Social Icons

Sunday, 7 September 2014

HADITHI: Missed call ya shemeji -3


Usiku wa siku hiyo, Beka na mke wake, Aisha walitofautiana chumbani, ikawa zogo…
“Mimi nataka nikisema unisikilize, siyo kujibishanajibishana, we mwanamke vipi?”
“Vipi kwani vipi, wewe mwanaume vipi?
ENDELEA KIVYAKO…

Dada wa Aisha, alisikia malumbano hayo kupitia chumbani anakolala, akashtuka na kukaa kitandani ili asikilize kwa undani.

“Kwani ina maana mimi sichoki siyo? Kila siku, kila siku utadhani chakula bwana,” alisikika Aisha akisema.
Dada mtu alijisikia vibaya sana kwani alijua kilichokuwa kimetawala malumbano yao ni masuala ya unyumba kama si ndoa…

“Sasa huyu mdogo wangu, kama amefikia hatua ya kusema hivyo kwa mumewe, ndoa si itamshinda! Mke anaweza kweli kusema maneno kama hayo kwa mumewe? Kwa hiyo anataka mumewe achukue uamuzi gani sasa? Akitoka nje ya ndoa maneno, ooo… nasalitiwa! Kumbe yeye mwenyewe ndiye chanzo.”
***
Asubuhi iliyofuata, dada mtu aliamka mapema, akaenda sebuleni kama ilivyo kawaida yake, akakaa na kuwasha Tv kuangalia vipindi mbalimbali, mara akatokea Beka.
“Za asubuhi shemeji?” alisalimilia Beka huku akionesha uso usiokuwa sawa tofauti na kawaida yake ya kupenda kumtania shemeji yake huyo.

“Salama shemeji, pole…ee! Umeamka salama?” dada wa Aisha alijichanganya hapo, lengo lake aseme umeamkaje, akajikuta anatoa pole kwa sababu mawazo yake yalikuwa kwa lile tukio la usiku.
“Nimepoa shemeji,.” Alisema Beka, shemeji yake akashangaa kuona mwenye pole ameikubali bila kuuliza ni pole ya nini.

Hiyo ilimpa nguvu dada mtu kuuliza zaidi…
“Kwani shemeji nini kimetokea?”
“Aah! Shemeji mdogo wako wakati mwingine siyo.”
“Kafanyaje?”
“Unajua….”

Beka alipoanza kusema tu, alisikia mlango wa chumbani unafunguliwa, ina maana Aisha anatoka, akasema…
“Shem nitakusimulia baadaye.”
“Poapoa!”
***
Ni kweli Aisha ni mdogo wa Ime, lakini hudhani ni mapacha kwani udongo uliotumika kumuumba Ime ni wa aina yake, pengine ni huo wanaouita mfinyanzi kwani kwa macho haikuwa rahisi kumjua nani mkubwa, nani mdogo.

Mbaya zaidi walifanana hata sura na maumbo, tena umbo la Ime usiseme, alifungasha kwelikweli, kwa vile tu alichakazwa na maisha magumu ya kwa mume wake alikotoka.

Ila yeye pia alijaliwa weupe kumzidi mdogo wake Aisha, sasa kama angekuwa na maisha ya mjini na kutumia yale ‘mambo yetu’ huenda weupe wake ungefanana na wa Mchina kama si Mzungu achilia mbali Mwarabu.
***
Aisha alitoka, akamkuta dada yake anawekaweka vitu sawa sebuleni huku akifuatilia matangazo kwenye Tv…
“Shikamoo dada.”

“Marhaba, umeamkaje Aisha?”
“Salama tu, naona unapangapanga!”
“Ah! Usingizi unaisha mapema sana mdogo wangu, mawazo kibao.”
“Usiwaze sana dada, nimekwambia we ishi hapa, kwani tatizo lako nini?”
“Najua, lakini mtu kwake mdogo wangu.”

“Imeshindikana sasa, utalazimisha dada?”
“Lakini kweli mdogo wangu.”
Aisha alipita kwenda jikoni kisha akaenda uani na kumalizia na chooni kuangalia usafi ulivyofanywa na msichana wa kazi.

Mumewe alirudi ndani akiwa ameshaoga, alijiandaa akatangulia kutoka kwenda kazini…
“Shem, mimi nawahi kibaruani, baadaye.”
“Baadaye shemeji yangu, uniletee matunda bwana.”
“Sawa shemeji.”

Aisha yeye alicheka tu kisha akamtania mume wake…
“Na mimi baby uniletee matunda.”
“Sawa.”

Ndani ya moyo, dada yake alipata tabu sana kwani alijiuliza kama Aisha anasema vile asubuhi wakati usiku alitoka kumwekea ngumu mumewe kuhusu tendo la ndoa ni sahihi? Aliona si sahihi wala si sawasawa kwa mwanamke mwenye akili zake timamu kichwani. 

Alihisi mdogo wake ameacha maadili waliyofundishwa na wazazi wao  na kushika yake ambayo yametawaliwa na ubabe na kutokuwa na adabu ndani ya nyumba.

Alitamani sana kummbwatukia mdogo wake lakini moyoni akasema kwa sababu shemeji yake alimwambia atamsimulia baadaye hivyo ni muhimu kusubiri muda ufike ili amsikie ndipo aone uwezekano wa kuzungumza na Aisha.
***
Siku hiyo, Beka alirejea nyumbani saa kumi na mbili jioni. Sebuleni alimkuta shemeji yake…
“Ohoo, karibu mume wangu, pole kwa kazi jamani?”

“Nimekaribia mke wangu, nashukuru sana kwa kunipa pole kwa kazi,” alisema Beka huku akiachia mfuko mkubwa wa rambo uliokuwa ukipokelewa na shemeji yake huyo.
Alifikia kukaa kwenye kochi, akavua viatu, soksi na kuhema kidogo kisha akaulizia kama mke wake alisharudi…

“Mke mwenzio amerudi?”
“Bado, tena kanipigia sasa hivi, kasema akichelewa, nianze kuchambua mchele maana kuna foleni,” alisema shemeji huyo akipeleka jikoni ule mfuko ambao ndani yake mlikuwa na matunda.
“Ni kweli kuna foleni sana.”

Shemeji alipoona Beka ndiyo amewahi kufika kuliko mkewe, aliamini ndiyo wakati muafaka wa kumsikia alichotaka kumwambia…
“Shemeji,” aliita dada wa Aisha huku akikaa…
“Yes shemeji…”

“Asubuhi uliishia kuniambia utaniambia, ni nini kwani shemeji?”
“Ah! Shemeji mdogo wako anazinguaga sana. Basi tu! Hivi unaweza kuamini kwamba wakati mwingine inapita wiki tatu hataki kunipa unyumba? Ni akili hizo?”
“Kweli?”
“Kabisa.”

“Ah! Aaaa! Madai yake?”
“Si ya msingi…”
“Kwamba..?”

“Anakuwa amechoka!”
“Na..?”
“Anajua yeye.”

“Mh!” aliguna dada mtu huyo huku akimwangalia shemeji yake kwa macho ya huruma…
“Sasa ina maana unaishije shemeji?”
“Kivipi shemeji?”   
 
Inaendelea.

No comments:

 
 
Blogger Templates