Social Icons

Thursday, 4 September 2014

JWTZ LATIMIZA MIAKA 50


WIKI hii, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetimiza miaka 50 kamili tangu kuanzishwa kwake katika mazingira magumu. Kutoka kuwa Jeshi lililoasi hadi kuwa Jeshi la Ukombozi wa Mwafrika ni hatua kubwa sana.

Katika miaka yake 50, JWTZ imebaki kuwa miongoni mwa taasisi chache zilizobaki nchini ambazo zinaheshimika na jamii yote kwa ujumla.

JWTZ ni Jeshi ambalo limekuwa sehemu ya Watanzania katika nyakati zote za shida na raha. Kwenye sherehe za kitaifa limetuburudisha na kwenye nyakati za vita limetupa ushindi. Iddi Amin ni shahidi wa hili.


Katika namna ya kipekee kabisa, sisi wana Raia Mwema tunapenda kupongeza taasisi hiyo kwa ujumla wake lakini pia kutaja wachache ambao mchango wao binafsi hautasahaulika.

Kwanza kabisa ni kwa Amri Jeshi Mkuu wa Kwanza wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye ndiye aliyeamua ni namna gani JWTZ itapaswa kuwa. Badala ya kuwa Jeshi la Mkoloni, liwe Jeshi la Wananchi.


 Badala ya kuwa Jeshi la Mabavu na Vitisho, liwe Jeshi la Upendo na Ukombozi ! Pasipo kuwa na fikra sahihi za Amiri Jeshi Mkuu, Jeshi letu lisingekuwa na sifa hizi ilizonazo leo.

Tunapenda pia kuwashukuru Jenerali Mirisho Sarakikya na Kanali Ameen Kashmiri ambao ndiyo waliokuwa viongozi wa juu wa JWTZ wakati likianzishwa. Hawa ndiyo walisimamia maono ya Amiri Jeshi na kuhakikisha Jeshi letu linakuwa na viwango vya kimataifa.

Shukrani pia kwa Brigedia Jenerali Hashim Mbita ambaye kazi yake katika Ukombozi Kusini mwa Afrika ililetea Tanzania heshima kubwa miongoni mwa jirani zetu. Watanzania leo wanatembea kifua mbele katika nyingi ya nchi za Kusini mwa Afrika kwa sababu ya kazi walizofanya akina Mbita.

Shukrani kwa Majenerali David Musuguri, Mwita Marwa, Ernest Mwita Kiaro, John Walden, Imran Kombe, Abdallah Twalipo, Benjamin Msuya, Robert Mboma na wengineo waliofanikisha ushindi wakati wa Vita ya Kagera.


Kuna maelfu waliopoteza maisha yao katika matukio mbalimbali ya kishujaa kwa ajili ya faida ya Watanzania wote na kwa sababu za wazi hatuwezi kuwataja katika nafsi hii ndogo.

Ifahamike tu kwamba Raia Mwema linathamini mchango wa askari wote; wake kwa waume, ambao wameamua kujitolea jasho na damu zao kwa ajili ya kuifanya Tanzania iwe sehemu salama ya kuishi.

Tunaamini kwamba huu ni mwanzo wa miaka mingine 50 inayokuja ya JWTZ imara zaidi, thabiti zaidi na eledi zaidi.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/ahsante-sana-kwa-jwtz#sthash.d3als4eU.dpuf

No comments:

 
 
Blogger Templates