Social Icons

Sunday 7 September 2014

HADITHI: Missed call ya shemeji 2


DADA Ime, kama wewe dada yangu kweli niambie ukweli, nini kinaendelea kati yako na mume wangu?”

“Hakuna mdogo wangu, unajua mumeo amezidi sana utani. Ni hilo tu.”
“Mbona jana usiku alikuja chumbani kwako nilipotoka kwenda chooni mkajifanya mnaulizana chaja ya simu?”

“Eee, alisema chaja yake imepotea na simu haina chaja anataka kuongea na wazazi wake.”
“Oke, wewe unaishi kwangu na hufanyi kazi, lakini kila siku una vipodozi vipya, pafyumu za kisasa, nguo za maana, nani anakununulia na unashinda ndani mchana kutwa?”
“Nilikuwa na akiba kidogo nilipotoka kwa mume wangu.”

“Juzi usiku nilipopita usawa wa mlango wako kwenda chooni nilikusikia unalia kimahaba, mume wangu alikuwa hajarudi lakini cha ajabu aliporudi nilishtukia anaingia ndani, je! Hakuwa kwako?”
“Akha! Yeye amesema alikuwa kwangu? Muongo mumeo, anataka tuvurugane.”

“Hajasema alikuwa kwako, ila mimi nahisi alikuwa kwako. Dada please, niambie ukweli, naweza kumwambia baba kijijini kwamba unatembea na shemeji yako.”
”Noo, hautakuwa umenitendea vyema Aisha mdogo wangu, mimi na wewe ni ndugu na Beka ni mumeo, sasa ukisema uwaambie wazazi jambo zito kama hilo ni vibaya, naamini umenifikiria tofauti mdogo wangu.”

Aisha alimkazia macho dada yake Ime ambaye kirefu chake ni Imejinina akiamini anatembea na mume wake. Moyoni alisema...

“Wengi niliowahi kuwasikia wakilalamika kuhusu mashemeji ni wakubwa kuhisi au kugundua wadogo zao wanatembea na mashemeji zao, sasa mbona huyu ni dada yangu, tena wa kwanza, kuna wawili katikati yetu.
“Halafu ni kwa nini, mume wangu ni mdogo sana kwake na ndiyo maana anampa shikamoo.”

***
Mara ya tatu, Ime kufika kwa mdogo wake huyo na kuomba hifadhi baada ya kuachika kwa mumewe kwa madai mwanamke huyo ‘ana mdomo sana’ ilikuwa Jumapili jioni ambapo alipofika alimkuta Beka tu, shemejiye kwa mdogo wake, Aisha.
“Oooh! Shemeji, karibu sana mke wangu. Mbona ghafla kwema huko?”
“Kwema shemeji, sijui nyie hapa?”

“Sisi wazima sana. Ila mdogo wako amekwenda saluni muda si mrefu,” alisema Beka huku akiingiza begi kubwa kwenye chumba cha wageni.
Alipotoka chumbani alifikia kukaa sebuleni…
“Enhe shemeji, vipi huko?”

“Da! Shemeji nyumbani kwangu bwana si kwema.”
“Nini tena shemeji?”
“Nimeachwa.”
“Ha! Umeachwa?”
“Ndiyo.”

“Una maana umeachika siyo?”
“Ndiyo kuachwa shemeji.”
“Kisa nini shemeji?”
“Sijui mwenyewe, jana usiku kaniambia mimi na yeye basi, hanitaki tena. Sasa nitamlazimisha shemeji?”
“Watoto?”

“Amesema anabaki nao kwa vile umri wao umefikia kuweza kuishi na baba yao pia.”
“Mh!” aliguna Beka huku akijikuna kichwani kwa ishara kwamba, hakuwa akiwashwa bali ni mawazo kuhusu sakata la shemeji yake.

Angekuwa analingana umri na mume wa shemeji yake huyo angempigia simu na kumuuliza kulikoni lakini sasa umri uliwatofautisha sana.
“Shemeji we pole sana, lakini pia karibu sana, jisikie hapa upo nyumbani kwako shemeji yangu, sawa?” alisema Beka huku akisimama na kumpiga begani kama kumpoza, akaenda kwenye simu ambayo ilikuwa chaja akampigia mke wake…

“Aisha, ndoa yako na yangu leo imevunjika, nyumbani kaja mke wangu mkubwa, we ulie tu.”
Aisha kwa vile alijua mke mkubwa ni dada yake Ime, alimuuliza mume wake mbona mgeni huyo amefika ghafla sana?
“Kuna matatizo makubwa alikotoka.”
“Kama yapi?”
“Ungekuja basi, maswali gani hayo?”
“Oke, nakuja.”

***
Baada ya dakika ishirini na tano, Aisha alifika nyumbani kwake na kumkuta dada yake ameshabadili nguo za safari na sasa yu ndani ya vitenge ambavyo alijifunga viwili, kimoja kilikatisha usawa wa nido kingine kwenye kiuno.
Jane alimkumbatia dada yake, wakaganda kama dakika moja nzima huku wakiulizana hali za watoto na maisha.

“Karibu sana dada.”
“Haya asante.”
“Kwema kabisa lakini huko?”
“Si kwema sana mdogo wangu, shemeji nimeshamsimulia kila kitu kuhusu nitokako.”
Aisha akamgeukia mume wake na kumwangalia kwa macho ya kuna nini kwani…
“Ndoa ya shemeji imevunjika!”
“Eti nini?”

“Ndiyo hivyo mdogo wangu, shemeji yako kaniacha, kasema hanitaki tena ndiyo nikaamua nije kwako nipumzike kidogo kabla sijarudi kijijini kwa wazazi.”

Aisha alilia sana tena sana hasa alipokumbuka siku ya ndoa ya dada yake huyo ambapo yeye alikuwa mpambe.

“Sikia nikwambie dada yangu…”
“Nakusikia mdogo wangu…”

“Kaa hapa mpaka utakapochoka, hakuna haja ya kwenda nyumbani wala kwa nani. Ukisema uende kwa wazazi utawapa mzigo, mimi sikushauri hata kidogo.”
“Mh! Vizuri mdogo wangu, nilidhani hata nyinyi nitakuwa nimewapa mzigo.”
“Wala shemeji, usijali kabisa kuhusu hilo,” alisema mume wa Aisha, Beka huku akionesha dalili za uchangamfu wa hali ya juu kwa shemeji yake huyo, akaingiza na kautani…

“Ungechelewa kuolewa ningekuoa mimi, wala leo usingepata tabu kama hivi,” wakacheka wote mpaka mbavu hawana!

***
Wiki ilipita, awali mtu wa kwanza kuamka ndani ya nyumba huyo alikuwa Beka, lakini tangu aje dada wa Aisha yeye ndiye amekuwa mtu wa kwanza kuamka na kukaa sebuleni akiwa amewasha tivii, akitokea Beka husalimiana kisha hutoka kwenye tivii kwenda kufanya kazi nyingine za ndani ya nyumba hiyo.

Na mara nyingi Beka akimkuta sebuleni, shemeji mtu huyo humchangamkia sana…
“Ah! Mume wangu huyo! Umeamkaje baby?”
“Nimeamka salama mke wangu, vipi wewe na kuamka kwako?”
“Mimi sijambo, najisikia nimeshazoea mazingira ya hapa.”
“Utazoea zaidi maana upo kwa mumeo wa ukweli,” alijibu Beka akiwa anaachia tabasamu.

***
Usiku wa siku hiyo, Beka na mke wake, Aisha walitofautiana chumbani, ikawa zogo…
“Mimi nataka nikisema unisikilize, siyo kujibishanajibishana, we mwanamke vipi?”
“Vipi kwani vipi, wewe mwanaume vipi?  

Itaendelea tena

No comments:

 
 
Blogger Templates