Social Icons

Monday, 14 July 2014

CCM ikiiwezesha UVCCM itafika mbali




NA GORDON KALULUNGA

KUNA msemo unatumika na watu wa nyikani kuwa, mtu ambaye haonekani kwenye shamba la karanga, hawezi kuonekana kwenye shamba la Mpunga.

Julai 6, mwaka huu, ilikuwa ni siku ya historia kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya.

Historia hiyo ilijikita katika tukio la kuapishwa makamanda wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi. (UVCCM).

Tukio hilo lilifanyika katika uwanja wa CCM Ilomba, Jijini Mbeya. Mgeni rasmi alikuwa ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa, Jerry Silaa, ambaye pia ni Meya wa manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

UVCCM imeutambua msemo wa watu wa nyikani. Sasa wamesikia. Wameona. Wamegusa na kunusa.

Wameanza kuonekana kwenye shamba la karanga ili baadae waonekana kwenye shamba la Mpunga.

Makamanda walioapishwa siku hiyo walikuwa ni Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Yona Sonelo, Kamanda Wilaya ya Mbozi, Ibrahim Sanga, kamanda Wilaya ya Chunya, Philipo Mulugo, kamanda wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, Oran Njeza na kamanda wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Tonebu Chaula.

Ambao hawakufika ni kamanda wa Ileje, John Cheyo, kamanda wa wilaya ya Rungwe, Richard Kasesela, wilaya ya Momba, Twaha Kilabeba, Mbarali, Ibrahim Mwakabwanga na Kyela Elius Asangalwisye.

Baada ya uapishwaji wa makamanda hao, ulifanyika mkutano wa hadhara katika viwanja hivyo.

Kabla ya kuapishwa makamnada hao, kulitanguliwa na Baraza kuu la mkoa Julai 5, mwaka huu, ambalo mgeni rasmi alikuwa ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Ndugu, Bashiru Madodi, akitoa nasaha zake kwa vijana alisema, tatizo kubwa la baadhi ya vijana walioko katika UVCCM wanatumika vibaya na watu wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama katika uchaguzi mkuu wa mwakani na kuacha kufuata taratibu za chama na kutembea na wagombea mifukoni, kiasi cha kuanza kutoa matamko ambayo yalitakiwa kutolewa na chama. 

Ndugu Madodi aliwaonya vijana kuacha tabia hiyo kwani inakivuruga chama na kuwavuruga wanachama na wananchi kwa ujumla, aliwataka vijana kutoa matamko yanayohusu uendeshaji wa jumuiya yao na si masuala yanayohusu utendaji wa CCM.

Pia Ndugu Madodi aliwakumbusha vijana kuwa wakiendelea na tabia hiyo yanaweza kuwakuta yaliyowakuta vijana wakati wa uongozi wa Guninita ya kufutwa uongozi wote wa makao makuu ya jumuiya na kubaki mikoani, katika wilaya na kata.

Mwisho aliwataka Vijana kusubiri Chama kitoe matamko na wao waingie uwanjani kukitafutia ushindi chama dhidi ya vyama vingine vya siasa.

Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Mbeya kutoka wilaya ya Momba Mbeya, Hassan Nyalile, anasema, anaunga mkono kauli ya Madodi na kusema kuwa kauli aliyoitoa ni ya kiungozi na kwamba Makonda anatakiwa kujirekebisha na kurudi kwenye majukumu yake.

“Makonda anatakiwa atafsiri vema kauli ya Madodi na kurejea kwenye misingi ya kanuni ili aweze kufanya vema kazi za jumuiya yake ya watoto badala ya kila wakati kuinuka na kutoa matamko ambayo yanaashiria yupo na kiongozi mmoja mfukoni kutafuta nafasi ya Rais mwaka 2015”

Kwa upande wake, Paul Makonda ambaye alikuwepo kwenye Baraza hilo, ndiye aliyeanza kueleza kuwa vijana wapo ndani ya mifuko ya wanasiasa wakubwa, ndiyo maana inafikia mahala chama hakiwaamini.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, anasema vijana wangoje chama kitoe maamuzi kwanza ya mgombea nafasi ya Urais ndipo wamuunge mkono, badala ya kugawanyika kwa sasa.

Katibu wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Said Yasin, anasema umoja ndiyo kila kitu katika kufanikisha ushindi wa chaguzi zijazo, yaani uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2015.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo chakula na ushirika, Godfrey Zambi, anapongeza kamati ya utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Mbeya, kwa kuendeleza kudumisha muungano kwa kuwaalika viongozi wengine wa umoja huo kutoka mikoa mingine ya Tanzania Bara na visiwani.

“Si vibaya ili kuendelea kudumisha muungano kuendelea kuoleana. Nawaagiza makabitu wote kuacha tabia ya kutumia magari haya katika kazi zao binafsi kama kwenda harusini,kanisani,sokoni ili hali kuna shughuli za chama,vijana iwapo mtanyimwa gari na katibu yeyote kwa shughuli ya chama nipigieni simu mimi moja kwa moja,”anasosoyiza Zambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki.

Leo sauti ya nyikani haitajadili suala la Baraza hilo wala Mkutano wa hadhara, lakini baadhi ya vijana wanaelezea kuhusu taasisi yao hiyo.

Sauti ya Katibu wa UVCCM wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, George Silindu, inasema kuwa, CCM ina jambo la kujifunza kutokana na mkutano huo wa Jumuiya yake.

Anasema ukubwa wa mkutano huo na uwingi wa watu waliojitokeza, ni funzo kwa chama, kwa madai kuwa ushirikishwaji wa uandaaji mikutano ni jambo jema.

Anafafanua kuwa baadhi ya mikutano ya CCM haina mwitikio kutokana na ukiritimba wa mgawanyo wa kazi za uandaaji wa mikutano hasa zile zinazohusu fedha.

“Katika mkutano wetu vijana kulikuwa na vyombo vyote vya habari, kamati ya utekelezaji ilishirikisha wajumbe mbalimbali, wakiwemo watendaji na wenyeviti,katika maandalizi na ndiyo maana mkutano ulifana kuliko hata wa miaka 37 ya CCM Taifa” anasikika Silindu.

Anaelezea mikakati ya wilaya yake kuwa baada ya kumpata kamanda wao wa vijana, wana mikakati ya kuhakikisha vijana wa wilaya hiyo wanakuwa nuru kwa chama na jamii ya watanzania.

Anasema, vijana wengi waliopitia katika tanuru la UVCCM na kuteuliwa katika ngazi za chama na serikali, hawapati shida katika kuongoza, tofauti na wale ambao hawajapitia katika jumuiya hiyo.

Kamanda wa UVCCM wilaya ya Mbozi, Ibrahim M. Sanga, anapaza sauti yake kuwa, licha ya yeye kutokuwa mwanasiasa wa majukwaani, anawapenda vijana.

Anasema, vijana wakipata ajira chama hicho kitakuwa salama.

Anaeleza mikakati ya kuwainua vijana kiuchumi kuwa ni kuunganisha nguvu na mawazo ya vijana na wadau wengine ndani na nje ya wilaya ya Mbozi, kutengeneza mradi ambao utawapatia vijana ajira.

“Tutakuwa wilaya ya mfano kwa vijana wa chama mkoani Mbeya, kupata ajira kupitia mradi tutakaoutengeneza, na hiyo itakuwa chachu ya vijana kukipenda chama na nchi yao’’ anasema Kamanda huyo wa vijana wa wilaya ya Mbozi.

“Utakuta wamekwenda kukitumikia chama na wanarudi bila chochote kwa ajili ya maisha yao ya kila siku, ndiyo maana wanahamia vyama vingine na kuishi kwa matumaini kuwa huenda kuna siku vyama hivyo vitapata madaraka na wao wakapata chochote’’ anasema Ibrahim Sanga.

UVCCM ni tanuru la uongozi wa serikali na CCM.

Pamoja na ukweli huo na chama hicho kinavyoamini, vijana hao wanapaswa kupata mafunzo kadhaa.

Chama hicho kione umuhimu wa dhahabu hii ya vijana ambao wapo kwenye tanuru la uongozi, kupatiwa mafunzo ili wajitambue.

Mafunzo ambayo wanapaswa vijana wa UVCCM, wajifunze ni maadili na nafasi ya vijana katika mapambano ya rushwa, nadharia ya chaguzi za dola katika mfumo wa vyama vingi na uhusiano kati ya CCM, UVCCM na serikali.

Mada zingine ziwe ni zile zinazolenga umuhimu wa matumizi ya vyombo vya habari na sanaa katika chaguzi, ujasiri na maarifa ya uhai wa UVCCM, mawasiliano na uandishi wa utunzaji wa kumbukumbu.  

Chanzo: Kalulunga blog.

No comments:

 
 
Blogger Templates