Social Icons

Wednesday, 10 September 2014

HADITH: Nilioa jini niamsaliti -8


Waliendelea kula kimyakimya hakukuwa na mazungumzo yoyote mpaka walipomaliza na kuondoka. Walipofika ofisini Thabit alionekana amechoka hakukaa alimuaga Subira kuwa anatoka kidogo. 
SASA ENDELEA…

Baada ya kutoka Subira alijiuliza  maswali mengi juu ya hali ya bosi wake kugeuka vile wakati alikuwa amechangamka na kumpa matumaini hasa pale  alipoonesha kumuulizia kuhusu uhusiano wake aliamini dawa za mzee Mukti zilikuwa zikifanya kazi.

Lakini hali iliyomtokea muda mfupi baada ya kufika Steers ilimshtua sana, alijiuliza hali ile ilitokana na nini. Alinyanyua simu yake na kumpigia mzee Mukti, baada ya kuita ilijibu kuwa inatumika. Alisubiri kwa muda kidogo na kupiga tena ambayo muda ule ilipokelewa.

“Haloo.”
“Haloo mzee wangu.”
“Ndiyo mama unasemaje?”
Subira alimweleza yote yaliyotokea muda mfupi, baada ya kumsikiliza mzee Mukti Buguju alishusha pumzi ndefu na kusema:

“Subiri kidogo,” mzee Mukti alisema na kukata simu ili aangalie kilichotokea kimetokana na nini. 
Baada ya muda mfupi alipiga simu iliyopokelewa na Subira.
“Ndiyo mzee wangu.”
“Nimeona.”

“Umeona nini mzee wangu?”
“Hali iliyomtokea bosi wako ilitokana na kuhama kimawazo yalikuwa ni mawasiliano kati yake na mkewe jini Nargis. Lakini yalikuwa ya kumbukumbu baada ya kuingia, Jini Nargis alijitahidi kumvuta ili azungumze naye lakini hayakuweza kumpata vizuri. Mkewe ameisha jua nini kinatendeka duniani lakini kwa sasa hana nguvu tena baada ya kuiua nguvu ya pete ambayo ndiyo iliyokuwa kiunganishi kikubwa kati ya bosi wako na mkewe jini.

Walichoweza ni kumtia uchovu ili akalale awaze kuwasiliana naye, kwa vile pete haikuwa na nguvu, lazima Jini Nargis atawatuma vijakazi wake waichukue na kuirudisha chini ya bahari kwenda kuongezewa nguvu kisha atarudishwa kabla hajaamka na kuvisha kuanzia hapo mawasiliano yatarudi kama kawaida. Na tukichelewa tutakosa kila kitu na wewe kufukuzwa kazi”

“Mungu wangu! Sasa itakuwaje?” Subira aliuliza.
“Kuna kazi nataka nikupe muda huu ili kumuwahi.”
“Kazi gani?”

“Ile dawa ya unga ipo?”
“Ndiyo.”
“Unajua anapokaa bosi wako?”
“Ndiyo, lakini sijawahi kufika.”

“Chukua hiyo dawa, kanunue maji safi lita moja na nusu kisha chukua dawa kidogo changanya. Ondoka na hayo maji nenda moja kwa moja hadi anapokaa bosi wako ukifika getini mwaga kidogo kisha ingia ndani ya uzio mwaga kidogo. Nenda mpaka kwenye nyumba ya bosi wako mwaga kidogokidogo kuizunguka nyumba yote kisha ingia ndani na kumwaga kidogokidogo nyumba nzima.

“Kuna vitu utavisikia wakati ukiendelea na zoezi hilo usiogope fanya kazi niliyokuelekeza, hata viwe vinatisha vipi endelea na zoezi lako kwa vile havitakudhuru kwani utakuwa ukiua nguvu za kijini. Utashangaa kukuta jumba lote lile hakuna mtu, kama nilivyokueleza awali baada ya mkewe jini Nargis kuondoka alimuachia vijakazi ambao walimfanyia kazi zote za usafi na kumpikia. Lakini dawa utakayoimwaga ndiyo itakayo waondoa na kutimka kwa maumivu.


Ukiisha maliza zoezi hilo ingia chumbani kwa bosi wako utamkuta amelala lakini kidoleni hana pete ambayo itakuwa imepelekwa ujinini kurudishiwa nguvu ya awali. Mpake maji kichwani na kumuacha, nenda bafuni weka maji kwenye beseni, weka dawa hiyo oga maji hayo na kubakisha mengine. Rudi ndani muamshe Thabit akiamka mshike mkono atakuwa kama zezeta kwa vile nguvu za kijini zitakuwa zimetoka.

“Mpeleke bafuni mwogeshe maji ya dawa, muda ule atarudi katika hali yake ya kibinadamu. Mtarudi chumbani mtalala kama wapenzi. Ukifanya zoezi zima kwa umakini huo ndiyo utakuwa mwanzo wako wa kuishi na Thabit.

“Najua vita itakuwa kubwa ya kutaka kukutoa mikononi mwake lakini kuna dawa nitakupa hakuna jini wala mchawi atakae kugusa. Kisha kuna kazi nyingine nzito ya kulinda mali ya Thabit ambayo ni ya majini ambao watataka kuirudisha mikononi mwao kama wakishindwa kumpata Thabit. Japokuwa najua ni ngumu lakini tutashinda na zawadi mtanipa.”

“Sawa mzee wangu nikikwama nitakupigia simu.”
“Hakuna tatizo lakini zoezi hilo lifanye sasa hivi.”
“Sawa mzee.”

“Nilitaka kusahau hakikisha baada ya kukutana naye kimwili unaondoka kuja kwangu, jitahidi kabla kivuko hakijasimama.”
“Sawa mzee wangu.”

Baada ya mazungumzo Subira alivuta droo ya meza yake na kutoa karatasi iliyokuwa na dawa ya unga, aliirudisha na kutoka kwenda dukani na kununua maji ya lita moja na nusu na kurudi nayo ofisini. Aliingia ofisini kwa bosi wake ambako aliamini ni sehemu salama na kuitia dawa kwenye maji na kuitikisa kisha aliiweka kwenye mfuko wa plastiki.

Alitoka na kukodi bodaboda hadi nyumbani kwa bosi wake, aliteremka na kumlipa dereva. Alisogea karibu ya mlango wa kuingilia, alitoa chupa yake kwenye mfuko na kuishikilia mkononi. Huku mapigo ya moyo yakimwenda kwa kasi alitembea kuelekea mlango mkuu.

Aliifungua chupa na kuanza kumwaga getini, maji yalipogusa chini alisikia mtikisiko, japokuwa  mapigo ya moyo yaliongezeka lakini alijikaza na kuingia ndani. Kila alipomwaga maji mtikisiko  mkubwa ulitokea. Akwenda hadi kwenye jumba la kifahari na kuendelea na zoezi la kumwaga maji kuizunguka nyumba ile.

Mtikisiko uliongezeka mara dufu aliona kama nyumba inataka kudondoka, kama asingepewa maelekezo angekimbia hali ilikuwa ikitisha sana. Baada ya kumaliza zoezi la kuzunguka nyumba aliingia ndani na kuendelea na zoezi lake. Alishangaa kukuta nyumba tupu lakini ikinukia manukato mazuri sana.
Alipoanza kunyunyiza maji ndani alisikia vishindo na sauti za vilio vya maumivu. 

Itaendelea

Chanzo globalpublishers


No comments:

 
 
Blogger Templates