Social Icons

Wednesday, 24 September 2014

HADITHI: Nilioa jini nikamsaliti -21


Alijikuta akishtuka na mapigo ya moyo kwenda mbio na kuamini mumewe alikwenda kujihami lakini yule ni mpenzi wake.
“Thabit,” alimwita kwa sauti kama ya mtu mwenye pumu.
“Naam mke wangu,” Thabit aliyekuwa ameshika mlango wa ofisi ili afungue aligeuka kumsikiliza mke wake.
SASA ENDELEA...

Alipogeuka hali ilikuwa ileile ‘love bite’ zilikuwa kifuani na kwenye mashavu na mdomoni.  Subira alizidi kuchanganyikiwa na hali ile na kuona jinsi Thabit asivyo muaminifu na alitoka ili kumhadaa lakini ndani kulikuwa na matendo ya mapenzi.
“Mume wangu!”
“Naam.”

“Unanifanyia nini?” Subira alimuuliza huku akiangua kilio.
“Kivipi?” Thabit alishtuka.
“Yaani unanigeuza mtoto mdogo kwa nini?” Subira aliuliza huku akilia kitu kilichozidi kumshangaza Thabit na kutaka kujua kulikoni.
“Mke wangu umekuwaje leo?”

“Siyo nimekuwaje, ila unaonesha jinsi gani ulivyo muongo tena si muaminifu.”
“Mbona sikuelewi una nini mke wangu?” Thabit alizidi kumshangaa mkewe na lawama zake.
“Unanidanganya eti umemfukuza yule mwanamke kama mbwa kumbe ndani mlikuwa na matendo ya kimahaba.”

“Mimi Thabit?” Thabit aliuliza huku akijishika kifuani kwake.
“Ndiyo, hata kama kusoma sijui basi picha nimeiona.”  
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Hebu angalia kifuani mwako.”
Thabit alijitazama na kukuta kuna love bite  na kushtuka.
‘Ha!”

“Unashtuka nini? Eti nilimfukuza kumbe mpenzi wako Mungu kakuumbua,” Subira alisema kwa hasira huku amemshikia pua.

“Hii ni ajabu vitu hivi vimetoka wapi, nakuapia mke wangu hakunibusu kwenye nguo alinibusu shavuni kwa nguvu na kutoka baada ya kumkatalia mambo aliyokuja nayo ya kimahaba,” Thabit alijitetea.
“Siwezi kukuamini naona hunipendi na kumwita yule mwanamke mzuri ili kunionesha.”
“Sijamwita hata hizi love bite nashangaa kuziona.”
“Si mbele tu angalia na nyuma.”

Kauli ile limfanya Thabiti kuvua shati ili aangalia, hali ilikuwa vilevile alama ya midomo ilikuwa kwenye shati jeupe na kumfanya Thabit abaki akiwa ameduwaa na kujishangaa alama zile zilitoka wapi.
Wakati huo Subira alikuwa akiendelea kulia kwa kuamini kwa uzuri wa yule mwanamke hana chake. Moyoni aliapa kama aliweza kumdhibiti jini basi hatashindwa kumdhibiti mwanadamu mwenzake hata angekuwa mzuri kama malaika.

“Mke wangu nakuapia yule mwanamke hakunibusu kote huku bali shavuni kwa nguvu na kutoka nje.”
“Si kweli Thabit una uhusiano naye hawezi kukubusu tu bila kuwa na uhusiano naye, kama umenichoka nipe talaka yangu,” Subira alitikisa kiberiti.

“Hapana mke wangu siwezi kufanya hivyo nakuhakikishia nakupenda wewe peke yako,” Thabit alisema huku akipiga magoti mbele ya mkewe kuomba afute kauli ya kuomba talaka.
“Mume wangu hunipendi,” Subira alijilaza kiuongo kuonesha ameumizwa.
“Haki ya Mungu sina uhusiano wowote na huyo mwanamke ndiyo maana nimekuambia asimruhusu kesho akija.”

“Nimekuelewa mume wangu,” Subira alisema huku akimnyanyua mumewe alipopiga magoti. 
Thabit alirudi ofisini na kumuacha Subira akiwa na mawazo juu ya kauli ya mumewe kuhusu alama za midomo ya busu kwenye shati na usoni. Alijiuliza kama mumewe hakubusiwa sehemu zote zile basi aliamini yule mwanamke huenda si kiumbe wa kawaida.

Japokuwa alikuwa hajawahi kumuona jini lakini alisikia sifa zao kuwa majini wa kike huwa wazuri sana. Alijikuta akiingiwa na wasiwasi labda yule mwanamke ni jini, lakini alipingana na mawazo yake kutokana na kuelezwa na mzee Mukti Buguju kuwa jini hata wasogelea.

Lakini alitaka kujiridhisha alimpigia simu mzee Mukti ili kuupata ukweli wa tukio la yule mwanamke mrembo aliyemtia wasiwasi hasa kutokana na kauli za mpenzi wake. Baada ya simu kuita kwa muda bila kupokelewa alirudia tena mara mbili lakini haikupokelewa pia.

Alishtuka simu ya mzee Mukti kushindwa kupokelewa, alijiuliza kuna nini. Wakati akiwa katika lindi la mawazo simu yake iliita. Alipoangalia ilikuwa inatoka kwa mzee Mukti, aliipokea haraka.
“Haloo babu,” alipokea huku akihema.

“Eeh! Vipi mjukuu  mbona presha juu kuna nini tena?” mzee Mukti alishtuka.
“Kuna kitu kimenichanganya mzee wangu!”
“Kitu gani?”
Subira alimueleza kilichotokea muda mfupi ofisini kwake, habari ile ilimshtua sana mzee Mukti akamuuliza:

“Unasema huyo mwanamke aliingia ofisini?”
“Ndiyo.”
“Yukoje?”
“Mmh! Mzee wangu uzuri wa yule mwanamke ndiyo kwanza leo nimeuona, tena hata manukato yake ni mageni puani kwangu, sijawahi kuyasikia.”
“Mmh! Subiri.”

Mzee Mukti alikata simu na kuangalia kwenye rada zake alijikuta mwili ukimtetemeka baada ya kuona ni jini Nargis mke wa Thabit waliyemdhibiti asiingie popote alipo Thabit na mkewe. Alijiuliza amekosea wapi mpaka kuingia alipopafunga, baada ya kuangalia zaidi aligundua ujaji wake ndiyo uliomaliza nguvu za kumzuia pale alipokwenda kibinadamu tofauti na mwanzo alipokwenda kijini.

Inaendelea 

 Chanzo globalpublishers 

No comments:

 
 
Blogger Templates