Social Icons

Sunday 7 September 2014

HADITH: Missed call ya shemeji 1



“Dada Ime, kama wewe dada yangu kweli niambie ukweli, nini kinaendelea kati yako na mume wangu?”
“Hakuna mdogo wangu, unajua mumeo amezidi sana utani. Ni hilo tu.”
“Mbona jana usiku alikuja chumbani kwako nilipotoka kwenda chooni mkajifanya mnaulizana chaja ya simu?”

“Eee, alisema chaja yake imepotea na simu haina chaja anataka kuongea na wazazi wake.”
“Oke, wewe unaishi kwangu na hufanyi kazi, lakini kila siku una vipodozi vipya, pafyumu za kisasa, nguo za maana, nani anakununulia na unashinda ndani mchana kutwa?”
“Nilikuwa na akiba kidogo nilipotoka kwa mume wangu.”

“Juzi usiku nilipopita usawa wa mlango wako kwenda chooni nilikusikia unalia kimahaba, mume wangu alikuwa hajarudi lakini cha ajabu aliporudi nilishtukia anaingia ndani, je! Hakuwa kwako?”
“Akha! Yeye amesema alikuwa kwangu? Muongo mumeo, anataka tuvurugane.”
“Hajasema alikuwa kwako, ila mimi nahisi alikuwa kwako. Dada please, niambie ukweli, naweza kumwambia baba kijijini kwamba unatembea na shemeji yako.”

”Noo, hautakuwa umenitendea vyema Aisha mdogo wangu, mimi na wewe ni ndugu na Beka ni mumeo, sasa ukisema uwaambie wazazi jambo zito kama hilo ni vibaya, naamini umenifikiria tofauti mdogo wangu.”

Aisha alimkazia macho dada yake Ime ambaye kirefu chake ni Imejinina akiamini anatembea na mume wake. Moyoni alisema...

“Wengi niliowahi kuwasikia wakilalamika kuhusu mashemeji ni wakubwa kuhisi au kugundua wadogo zao wanatembea na mashemeji zao, sasa mbona huyu ni dada yangu, tena wa kwanza, kuna wawili katikati yetu.

“Halafu ni kwa nini, mume wangu ni mdogo sana kwake na ndiyo maana anampa shikamoo.”

***
Mara ya tatu, Ime kufika kwa mdogo wake huyo na kuomba hifadhi baada ya kuachika kwa mumewe kwa madai mwanamke huyo ‘ana mdomo sana’ ilikuwa Jumapili jioni ambapo alipofika alimkuta Beka tu, shemejiye kwa mdogo wake, Aisha.
“Oooh! Shemeji, karibu sana mke wangu. Mbona ghafla kwema huko?”
“Kwema shemeji, sijui nyie hapa?”

“Sisi wazima sana. Ila mdogo wako amekwenda saluni muda si mrefu,” alisema Beka huku akiingiza begi kubwa kwenye chumba cha wageni.
Alipotoka chumbani alifikia kukaa sebuleni…
“Enhe shemeji, vipi huko?”
“Da! Shemeji nyumbani kwangu bwana si kwema.”
“Nini tena shemeji?”

“Nimeachwa.”
“Ha! Umeachwa?”
“Ndiyo.”

“Una maana umeachika siyo?”
“Ndiyo kuachwa shemeji.”
“Kisa nini shemeji?”
“Sijui mwenyewe, jana usiku kaniambia mimi na yeye basi, hanitaki tena. Sasa nitamlazimisha shemeji?”
“Watoto?”

“Amesema anabaki nao kwa vile umri wao umefikia kuweza kuishi na baba yao pia.”
“Mh!” aliguna Beka huku akijikuna kichwani kwa ishara kwamba, hakuwa akiwashwa bali ni mawazo kuhusu sakata la shemeji yake.

Angekuwa analingana umri na mume wa shemeji yake huyo angempigia simu na kumuuliza kulikoni lakini sasa umri uliwatofautisha sana.
“Shemeji we pole sana, lakini pia karibu sana, jisikie hapa upo nyumbani kwako shemeji yangu, sawa?” alisema Beka.

Itaendelea kesho


No comments:

 
 
Blogger Templates