MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alisababisha kicheko kwa Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine wa vyama vya upinzani baada ya kulalamika hadharani kuhusu hatua ya Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, kutaka kuwania ubunge katika Jimbo la Vunjo, Raia Mwema limeambiwa.
Hiyo ni mojawapo ya taarifa kutoka ndani ya kikao baina ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya upinzani nchini kilichofanyika Jumapili iliyopita katika Ikulu ndogo ya Chamwino mjini Dodoma.
Wakati mkutano huo ukiendelea, Mrema, mwanasiasa aliyewahi kushika wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu katika Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema wakati viongozi hao wamekuwa ni wamoja kwenye kudai haki zao, wengine wamekuwa wakiwatilia wenzao fitina.
“Mimi nasikia kuna watu wameamua kunifuata kule Vunjo kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao. Mimi nasema hashindwi mtu hapa. Uchaguzi bado haujafika sasa watu mnanifuatafuata nini jamani?” alisema Mrema ambaye alikuwa amekaa katika viti vinavyotazamana na Mbatia aliyeangua kicheko pia.
Suala hilo la Mrema lilichomekwa tu kwenye mazungumzo hayo kwani ajenda rasmi zilikuwa mbili ambazo ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao na mchakato wa kutafuta Katiba mpya.
Viongozi waliohudhuria mkutano huo ambao wamezungumza na gazeti hili wameeleza kwamba kwa ujumla kikao kilikwenda vizuri na kwa muda mrefu Kikwete alikuwa msikilizaji zaidi na alikuja kuongea mwishoni.
Gazeti hili limearifiwa kwamba katika mkutano huo, Kikwete aliwaambia viongozi wenzake kwamba hana mpango wa kuendelea kubaki madarakani baada ya kumaliza kipindi chake cha kikatiba, na kwamba angependa aondoke akicha Katiba mpya.
“Hofu kubwa ya Rais Kikwete ilikuwa kwamba, je, kama yeye akiondoka madarakani tuna uhakika kuwa rais mpya naye atataka kuendelea na mchakato huo? Kwake anaona ni rahisi kumaliza hili endapo yeye atakuwa madarakani.
“Tumekubaliana kwenye kikao kwamba endapo mchakato huu utasitishwa kwa sababu yoyote ile, ni lazima iwekwe kwenye sheria kwamba Rais ajaye ni lazima aendeleze mchakato huu,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Imefahamika kwamba katika mkutano huo wa wiki iliyopita, wapinzani walikuwa na madai makubwa manne ambayo ni kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, Matokeo ya Urais kupingwa Mahakamani, mshindi wa Urais kupatikana kwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi.
Katika msingi huo, viongozi wa upinzani walimweleza Kikwete kwamba wanadhani ni busara kwa Katiba ya sasa kuingizwa mambo hayo kwa ajili ya kufanya uchaguzi ujao uwe salama na kisha mabadiliko ya Katiba yaje baadaye.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo na Mrema waliunga mkono kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) kinyume cha msimamo wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment