Woga ulimtawala alitaka kukimbia nyumba ilikuwa na mtikisiko mkubwa huku akisikia sauti za watu wakikimbia na vishindo kama watu wakiruka toka juu na kutua chini.
Alijipa moyo na kuendelea na zoezi lake, nyumba ilikuwa kama imekumbwa na tetemeko zito, hakuacha kunyunyuzia maji kila kona kama alivyoelekezwa mpaka alipoingia chumba cha Thabit alishangaa kukuta chumba kizuri sana chenye kitanda kizuri ambacho hakuwahi kukiona katika maisha yake.
Kilikuwa kimenakshiwa na fito za dhahabu na shuka zake za uzi wa hariri. Kitandani alikuwa Thabit amelala hajitambui, alimuangalia kidole cha mkono wa kulia hakuiona pete. Hakushangaa kwa vile aliisha elezwa kila kitu na mzee Mukti alijua imeenda wapi.
Mara moja alimuosha maji ya dawa kichwani na kumuacha kitandani bila kumuamsha na kwenda bafuni. Bafu nalo lilikuwa zuri likinukia manukato mazuri sana. Hakupoteza muda alifungulia maji kwenye beseni kisha aliweka dawa kidogo na kuyachanganya.
Alioga maji ya dawa na kubakisha nusu, alirudi chumbani ambako alimuamsha Thabit ambaye aliamka kwa shida. Alionekana kama mtu asiyejielewa alimshika mkono hadi bafuni ambako alimuosha maji ya dawa. Baada ya maji kumpata mwili nzima Thabit alirudi katika hali yake ya kawaida.
Alishangaa kumuona Subira aliyekuwa kwenye vazi la khanga moja mbele yake.
“Vipi tumekuja saa ngapi?” Thabit aliuliza akiwa anamtazama.
“Tumekuja muda,” Subira alidanganya.
Alimshika mkono na breki ya kwanza ilikuwa kitandani, kwa vile Thabit alikuwa hajielewi alifanya mapenzi na Subira. Baada ya kustarehe kila mmoja alipitiwa usingizi. Subira alishtuka usingizini, alipoangalia saa ya ukutani ilimuonesha saa nne usiku. Kwa vile hakutakiwa kulala alimshtua Thabit aliyekuwa usingizini.
“Thabit.”
“Naam.”
“Mpenzi naomba niondoke.”
“Kwa nini usilale uondoke kesho?” Thabit alijibu huku akiangalia saa ya ukutani.
“Hapana mpenzi sikuaga nyumbani kuja huku ulinilazimisha kwa vile nakupenda nilikukubalia sikutaka kukuudhi mpenzi wangu,” Subira alizidi kutengeneza uongo ambao Thabit aliukubali.
Thabit alitaka kumsindikiza, lakini Subira alikataa kusindikizwa kwa vile alitakiwa usiku ule lazima arudi kwa mzee Mukti ili amalize mambo kabisa. Alitoka nje na kukodi gari mpaka Kigamboni na kukodi Bajaj mpaka Mji Mwema kwa mzee Mukti Buguju.
Alifika majira ya saa tano kasoro, hakuchelewa alipatiwa tiba ya mwisho na kupewa hirizi ndogo ambayo ataifunga kwenye mkono sehemu za begani. Pia alipewa dawa ya kuweka pembe nne za jumba lile kama kinga ili majini yasiingie.
“Mzee zingine ungenisaidia wewe.”
“Basi weka unga huu kwenye kona kila siku, wiki moja baada ya kuanza kukaa pale nitakuja kuzindika nyumba pia sehemu zote za biashara ili zisichukukiwe na nguvu za kijini.”
“Sawa kama hivyo.”
“Dawa ya kufukiza utafukiza kila ikifika saa sita usiku muda ambao majini huja duniani.”
“Sawa nitafanya hivyo, mzee wangu nina zawadi kubwa nimekuandalia.”
“Wewe tu.”
“Kuna kitu nilisahau, unatakiwa kuwahi nyumbani kwa mpenzi wako ili umuandalie kifungua kinywa. Nitakupa dawa ambayo utatumia kumpikia chakula ili kuondoa chakula alichokuwa akila toka ujinini. Kuanzia kesho utahamia kwake hapo hutotoka tena mpaka ndoa yenu.”
“Nitafurahije mzee wangu.”
“Kazi imekwisha sasa hivi Thabit ni mume wako.”
Baada ya zoezi zito lililoisha saa sita usiku. Subira hakulala alikodi gari mpaka kwake na kulala na kuamka alfajiri na kununua vitu vya kwenda kumuandalia kifungua kinywa Thabit. Alimkuta bado hajaamka aliingia ndani na kwenda jikoni kumuandalia kifungua kinywa kisha alimuamsha aoge afungue kinywa na kuondoka pamoja kwenda kazini.
***
Chini ya bahari jini Nargis mke wa Thabit alishtuka kitandani kwake na kuona kiza sehemu iliyokuwa ikimuonesha kila alipokuwa mume wake. Alijaribu kutumia nguvu za kijini kumvuta mpenzi wake lakini hakumuona. Alichanganyikiwa na kusimama na kuanza kutangatanga chumbani kama kuku anayetaka kutaga.
Alitoka chumbani bila ushungi kichwani hadi sebuleni alipokuwa amekaa mama yake malkia Zabeda na dada yake Hailat ambao walishtuka kumuona Nargis katika hali ya taharuki.
“Vipi mbona hivyo?” mama yake alimuuliza.
“Baba Zumza (Thabit) simuoni.”
“Humuoni kivipi?” dada yake alimuuliza.
“Nimeshtuka usingizini na kuona kiza kizito sehemu niliyotegesha kumuona kila wakati,” Nargis alisema machozi yakimtoka.
“Kwani pete yake si anayo?” dada yake Hailat aliuliza.
“Ndiyo lakini nashangaa simuoni.”
“Basi atakuwa ameivua.”
“Hebu rudi kwanza ndani ukaangalie vizuri,” mama yake alimshauri.
Nargis alirudi ndani kuangalia tena, lakini alikuta hali ni ileile kiza kizito kilitanda eneo lile.
Itaendelea
Chanzo Globalpublishers
No comments:
Post a Comment