Social Icons

Thursday, 10 July 2014

Tatizo la uoga kwa Watanzania

KATIKA toleo la hivi karibuni kwenye gazeti hili, ndugu yangu na mwandishi ninayeheshimu sana makala zake, Sylvester Hanga, aliandika makala yenye kichwa: ‘U-mungu mtu wa CCM unalifukarisha Taifa’. Katika makala hiyo akalinganisha Watanzania walivyo waoga na jinsi Wakenya, Wamalawi na raia wa Jumuia ya Ulaya (EU) jinsi wasivyo waoga.

Nikiri kwamba nakubaliana naye kuwa Watanzania ni waoga, na kama kungekuwa na World Cup ya waoga, nadhani timu yetu ingeshiriki kila WORLD COWARDS WORLD CUP! Na huenda ‘Shirikisho la Watu Waoga Duniani’ lingetuteuwa kuwa waandaaji wa kwanza wa hiyo World Cup! Pia nikiri kuwa nakubaliana naye kuwa uoga huu uliokithiri umezalisha miungu watu nchini. 

Si madhumuni yangu kumkosoa ndugu Hanga bali kujaribu kuelezea ni kwa nini Watanzania wanaonyesha kiwango kikubwa cha uoga ukilinganisha na Wakenya, Wamalawi, raia wa EU, na kwa hakika kushinda raia wa nchi nyingi nyinginezo.

Ukitaka kujua kiwango cha uoga wa Watanzania, angalia mfano huu: Pale Nairobi polisi mmoja mwenye kirungu hathubutu wala akili haiwezi kumtuma aende mitaani akamate msururu wa watu, awafunge mashati na awaswage kituoni kama mbuzi wa hitima! Pale Nairobi askari akiwa zuzu akafanya hivyo inaweza hiyo ndio ikawa kazi yake ya mwisho duniani!

Kwa Dar es Salaam yetu, mambo ni tofauti!  Unaweza kuona polisi mmoja (tena dhaifu hivi) kawafunga watu mashati, akawaweka chini ya nguzo ya umeme, akaenda kukamata wengine, akarudi, akawajumuisha na kuondoka nao!

Sanasana utawaona wakiomba ‘msamaha’ toka kwa huyo polisi mwenye kirungu! Msamaha usipotolewa atatinga nao kituoni wawe wana makosa au la! Na wakifika kituoni, hawasemi hawana makosa, hapana! Wanaanza kuomba, kuomba na kuomba! Na hatimaye wanaishia kutoa pesa ili waachiwe! Kinachofuata si kudai fidia kwa kukamatwa bila makosa bali ni kujihadhari wasikamatwe tena!

Nimewahi kuishi jijini Dublin kule Ireland na Washington DC kule Marekani. Pale Dublin kuna kitongoji kinaitwa Sheriff. Hiki ni kitongoji ambacho polisi hawaendi mpaka wawe kamili! Wakienda hovyo hawarudi bila ngeu!

Pale Washington DC eneo la Kusini Mashariki polisi hawaendi bila kujiandaa kisawasawa! Hili ni eneo ambalo watumishi wa serikali wanapewa posho ya ziada ili wakubali kufanya kazi huko!

Sijatoa mifano hii eti kwa kuwa nashabikia uhalifu! La hasha! Mimi ni muumini wa kutii sheria, lakini kutii sheria hata pale haki zako kama raia zinapovunjwa ni uzuzu wa hali ya juu! Kwa hakika, ni uvunjifu wa sheria!

Haijalishi ni nani anavunja haki zako. Raia mwema anawajibika kuripoti (hata kuzuia) uvunjifu wa sheria. Tabia hii ya kutii sheria kizuzu imechochea tabia ya vyombo vya dola kuendelea kuvunja haki za binadamu kwa kiwango cha kutisha!

Na haki za binadamu zikivunjwa kwa kiwango cha kutisha husababisha UOGA unaokera! Hata hizo sehemu nilizotolea mifano chanzo cha watu kujikita  katika kulinda haki zao kwa njia za kihalifu ilikuwa ni kutokana na uvunjifu wa haki za raia uliofanywa na vyombo vya dola! Watu wakaamua imetosha!

Kwa maneno mengine, ni majibu (matendo) ya watu dhidi ya uonevu ambayo baadaye huzaa uhalifu. Hata nchini Tanzania sasa kuna maeneo yameanza kuonyesha dalili hizi! Polisi mmoja na kirungu hawezi kutia mguu akatoka salama!

Tuwalaumu Watanzania kwa kuwa na uoga unaokera?

Kabla hatujaamua nani wa kulaumiwa hebu tuangalie chimbuko la uoga. Uoga (kwa kimombo fear) hutokea pale kiumbe kinapoona maisha (life), mali (property) au maslahi (benefits) yake yapo hatarini.

Pia ni vyema kutambua kuwa kuna mazingira uoga ni jambo lenye faida. Kwa mfano kiwango kidogo cha uoga kabla mtu hajatoa hotuba au kuwasilisha mada unasaidia kuboresha uwezo wa mtu kufikiri. Kiwango kidogo cha uoga siku ya mtihani kinamsaidia mwanafunzi kubungua bongo!

Ni nini chimbuko la uwoga wa Watanzania unaowafanya wawe mabingwa wa uoga kama si wa Afrika basi wa dunia?

Mwanafalsafa mmoja Barnhil John Basil mwaka 1914 alisema hivi: ‘Where people fear the government you have tyranny and where government fear the people you have liberty .’ Kwa kiswahili chepesi ni: ‘Ikitokea watu wakaogopa serikali yao, basi unaambulia ufedhuli na ikitokea serikali ndiyo inaogopa watu, basi unaambulia uhuru’.

Kwa hakika, Watanzania wanaogopa serikali yao, na kwa mtazamo wangu hali hii ni matokeo ya mambo haya:

  • Kuvunjika kwa utawala wa kimila (Chieftainship)

Ukitazama mataifa mengi ya Kiafrika yaliyoendeleza mfumo wa uchifu utaona utiifu wa watu si kwa watawala serikalini bali kwa viongozi wao wa kimila. Angalia nchi kama Ghana, Nigeria, Senegal, Ethiopia, Mali, n.k. Chifu akitoa amri hata Raisi wa nchi hathubutu kuipinga labda awe hataki kura uchaguzi ujao.

Kwa kuwa machifu walitawala ‘kifamilia’ zaidi ya ‘kiserikali’ na walikuwa wana mtizamo kuwa anaowatawala ni  wana familia, hakukuwa na haja ya kuwepo matumizi makubwa ya maguvu au vitisho.

Ndio maana, kwa mfano, hata ‘kodi ya chifu’ ilikusanywa na kupelekwa kwa chifu kwa hiari au kwa njia za kistaarabu! Mfumo huu haukuruhusu UOGA kujijenga katika jamii.

Kwa bahati mbaya kwa Tanzania mfumo huu ulivunjwa mapema baada ya uhuru. Kukawepo na mfumo mmoja wa kiserikali ambao moja ya sifa yake kuu ni matumizi ya maguvu.

Pia mfumo huu una sifa ya kuamulia watu na kulazimisha watu watekeleze bila kuhoji. Ukihoji unapambana na maguvu ya serikali na waliotoa maamuzi. Matumizi ya maguvu na kutakiwa kutekeleza maamuzi ya wengine hujenga jamii yenye UWOGA.

Asilimia kubwa ya Watanzania wamezaliwa na kukulia ndani ya mfumo huu unaolea UWOGA! Na usishangae kuwa wale ambao wameonyesha kutokuwa na uwoga wengi ni wazee waliouona utawala wa machifu!

Kuna saa ubongo unawakumbusha inawezekana kuacha uwoga! Vijana wengi katika Tanzania bado waoga kwa sababu wamezaliwa na kukulia kwenye mfumo unaolea uwoga.

Kwa bahati mbaya uwoga ni sawa na magonjwa mengine! Mtu akishaugua uwoga (fear) kwa muda mrefu au kwa kiwango kikubwa au yote mawili haponi kwa urahisi. Lazima apate tiba.

Huwezi kutamani uwoga ukuondoke ukaondoka! You cannot just wish fear to go away as you cannot wish malaria to go away!

Kuna watu wanahofu ya giza (Scotophobia), kuna wengine ni uwoga wa buibui (Arachnophobia), wengine kina kirefu kwenda juu (Acrophobia), wengine mitihani (Testophobia), wengine upweke (isolophobia), wengine damu (Hemaphobia), wengine nywele (Chaetophobia), wengine kufanya kazi (Ergophobia), wengine vitabu (Bibliophobia), wengine mabadiliko (Metathesiophobia) na kadhalika na kadhalika.

Wote hao ni wagonjwa na wanahitaji tiba sawa na Watanzania waoga! Uwoga katika Tanzania ni ugonjwa wa kitaifa -  A national health pandemic! Ni janga kubwa zaidi ya HIV na ukimwi!

Watanzania wote (watawala na watawaliwa) wanaugua uoga wa watu au mfumo wa kijamii (sociophobia). Watawala wanawaogopa watawaliwa na watawaliwa wanawaogopa watawala.

Uoga hauwezi kusimama upande mmoja! Lazima kuwe na mtu au kundi zaidi ya mmoja ili uoga ufanye kazi! Kwa hiyo, katika Tanzania si raia peke yao wanaougua sociophobia. Watawala nao wanaugua ugonjwa huu - tena pengine kuzidi raia!

  • Kupata mtawala mheshimu haki za raia mara baada ya Uhuru.

Kuna msemo wa kimombo kuwa: ‘If the government becomes a law-breaker, it breeds contempt for the law. It invites every man to become a law unto himself. It invites anarchy’.

Hali hii ya anarchy inakomaza raia! Inawaondoa uoga!  Ukilinganisha na nchi nyingi za kiafrika Tanganyika ilipata bahati ya kupata kiongozi aliyekuwa anaheshimu kwa kiwango cha juu haki za aliowatawala – Mwalimu Nyerere.

Lakini wahenga husema ‘masika huja na mbu!‘ Bahati hii imetutumbukia nyongo. Kutokana na watawaliwa kuwa na uhakika kuwa mtawala anajali haki zao ‘walilemaa’! They lowered their guard. Iliwanyima watawaliwa fursa ya kujifunza namna ya kukabiliana na serikali au watawala wanapovunja haki zao.

Ukitaka kuelewa mantiki ya dhana hii tupa macho Zanzibar. Kwa kuwa watawala kuanzia utawala wa Sultani na ule baada ya Mapinduzi haukujali sana haki za binadamu, Wanzanzibar walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kukabiliana na watawala wavunja haki zao.

Leo hii tunaona watu wa Zanzibar wanavyotoa ‘somo’ kwa wenzao wa Bara namna ya kusimama kidete kutetea haki za raia pale zinaposiginwa na watawala. Hata hili sakata la Katiba linategemea mno msimamo wa watu wa Zanzibar kuliko wa Bara! Ikiwa Wazanzibar watasimama kidete itapatikana Katiba yenye kujali maslahi ya wananchi. Ikiwa Wanzanzibar watalegea au kulegezwa itapatikana Katiba ya maslahi ya kikundi cha watu wachache.

Hata wale waliokuja na rasimu yao wanalijua hili! Yaani Watanganyika waoga wataponea ungangari wa Wazanzibari! Wakati mwingine ni vyema kupata uhuru kwa mbinde au kupata mtawala wa mwanzo ‘katili kidogo’. Si siri mtoto aliyedekezwa huwa zobe ukubwani!

  • Kutawala kupita kiasi (over governance)

Mwanafalsafa mmoja Hendry David Thoreau mwaka 1849 alipata kusema–‘ the government is best when it governs least’Kwa Kiswahili chepesi ni: ‘Serikali inakuwa serikali bora pale inapotawala kwa kiwango kidogo au cha kadri’!

Ukilinganisha mfumo wa utawala wa Tanzania na nchi jirani au nyingi za Afrika utaona kwamba Tanzania ina utawala wa kupita kiasi (excessive governance). Utawala umesambaa hadi nyumba kumi!

Yaani mkono wa serikali umejikita hadi majumbani mwa watu. Hata watu (pamoja na watawala) utawasikia wakijitapa ‘usicheze na nchi hii, kuna system bwana’! Na kweli, kwa miaka mingi usingeweza kufanya kitu hata kijijini na kitu hicho kisijulikane!

Lakini kuna faida na hasara zake. Hasara zake ni kujenga tabia ya woga! Hamna tofauti na Serikali ya Marekani ilipopitisha sheria ya kusikiliza hata maongezi ya simu ya mtu. Iliwatia uoga Wamarekani. Hiyo ni matokeo ya over governance!

Hata ndani ya nyumba kama wazazi wataanza kuwa na tabia ya kupekua vyumba vya watoto watajenga uoga kwa watoto wao! Ni mtazamo wangu kuwa  over governance Tanzania imezalisha miungu watu toka vijijini, katani, wadini, wilayani, mikoani hadi taifani. Hawa wamekuwa wakala wa uwoga. Wana nguvu za ajabu na wako juu ya sheria. Nchi za wenzetu hazina hawa miungu watu kama sisi!

  • Serikali kugeuka kundi la watu wasiotawalika (when a government turns into a group of people notably ungoverned).

Ukilinganisha watawala wa Tanzania na wale wa wenzetu utagundua watawala wa Tanzania hawatawaliki. Serikali nzuri ni ile ambayo watawala wanatawalika. Watawala ambao kazi yao ni kutawala raia si watawala wema!

Watawala wasiotawalika wanahamasika kutenda matendo yanayosababisha watawaliwa kujenga uoga kwa kuwa wanaamini hakuna wa kuwatawala aidha wakiwa madarakani au wakishaondoka madarakani.

Watawala wa aina hii watavunja haki za raia with impunity kwa kuwa wanaamini wako juu ya sheria. Watatoa kauli za dharau na kutia hofu. Ndio maana utasikia kauli hizi: ‘Tutatawala miaka 100’, ndege ya raisi itanunuliwa hata ikibidi mle nyasi’, watawaliwa ni wavivu wa kufikiri’, n.k.

Hawatawaliki! Hebu fikiria umestaafu, umenunua daladala usife haraka kwa kukosa hela halafu umeajiri dereva lakini hatawaliki na huwezi kumtimua kazi? Utalala usingizi? 

Hawa watawala wetu wasiotawalika huwa kila miaka mitano wanakuja kuomba ajira! Tukiwapa kazi hawatawaliki! Wanaenda Dodoma wanajipangia mishahara na marupurpu ya kufuru. Wanapata mafao ya kustaafu makazini kwao na bungeni bila aibu!

Wakija tena baada ya miaka mitano wanakuja na mihela chungu mbovu waliyotuibia na wanachaguliwa tena! Wana tofauti gani na yule dereva wa daladala? Watawaliwa wanajua hawatawaliki lakini wanashindwa kuwanyang’anya funguo za gari! Si lazima uwaogope?

  • Kuwa na mfumo uliotufanya tuwe kama watu wa familia moja

Mara baada ya uhuru Tanzania ilipata bahati nyingine ya kuwa na kiongozi aliyejenga mshikamano wa taifa. Wote tukawa watu wa familia moja. Hii ni mvua nyingine ya masika - ilikuja na mbu wa malaria!

Jamii ikiwa moja huwa inakosa changamoto. Wote mnafanana, mnaheshimiana, mnapendana. Hakuna wa kudhulumiwa au kudhulumu. Mnatulia! Kwa kutulia huku mnakosa fursa ya kufikiri tofauti au kujifunza mbinu za kutetea haki zenu.

Ndio maana mpaka sasa bado Watanzania wengi wanaamini hakuna haja ya kugombana. Na watawala wanajua hili. Utawasikia wakisema: ‘Nchi yetu ni kisiwa cha amani’! Au ‘tukitofautiana ama kubadili viongozi ama chama tutapigana vita kama waleee’!

Wanajua akili za Watanzania wengi bado zinaamini sisi wote bado ni watu wa familia moja kama zamani. Hii hofu ya kuvunja hii ‘familia’ ndiyo inayotutafuna sasa japo kwa hakika ile familia ya ‘Watanzania’ haipo tena! Iliondoka na Nyerere!

  • Katiba inayotisha

Ukitizama Katiba yetu na za majirani zetu utaona Katiba yetu ‘inatisha’! Hata tume walizounda watawala wenyewe zimethibitisha hilo. Marehemu Jaji Nyalali aliziorodhesha sheria kandamizi na kupendekeza zifutwe. Ingawa watawala wanatuambia nyingi zimefutwa ukitizama Katiba unajiuliza ‘ipi’?

Bado Katiba yetu inawapa watawala madaraka ya kiutu Mungu - madaraka ambayo, penda usipende, yanatia na yanatumika kutia hofu!

  • Vyombo vya dola vinavyoamini utiifu ni kwa watawala badala ya raia

Ukiangalia utendaji kazi wa vyombo vya dola utaona majeshi yetu yamekuwa na yako karibu sana na watawala kuliko ilivyo kwa wenzetu. Ni Tanzania pekee ndio ulikuwa unaweza kusikia kuna makamisaa wa chama jeshini!

Kwa wenzetu wengi majeshi yaliwekwa kando kwenye masuala ya kisiasa na utawala wa raia. Pia kwa muda wa miaka mingi wenzetu walikuwa wanawaweka wanajeshi wao makambini wakati kwetu walichanganyika na raia uraiani.

Kitendo cha kuishi na ‘mjeshi’ karibu ni kitisho tosha kwa raia. Raia anajua siku akifanya fyoko mtu wa kumtia adabu hayuko mbali! Ni sawa na kuishi na mwalimu wako wa shule ya msingi kwani inabidi uwe na adabu maradufu ya wenzio!

Hebu fikiria ingewezekana Kenya, Uganda, Malawi kiongozi mkuu wa jeshi ajitokeza wakati wa kampeni aseme kama ambavyo kiongozi wetu mmoja  wa jeshi alivyotoa vitisho wakati wa uchaguzi? Jiulize tena ni mara ngapi umesikia kwa wenzetu eti mwanajeshi kagombana na raia baa, na kisha kaenda kambini kuchukua wenziwe kuja kupiga kila mtu mtaani?

Pale ambapo jeshi linaamini utiifu ni kwa raia huwa linaogopa kutenda hivyo. Pale ambapo jeshi lina utii kwa watawala kuliko kwa raia litatenda hayo. Nani wa kuwawajibisha?

Jiulize tena kwa wenzetu askari wanapanda mabasi ya watu bila kulipa nauli? Kwa nini Tanzania askari anaweza kupanda basi la mtu kama lake? Unadhani ni kwa nini hata wenye magari wanaogopa kuwadai nauli?

Jeshi ni chombo cha maguvu hivyo kikishaacha kuwatii raia lazima hofu ijengeke! Watawaliwa wataogopa jeshi na wataogopa watawala kwa kuwa wanajua lao moja!

Sasa tufanyeje ili tutibu sociophobia?     

Itakuwa si rahisi kuwapeleka Watanzania wote watawala na watawaliwa hospitali kutibiwa ugonjwa wa uoga! Kwanza tiba ya uoga si fani iliyojizatiti sana hapa nchini. Ili kupunguza gharama za tiba na kutibu Watanzania wengi iwezekanavyo tunahitaji SOCIAL THERAPY.

Social therapy inaweza kutekelezwa kwa njia mbalimbali lakini kwa leo nizingatie njia kuu mbili: ELIMU na KATIBA.

Elimu

Inahitajika elimu kubwa ya haki za raia kwa makundi yote, watawala na watawaliwa. Elimu hii isisubiri wakati wa uchaguzi pekee wala isiendeshwe mijini pekee. Iwe ni elimu endelevu na izame hadi vijijini. Iwe elimu itakayofanya Mtanzania mwanamke kwa mwanaume, kijana kwa mzee, mtoto, masikini kwa tajiri, mkulima kwa mfanyakazi, wa mjini na wa vijijini aweze kusimama kidete kutetea haki zake. Pia iwe elimu itakayotolewa kwa watoto mashuleni ili kizazi kijacho kisiambukizwe sociophobia kama sisi wazazi wao.

Katiba

Kwa kuwa sasa tunaunda Katiba mpya ni wakati muafaka kuhakikisha katiba inaondoa mamlaka, taasisi na sheria zilizotufanya tuugue sociophobia!  Katiba isafishwe kuondosha vitisho.

Tutumie muda mwingi kupata Katiba ambayo haina vitisho, inayoheshimu haki za raia, inayolinda rasilimali za nchi, inayofanya watawala watawalike, itakayotuondolea over governance, itakayoweka utaratibu wa kuwapata watawala wanaoheshimu sheria na mbayo itaweka utaratibu wa kila mtu kuwasilisha malalamiko yake ikiwa haki zake zitavunjwa na mtu yeyote yule.

Tusipoteze muda mwingi kutukanana, kupigana vijembe, kufanyiana mizengwe au kujadili mambo yasiyo kipaumbele. Kama ni mipasho wapo waimbaji wengi tu mitaani! Kama ni matusi yamejaa tele mitaani! Kama ni comedy mbona wako kibao tu mitaani?!

Wabunge wa Bunge la Katiba (japo kwa kweli sikubaliani na namna walivyopatikana) wageuke wawe madaktari na si wana mipasho! Watuletee tiba ya huu ugonjwa wa sociophobia.

Kinyume chake watakuwa wamechochea ugonjwa wa taifa! Hawatakuwa tofauti na madaktari walevi wanaosahau mikasi tumboni mwa mgonjwa! Wakiacha jukumu hili tutawakumbuka kwa matusi yao na inawezekana huko mbele ya safari wananchi wakawadai warudishe hela walizochukua kwani hawakufanya kazi waliyowatuma.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/uoga-wa-watanzania-ni-ugonjwa-wa-kihistoria-na-kimazingira#sthash.3AxX1eRK.dpuf

Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates