MAJINA sita yanatajwa kuliwania Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hata hivyo wengi wanatarajiwa kujitokeza kadiri siku zinavyosogea kuelekea 2015.
Sababu kuu inayotajwa kuchangia wingi wa wanachama wanaojitokeza kuonyesha nia ya kulihitaji jimbo hilo, ni imani yao kubwa kwamba chama hicho kitakamata dola baada ya uchaguzi wa mwakani.
Tayari wanasiasa ndani ya chama hicho wanaelezwa kujipa matumaini makubwa ya kushika dola mwakani, na moja ya dalili ni wananchi wengi zaidi, wakiwemo watumishi wa umma, wafanyabiashara na wasomi kujitokeza hadharani kukiunga mkono pamoja na kuwania nafasi mbali mbali za uongozi kupitia chama hicho. Ni jambo ambalo miaka mitano iliyopita lilihitaji ujasiri uliopitiliza.
“Wanasiasa ndani ya CHADEMA wanaangalia zaidi ya ubunge, nafasi zile za DC, RC na uwaziri, kikikamata dola, hizo ni nafasi zilizo wazi kwao na zenye kuhitaji watu wenye uwezo, leo hii wapo ndani ya CHADEMA,” anasema Christopher Nyenyembe ambaye ni Mwandishi Mwandamizi Gazeti la Tanzania Daima na Mjumbe Kamati ya Utendaji ya chama hicho Jimbo la Mbeya Mjini.
Katika uchaguzi uliopita, mwaka 2010, Nyenyembe alikuwa miongoni mwa wagombea watatu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, ambapo Joseph Mbilinyi aliibuka mshindi.
Nyenyembe anakiri kuonyesha nia ya kuliwania tena jimbo hilo, na matumaini yameongezeka baada ya kufanikiwa kuingia katika kamati tendaji ya jimbo hilo ambapo aliongoza katika wagombea 26.
Lakini jambo moja linalotajwa kukisumbua chama hicho katika uchaguzi ujao ni kujitokeza kwa makundi ndani ya chama yanayotokana na waonyesha nia hao, ambao safari hii sio wepesi kama ilivyozoeleka huko nyuma.
Inahofiwa kujitokeza kwa migawanyiko kama inayoikabili CCM katika kila uchaguzi, ambapo wanaoshindwa hujimega na kuamua kumuunga mkono mgombea wa chama kingine ikiwa kuonyesha hasira zao pamoja na kutoridhishwa na uamuzi wa chama chao kwa mgombea anayepitishwa kupeperusha bendera ya chama.
Hofu hiyo ni kwamba makundi yanayojengeka ndani ya CHADEMA kutokana na wenye kuonyesha nia ya kuliwania jimbo hilo, yatafanya kama ambavyo yamekuwa yakifanya makundi ndania ya CCM, jambo ambalo kwa mijini ni la kawaida sana kutokea.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija anakiri kujitokeza kwa makundi ndani ya chama yatayotokana na wagombea wao, jambo anajipa moyo kwamba hayajafikia hatua hiyo ya kukisaliti chama chao na kiasi cha kuunga mkono chama kingine.
“Hatujafikia hapo ku support vyama vingine, makundi lazima yapo na yatakuwepo, huwezi kuyazuia kwa chama kilipofika,” anabainisha Mwambigija katika mahojiano yake ya simu na Raia Mwema.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vyingi, Mkoa wa Mbeya umeshuhudia mifarakano ndani ya Chama cha Mapinduzi iliyotokana na makundi ya wagombea, na moja ya sababu inayotajwa kumbeba mbunge wa sasa wa jimbo hilo, ni mgawanyiko uliotokea kati ya kundi la Thomas Mwang’onda lililoshindwa na lile la Benson Mpesya lililoshinda katika kura za maoni ndani ya CCM.
Mbilinyi alinufaika na makundi hayo, kama ilivyokuwa kwa Polisya Mwaiseje katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi aliposhinda ubunge wa jimbo hilo, kundi la Mwang’onda linaelezwa lilimuunga mkono mgombea huyo wa CHADEMA ikiwa ni ujumbe wa hasira zao dhidi ya kushindwa kwa mgombea wao.
Hata hivyo hakanushi wala kukubali juu ya kutajwa kwake kuonyesha nia ya kuwania Jimbo la Mbeya Mjini, japo anadokeza kuwa labda kwa Jimbo la Rungwe Magharibi, na mjini anasema labda aliyepo aharibu sana.
Mwambigija anajilinganisha na bunduki ya msaada, kwamba hutengeneza pale wengine wanapoharibu, na anaenda mbali zaidi akitumia pia msemo wa Mzee John Malecela aliyewahi kuitwa jina la tingatinga, kwa maana ya kutengeza njia kwa wengine kupita huku yeye mwenye akizuiwa kuitumia.
Akionyesha kukubalika kwake ndani ya chama hicho jimboni humo, Mwambigija anasema katika mkutano unaotumika kumchagua pia mbunge ulimpa kura 240 kati ya 358, hivyo akiamua kuomba zitazidi.
Miongoni mwa majina yanayotajwa ni pamoja na waliokuwa washirika wa Mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Joseph Mbilinyi, wakielezwa kuwa ndio waliofanikisha ushindi wa mbunge huyo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010.
Sababu kubwa inayotajwa na wapambe hao wa Mbilinyi, ni pamoja na kwamba mbunge huyo amekuwa akichafua hali ya hewa jimboni humo, hivyo kuwapa kazi ya kila wakati kusafisha hali ya hewa.
Pamoja na washirika hao, wapo pia wanachama waandamizi wa CHADEMA mkoani humo walioonyesha nia ya kuliwania jimbo. Wanachama hao ni pamoja na Mratibu wa Chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu, Frank Mwaisumbe Mponzi na Mwalimu Kapange. Hawa wanajumika na kina John Mwambigija na Nyenyembe kukamilisha orodha iliyopo kwa sasa.
Zipo sababu zingine zinazotolewa kutokana na ongezeko la wanachama wa CHADEMA mkoani Mbeya kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi ya ubunge kwa jimbo hilo na hata mengine mkoani humo, lakini iliyo kuu ni watu kuondokana na hofu iliyokuwepo huko nyuma kuhusu vyama vya upinzani.
Katika chaguzi zilizopita, watumishi wa umma na wafanyabiashara walihofu kujihusisha na vyama vya upinzani, ikiwemo kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama hivyo, wakihofia kuharibikiwa katika shughuli zao.
Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka 2010 uliipa nguvu zaidi CHADEMA, baada ya kushinda majimbo mbal mbali muhimu nchini pamoja na na kata kwa nafasi ya udiwani. Nguvu hiyo imeipatia CHADEMA taswira chanya, imehamasisha watu na sasa wanakiona kuwa chama pekee kinachoweza kuwafikisha katika malengo yao ya kisiasa.
Mwaisumbe anaitaja sababu ya wimbi hilo la wanasiasa kuonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi mbali mbali ndani ya chama na uwakilishi wa wananchi kuwa ni kutokana na watu kubaini kuwa CHADEMA ni chama cha demokrasia kweli na ndicho pekee chenye kutoa nafasi kwa watu kuyafikia malengo yao ya kisiasa.
“Hakuna rushwa wala matabaka ya aina yoyote, yeyote anagombea,” anasema Mwaisumbe.
Hata hivyo hoja hiyo ya Mwaisumbe, kuhusu suala la kutokuwepo rushwa na matabaka katika chaguzi za chama hicho, inapingwa vikali na baadhi ya wanachama wake, wakibainisha kuwa tofauti iliyopo na washindani wao ni kiwango cha rushwa.
“Katika uchaguzi uliopita, watu walioamini katika hilo, kwamba hakuna rushwa, walijikuta wakipigwa mweleka na wenzao waliotumia rushwa kwa kuwanunua au kuwalaghai wajumbe,” anasema mwanachama mmoja wa chama hicho jijini Mbeya.
Wapo wanaoenda mbali zaidi wakibainisha kuwa hata zile ahadi za kujenga ofisi za kata za chama iwapo mgombea atachaguliwa, ilikuwa rushwa kwa sababu zilitolewa kwa lengo la kuwashawishi wajumbe, na zaidi ya hapo kulikuwepo na madai ya kuwapo wajumbe wa kutengenezwa na baadhi ya wagombea.
Hata hivyo, Mwaisumbe hakanushi wala kukubali kuhusu kutajwa kwake kuliwania jimbo hilo, akisema kuwa suala ya yeye kutajwa hawezi kuzuia watu kusema, na kwamba kila mtu ana tafsiri yake.
“Sijafikiria chochote kutokana na majukumu niliyonayo ya uratibu wa kanda, kusema kila mtu anakuwa na tafsiri yake, huwezi kuzuia,” anasema Mwaisumbe katika mahojiano yake ya Raia Mwema kwa njia ya simu.
Pamoja na kutopata kauli ya mbunge wa sasa, Mbilinyi, kutokana na kutopokea simu baada ya kupigiwa mara kadhaa, taarifa za ndani ya chama hicho zinathibitisha pasipo shaka kwamba atakitetea kiti chake baada ya kuonyesha nia ya kufanya hivyo.
Jambo moja lipo wazi, kwamba makundi yamejitokeza ndani ya chama hicho, makundi yenye kutokana na wanachama walionyesha nia ya kuliwania, na wafuatiliaji wa siasa za Mbeya wanaiona sinema ya wapambe wa wagombea wa CHADEMA kuhamia CCM na wa CCM kuhamia CHADEMA katika uchaguzi wa mwakani, kitakachoamua ni jinsi gani kila chma kitachanga karata zake kukabiliana na makundi hayo.
Chanzo Raia Mwema

No comments:
Post a Comment