Ghafla juu ya bahari kiza kizito kilitokea, Thabit alijiona kama akizamishwa ndani ya bahari, alipotaka kupiga kelele maji tayari yalikuwa yamejaa mdomoni. Aliposhtuka alijikuta amelala kwenye nyumba yao mpya waliyojenga kama Nargis akiondoka kwenda kujifungua ili aishi maisha ya kawaida ya kibinadamu.
Nyumba ilikuwa na kila kitu, kama kawaida Nargis alimuachia mumewe vijakazi toka ujinini kwa ajili ya kumpikia na kumfanyia usafi. Yalikuwa maisha mapya ya Thabit kuishi bila ya mpenzi wake jini Nargis.
SASA ENDELEA...
Thabirt aliyaanza maisha mapya wakati huo alikuwa amefunguliwa miradi mingi ambayo itamfanya awe bize ili watu washtuke kutaka kujua maisha yake ya kukaa tu akiwa na maisha mazuri. Thabit kila asubuhi alikwenda mjini kwenye moja ya duka lake kusaidiana na wafanyakazi wake kufanya biashara na jioni alirudi nyumbani.
Maduka mawili yalikuwa Posta na mengine mawili Kariakoo, yalikuwa maduka makubwa sana yaliyouza vitu mbalimbali. Moja liliuza vifaa vya elektoroniki ambavyo ni simu, redio, feni, friji na vifaa vyote vya umeme.
Lingine lilikuwa likiuza nguo za kike na kiume na viatu. Maduka ya Kariakoo moja liliuza vyombo vya ndani na lingine liliuza nguo za majumbani kama mashuka mapazia na vitu vyote vya ndani.
Pia alikuwa akimiliki magari ya kifahari, kila mtu alimfahamu mjini kwa utajiri wake. Wafanyakazi wake walifurahi malipo aliyowalipa na kufanya wamheshimu sana.
Kwa muda mfupi aliweza kufungua kampuni kubwa iliyokusanya miradi yake yote na yeye kuwa mkurugenzi wake. Jina la Thabit lilisambaa haraka kama moto kwenye nyasi kavu. Alikuwa ni mmoja wa watu wenye utajiri nchini huku kila mmoja akishamgaa uwezo wake wa kifedha kwa watu waliomfahamu toka enzi wakifanya kazi pamoja za vibarua kwenye makampuni ya Wahindi miaka ya nyuma kabla hajaonana na Jini Nargis.
Maisha yalimwendea vizuri japokuwa aliyakosa mapenzi ya mkewe Nargis, lakini kila usiku ulipoingia alijipaka mafuta. Usiku wote huwa na mpenzi wake Nargis ndotoni mpaka kunakucha ile kidogo ilimfariji na kujiona kama walikuwa pamoja.
Wasichana wengi kazini walimshangaa bosi mzima kama yule kutokuwa na mke, walipomuuliza aliwaeleza ana mke ambaye muda ule alikuwa amesafiri. Aliwaonesha mpaka pete ya ndoa kuonesha yeye ni mume wa mtu.
Lakini walishangaa toka awaeleze miaka zaidi ya mitatu ilikatika bila kumuona huyo mkewe kitu kilichoanza kuwafanya wawe na maswali labda bosi wao si rijali.
Subira sekretari wake siku zote alimpenda sana bosi wake lakini alishindwa kumwambia mateso ya moyo wake toka alipomweleza ana mke. Lakini muda ulizidi kukatika bila kumuona huyo mwanamke.
Alijiuliza kwa nini bosi wake hakuwa na mke! Siku zote aliumia sana lakini hakutaka kuendelea kuteseka, alimfuata shoga yake Sofia naye alikuwa mchemsha chai mpaka mpenzi wa bosi na kuwekwa kuwa sekretari wa kampuni tofauti.
Kwa vile walikuwa wameshibana na kuujua machepele wake wa kubadilisha wanaume alimweleza anavyompenda bosi wake.
“Si ana mke yule?”
“Ndiyo anavyosema lakini mwaka wa tatu unakatika hatujawahi kumuona mke wake.”
“Mmh! Basi atakuwa na tatizo!”
“Hapana naamini hana tatizo ila bado hatujamvutia kati yetu.”
“Sasa utafanyaje?”
“Ndiyo maana nimekuja unipe mawazo.”
“Labda tumwendee kwa babu.”
“Wewe unamjua nani mkali?”
“Mzee Mukti Buguju dawa za mapenzi mzee yule anatisha. Si unakumbuka yule shemeji yako Muhindi aliyekuwa bosi wa kampuni yetu? “
“Eeh! Mukesh, kweli siku hizi yupo wapi?”
“Shoga yaani majanga, nilipewa siku tatu nikamtia mikoni.
Aliniahidi vitu vingi wiki moja kabla ya kuvitekeleza si akaondoka kumbe mkataba wake ulikuwa umekwisha. Yaani kama angekuwepo mpaka sasa ningekuwa na nyumba na gari. Mzee Mukti Buguju namuamini sana.“
“Dawa zake hazima masharti magumu?”
“Wala zipo za kwenye chai na zingine za kufusha usiku chumbani na kuoga basi.”
“Yaani hivyohivyo tu mwanaume anakuwa wako?” Subira kama hakuamini vile.
“Tena anakutamkia mwenyewe.”
“Mmh! Nikipata bosi wangu mbona nitakuwa tajiri, nashangaa mwanaume mwenye pesa kama nini hana hata mtoto!”
“Basi shoga ukiwa tayari twende kwa mzee Mukti Buguju.”
“Anakaa wapi?”
“Mji mwema.”
“Si kuvuka Kigamboni?”
“Ndiko hukohuko.”
“Mmh! Huko panafaa mwisho wa wiki siku ambayo siendi kazini.”
“Kwani chai anamtengea nani?”
“Mimi.”
“Basi amekwisha, jihesabu ni wako.”
“ Yaani shoga nakuahidi zawadi kubwa kama nikimpata hata gari nitakununulia.”
“ Mmh! Gari?” Sofia alishtuka.
“Jamaa ana hela kama nini, nikimpata utakubaliana na mimi.”
“Ukifika kwa mzee Mukti Buguju utakubaliana na mimi.”
****
Wakati Thabit akifarijika kuwa na mkewe jini Nargis ndotoni, Subira naye alikuwa mawindoni. Mwisho wa wiki walielekea Mji Mwema kwa mganga mzee Mukti Buguju. Kama walivyopanga walipitiana na kupanda daladala mpaka feri na kuvuka kisha walipanda daladala kuelekea Mji Mwema.
Walipofika waliteremka na kutembea kwa dakika kumi kuingia ndani kidogo hadi kwa mganga Mukti Buguju. Alikuta nje ya nyumba kuna magari manne ya kifahari, alipita ndani na kukaa kwenye mkeka. Watu hawakuwa wengi sana kutokana na siku yenyewe.
Mzee Mukti Buguju alikuwa na wasaidizi wengi ambao ndiyo waliopokea wateja. Baada ya kukaa alipewa namba ya kuonana na mzee na kutulia baada ya kuelezwa wataitwa kwa namba. Wakiwa wamekaa waliona watu wazito serikalini wakitoka ndani na kuingia kwenye magari yao na kuondoka.
Sofia alimnong’oneza Subira kwa kumwambia:
“Yaani huyu mzee kiboko hakuna anachoshindwa kwake mpaka nanii anakuja hapa!”
“Muongo, ulimuona?”
“Hapana alinieleza mzee Mukti, siku anayokuja huwa hakuna mteja.”
“Mmh! Basi atakuwa kiboko.”
“Wee utaniambia mwenyewe baada ya kumpata bosi wako.”
Baada ya muda namba yao iliitwa, waliingia ndani ya chumba kikubwa chenye mikeka ya kisasa kila kona kulikuwa na udi uliokuwa ukiwaka na kukifanya chumba kinukie.
“Karibuni,” mzee Mukti aliwakaribisha, alikuwa mzee wa makamo mwenye mwili ulioshiba. Alivalia kanzu nyeupe na kibalaghashia.
“Asante mzee, shikamoo.”
“Marahaba, mmh! Mna shida gani?”
“Ni mwenzangu hapa, mimi nimemleta tu,” Sofia alisema.
“Ndiyo nimeona hapa mwenye matatizo ni mmoja, haya bibi shida yako nini?”
Subira alielezea shida iliyompeleka pale, baada ya kumsikiliza alisema:
“Mwanangu shida huyo imekwisha, dawa nitakayokupa nitakupa siku tatu usipompata njoo uchome moto dawa zangu.”
Inaendelea.
No comments:
Post a Comment