“Karibuni,” mzee Mukti aliwakaribisha, alikuwa mzee wa makamo mwenye mwili ulioshiba. Alivalia kanzu nyeupe na kibalaghashia.
“Asante mzee, shikamoo.”
“Marahaba, mmh! Mna shida gani?”
“Ni mwenzangu hapa, mimi nimemleta tu,” Sofia alisema.
“Ndiyo nimeona hapa mwenye matatizo ni mmoja, haya bibi shida yako nini?”
Subira alielezea shida iliyompeleka pale, baada ya kumsikiliza alisema:
“Mwanangu shida hiyo imekwisha, dawa nitakayokupa nitakupa siku tatu usipompata njoo uchome moto dawa zangu.”
“Nitashukuru mzee wangu.”
SASA ENDELEA...
Subira alipewa dawa ya kuweka kwenye chai na juisi, kufukiza chumbani kwake na ya kuoga, kazi yake haikuchukua muda mrefu.
“Mzee wangu ndiyo kiasi gani?”
“Hapana leo sitaki hela yoyote kwa vile huna hela ya kunipa, najua baada ya mwezi utaleta zawadi yangu.”
“Nashukuru mzee.”
“Haya kwaheri.”
Walitoka kwa mganga kuelekea barabarani huku Subira akiwa haamini kwa vile hawakutumia muda mrefu kupata huduma tofauti na watu waliowakuta. Walipanda daladala na kurudi nyumbani, wakiwa njiani Subira alikumbuka kuna kitu alisahau kuuliza.
“Sofi kuna kitu nimesahau kuuliza.”
“Kitu gani?”
“Kuhusu matumizi ya kwenye chai na juisi naweka kiasi gani?”
“Kumbe hilo, kiasi kidogo tu nusu kijiko cha chai.”
“Mara ngapi?”
“Subira mara moja, kwani mumeo useme utampa hata jioni.”
“Nilitaka kujua tu si unajua dawa hizi ukikosea masharti umeharibu kila kitu?”
“Ni kweli, lakini dawa za mzee huyu hazina masharti magumu kwa vile anaziamini.”
Baada ya kufika nyumba wakiagana kila mmoja alikwenda kwake, Subira pamoja na kuhakikishiwa kumpata Thabit kwake aliona kama ni uongo usiowezekana kwa mtu kumuwekea dawa kwenye chai na kumkubali kimapenzi.
Aliachana na mawazo yale aliangalia dawa alizofunga kwenye karatasi na kuzisoma, alichukua ya kuoga na kuweka kidogo kwenye maji na kwenda kuoga kisha alipata chakula.
Kabla ya kulala aliwasha moto wa mkaa na kuweka mikaa michache ya moto kwenye bakuli. Alichukua dawa ya kujifusha na kujifunika shuka kisha aliiweka kwenye moto huku akinuiza maneno ya kuhakikisha Thabit anaingia mikononi mwake. Baada ya kujifusha alipanda kitandani kulala.
***
Siku ya pili Subira aliwahi kazini na kufanya usafi kisha alimchemshia chai bosi wake na kuiweka kwenye chupa na kurudi sehemu yake kuendelea na kazi. Baada ya muda Thabit aliingia na kumsalimia kama ilivyo kawaida yake siku zote huwa mcheshi kitu kilichomchanganya Subira kushindwa kueleza badadiliko lolote kutokana na dawa alizofanya usiku.
Subira muda wote kazi ilimshinda macho yake hayakucheza mbali na saa yake ndogo ya mkononi kuangalia muda wa kumpelekea chai bosi wake. Kila alipoiangalia aliona kama mishale imesimama. Mapigo muda wote yalimwenda kasi kutokana na kuwa na wasiwasi na kitu alichotaka kukifanya kitakuwa na matokeo gani.
Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kama bosi wake akigundua na kuamua kumfukuza kazi itakuwa kilio kwake. Aliona kama saa ya mkononi inamdanganya alibadili na kuangalia ya kwenye kompyuta. Nayo hakuiamini aliangalia kubwa ya ukutani ilimuonesha bado dakika tano muda wa kupeleka chai utimu.
Aliporudia kuangalia saa zingine zilionesha zilikuwa sawa ila wasiwasi wake ulifanya azione kama zimesimama. Alinyanyuka hadi jikoni na kuchukua kikombe cha bosi wake na kufungua kikaratasi alichoweka dawa ya unga na kuchukua kidogo na kuiweka kwenye kikombe huku akinuiza kumpata bosi wake na kuiweka chai ya maziwa na kukoroga huku akinuiza kuukoroga moyo wake kama ile chai na kumfanya amejaze moyoni kama utamu wa chai ile.
Baada ya kukoroga alijifuta vizuri na kuibeba chai na kwenda ofisini, alipofungua mlango alikutana na tabasamu pana la bosi wake.
“Karibu Subira.”
“Asante bosi.”
“Hongera umependeza,” kauli ile ilimpa matumaini, tangu aanze kazi pale hakuwahi kusifiwa na bosi wake.
Subira aliitenga chai juu ya meza ya bosi wake na kumkaribisha.
“Karibu bosi.”
“Asante.”
Alisema huku akishika mkono wa kikombe na kunyanyua ili apeleke mdomoni. Subira alikuwa amesimama pembeni kumuangalia bosi wake akipiga funda la chai ndipo aondoke kwenda kuendelea na kazi kusubiri kutoa vyombo na kuangalia matokea ya siku tatu aliyopewa kumtia mikononi Thabit.
Kikombe kilipokaribia mkononi alishtuka kukiona kikipasuka na kutoa mlio huku chai ikitawanyika na kumuunguza kifuani kitu kilichofanya Thabit apige kelele za maumivu huku Subira akipigwa bumbuwazi na kutoamini kikombe kupasuka kama kimefungwa bomu.
“Bosi nini?” Subira aliuliza kwa mshtuko.
“Hata najua nashangaa kikombe kupasuka kama kimefungwa bomu.”
“Pole sana bosi hukuungua?”
“Kiasi si sana.”
“Itabidi uende hospitali.”
“Lazima kwanza nirudi nyumbani nikabadili nguo.”
Thabit alivua shati lililochafuka kwa chai alivaa koti na kutoka kuelekea nyumbani kubadili nguo. Baada ya kuondoka bosi wake, Subira aliingia woga moyoni mwake na kujiuliza kile kilichotokea ni nini. Kwa nini hakikutokea siku zote kitokee alipoweka dawa?
Alijiuliza Thabit akigundua alitaka kumuwekea dawa atamchukulia hatua gani. Mawazo yale yalimchanganya sana na kujikuta akikosa raha na kuanza kujilaumu kujiingiza kwenye mambo ya kishirikina. Aliamua kumpigia simu shoga yake kumueleza yaliyotokea ofisini.
Baada ya simu kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo shoga vipi?”
“Mambo mabaya.”
“Kivipi?” Sofia alishtuka.
Alimweleza kilichotokea muda mfupi na kuichanganya akili yake.
“Wewee! Hakijamponyoka?”
“Hakijamponyoka kimepasuka.”
“Amekwambia au umekiona kwa macho yako?”
“Yaani nimeona mwenyewe kwa macho yangu.”
“Kimepasuka kabisa?”
“Tena kimelia kama bomu.”
“Mmh! Hukukosea kitu?”
“Sijakosea nimefuata kila hatua toka jana usiku.”
“Sasa itakuwa nini, mbona mara zote haikikutokea kitu kama hicho.”
“Nikuulize wewe!”
Inaendelea.
No comments:
Post a Comment