakati za Ukawa yakioneshwa katika mkutano huo

Wakiwa na mabango yao mbele ya askari wa FFU

Profesa Lipumba akisisitiza jambo katika mkutano wake huo

Winfreda Ngoti akiuliza swali katika mkutano huo
UMOJA wa katiba ya Wananchi (Ukawa) umepokewa kwa mabongo yanayosisitiza umuhimu wa serikali mbili katika mkutano wao uliofanyika jana, mjini Mafinga.

Ukiwa na wazee na wanawake wachache, mkutano huo uliohudhuriwa na vijana wa kiume zaidi ulihutubiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa.

Wengine waliohutubia ni pamoja na mwakilishi wa chama cha NCCR-Magezuzi, Danda Juju na kiongozi wa taasisi ya kiislamu ya Shura ya Imamu, Rajabu Katimba.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na vijana hao yalikuwa na ujumbe uliosomeka “vijana Mafinga tuna mashaka na ndoa ya Ukawa, watauza nchi” na bango la waendesha bodaboda lilisomeka “ Rudisheni posho kwanza mjengoni dodoma.”

Mengine na ujumbe wake kwenye mabano ni lililowatambulisha wafanabiashara wa sokoni lililosomeka “Mafinga Sokoni, serikali tatu sio suluhisho la matatizo ya wananchi”, na la wapiga debe Mafinga stendi lilisomeka “Karume Oyee, Nyerere Oyee, Muungano Saafi.”

Bango la waliojitambulisha kuwa ni machinga lilisomeka “tunataka serikali inayojali wajasiliamali, sio kujali matumbo yao”, na lile la wakulima lilisomeka “kilimo kwanza, utaifa kwanza.”

Wakati mabango hayo yakizungushwa katika mkutano huo muda ambao Profesa Lipumba alikuwa akihutubia, usikivu ulipotea kwa dakika takribani 15 hadi 20 baada ya sehemu ya kundi la vijana lililokuwa likimsikiliza kuelekea upande waliokuwa vijana wenye mabango hayo.

Polisi waliokuwepo walilazimika kuingilia kati kadhia hiyo na mzozo baina yao na vijana waliokuwa na mabango hayo ulisikika.

Mmoja wa Polisi aliyekuwa akiwatuliza vijana hao alisema “Jamani huu ni mkutano halali wa kisiasa, achene wenzenu wafanye mkutano wao; yatoeni mabango yenu.”

Mmoja wa vijana aliyekuwa amebeba bango mojawapo jina halikupatikana mara moja alisikika akisema “Ukawa sio chama cha siasa, wao wana mtazamo wao na sisi tuna mtazamo wetu, kwahiyo sio jambo la ajabu wakajua kwamba Mafinga wengi hatuwaungi mkono na sio dhambi kuonesha hisia zetu katika mkutano wao.”

Akielezea vurugu hizo, Profesa Lipumba alisema zinafanywa na vijana waliotumwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwasababu ya msimamo wao wa kutaka serikali mbili, tuhuma zilizokanushwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu aliyehojiwa baaada ya mkutano huo.

“Siamini kama mkutano huu ungekuwa unahutubiwa na Mwenyekiti wa CCM wa Taifa Jakaya Kikwete wangekuja na mabango hayo na kufanya vurugu hizi?” alisema na sauti kutoka kwa baadhi ya vijana hao zikasikika zikisema.

“Kama angekuja na msimamo wa serikali tatu ni lazima angekutana na mabango haya; sisi tunataka serikali mbiliii.”

Hata baada ya vurugu hizo kupoa na Profesa Lipumba kuruhusu maswali baada ya kufafanua sababu mbalimbali zilizosababisha wasusie bunge la Katiba na kuanzisha Ukawa, mkutano huo ulitaka kuvurugika tena.

Swali lililotaka kuuvuruga mkutano huo lilitoka kwa kijana aliyejitambulisha kwa jina la Rashid; Rashid alitaka kujua kwanini CCM hawapo katika umoja huo.

Pamoja na vijana wengine kupiga kelele wakiashiria kwamba hilo sio swali, Profesa Lipumba alijibu akisema ni swali zuri.

Alisema milango ya Ukawa ipo wazi kwa mtu yoyote ndani nan je ya bunge la Katiba wakiwemo wabunge na viongozi wa CCM.

“Tutafurahi kuwapata wana CCM, tunawakaribisha Ukawa ili kwa pamoja tushirikiane kupata Katiba inayotokana na wananchi,” alisema.

Mwingine aliyeuliza swali alikuwa Winfreda Ngoti aliyesema harakati za kudai serikali tatu hazitakuwa na maana yoyote kama matatizo ya wananchi hayatashughulikiwa.

“Watanzania wana matatizo lukuki, vituo vya huduma za afya havina wataalamu, dawa, wakulima hawapati pembejeo kwa wakati na bei zake ni kubwa, wafanyabishara wadogo wanabanwa na kukamuliwa kodi, walimu hawapati mishahara kwa wakati, askari wana mishahara midogo na wanakula rushwa,” alifafanua.

Katika majibu yake, Profesa Lipumba alisema hayo yote yatafanyiwa kazi kukiwa na Katiba bora itakayosisitiza uwajibikaji na uadilifu.

Alisema rushwa na ufisadi vimekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya taifa hili katika sekta zote zikiwemo elimu, afya, kilimo, biashara, miundombinu na zinginezo.

No comments:

 
 
Blogger Templates