Social Icons

Friday, 5 September 2014

Mawaziri wazua balaa Mbeya, kisa 2015


KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 minyukano ilitawala katika siasa za Jimbo la Kyela, sasa ni zamu ya Jimbo la Ileje ambako minyukano imeanza huku manaibu waziri wawili wakitajwa.

Katikati ya mgogoro huo wapo viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ileje na Mkoa wa Mbeya, mtihani sasa upo CCM Taifa kutengua mtego huo, vinginevyo unaelekea kukidhalilisha chama hicho kwa mara nyingine Mkoani hapa.

Mawaziri wanaotajwa katika mgogoro huo ni Naibu Waziri wa Viwanda, Janet Mbene na Naibu Waziri wa Kilimo, Godfrey Zambi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.

Zambi anaingia kwenye mgogoro huo kutokana na nafasi yake kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa, ambaye anadaiwa alisimamia maamuzi ya kuisimamisha Kamati ya Siasa ya chama hicho Wilaya ya Ileje kwa madai ya kukidhalilisha chama wilayani humo.

Waziri Mbene ameingizwa kwenye mgogoro huo baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa kumtaka ajieleze uhusika wake kwenye mgogoro huo, pamoja na ukweli kwamba yeye si mjumbe wa Kamati hiyo ya Siasa Wilaya ya Ileje, iliyosimamishwa.

Hatua ya Kamati ya Siasa ya Mkoa inayomtaka Naibu Waziri huyo kujieleza, imeibua mjadala zaidi, huku wengi wakiamini kuwa ni njama za kumbana mama huyo asiweze kuwania jimbo kati ya Ileje na Mbeya Mjini ambako imevuma kuwa huenda akagombea.

Katika mahojiano yake na Raia Mwema, kuhusu madai ya yeye kuwania Jimbo la Ileje, Mbene anasema:

“Kosa langu kuwa mtoto wa Ileje, mimi kule ni nyumbani, wazazi wangu wanapohitaji nisaidie, ninasaidia, mimi ni mtoto wao, wanayo haki kuwatumia watoto wao, haya mambo ya ubunge nayasikia yanazungumzwa tu, wao ndio wanayajua, nachojua mimi nasaidia wazazi wangu, ndugu zangu.”

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, Kamati ya Siasa ya Mkoa huo, ikiwa imekasimiwa madaraka na Halmashauri ya Mkoa, CCM, imeisimamisha Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ileje kwa kosa la kufunga ofisi ya chama ya Wilaya hiyo kwa siku kumi.

“Ni uhaini kuzuia shughuli za chama, wamekifanya chama kunuka mbele ya jamii,” alisema Madodi katika mahojiano maalumu na Raia Mwema.

Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi huyo, kanuni za chama hicho zinaipa mamlaka Halmashauri ya Mkoa kusimamisha au kuwaondoa hadi wajumbe 12 wa Kamati ya Siasa ya Wilaya.

Taarifa kutoka wilayani Ileje zinabainisha chanzo kuwa ni mgogoro uliopo kati ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo na Katibu wake wa Wilaya, Lucian Mbosa, baada ya shauri hilo kupelekwa mkoani ndipo maamuzi ya kuisimamisha Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo yalipotolewa.

Pamoja na maamuzi hayo, Kamati hiyo ya Siasa ya Mkoa ilimtaka Naibu Waziri Janet Mbene kujieleza kuhusiana na uhusika wake kwenye mgogoro huo huku ikiwapa onyo baadhi ya viongozi wilayani humo akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mohamed Mwala.

Kutajwa kwa Waziri Mbene ndiko kumechochea zaidi mgogoro huo, wengi wilayani humo wakiamini amehusishwa kutokana na hofu ya baadhi ya wanasiasa kwamba anahitaji kugombea ubunge kupitia jimbo hilo.

Tayari kundi moja lenye kuusaka urais kwa udi na uvumba linatajwa kuingilia siasa za Ileje kutokana na ushiriki wa kiongozi mmoja wilayani humo ndani ya kundi hilo.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu mgogoro huo walibainisha kuwa, kumhusisha Mbene na siasa za Ileje kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani ni kumuonea, kutokana na ukweli kwamba naye ni mtoto wa wilaya hiyo hivyo ana haki ya kufika kwao na kusaidia ndugu zake pale anapohitajika.

“Waziri anatakiwa kujieleza kitu gani, kwani ni mjumbe wa kamati ya siasa, huyu Zambi kakurupuka, anapaswa kuelewa kuwa anayembeba habebeki,” anabainisha mtumishi mmoja wilayani Ileje, jina linahifadhiwa.

Kauli ya mtumishi huyo inaoana na msimamo wa baadhi ya wanasiasa waandamizi wa siasa za mkoa huo, ambao katika mahojiano yao na Raia Mwema wamemshutumu Mwenyekiti wao wa Mkoa kuwa amekurupuka kumtaja waziri mwenzie kwenye mgogoro huo, kwani hatoweza kulithibitisha hilo.

Naibu Waziri Mbene hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa linashughulikiwa na mamlaka za chama, ngazi ya Taifa, na kwamba amepewa maelekezo kumwandikia Mwenyekiti CCM, Mkoa wa Mbeya ampatie maelezo pamoja na uthibitisho wa madai yao.

“Nasubiri ngazi za juu kulitolea maamuzi, si busara mimi kujibizana kwenye vyombo vya habari, tusubiri uamuzi wa chama,” alisema Mbene.

Hata hivyo alibainisha kuwa suala la yeye kwenda Ileje sio mjadala, ni kwao hivyo huwa anaenda na kwamba alipoteuliwa kwenye nafasi ya Naibu Waziri iliwafurahisha wananchi wa Ileje.

“Wananitumia kama mtoto wao, nami wanaponishirikisha kwenye shughuli zao hushiriki, tatizo liko wapi,” anahoji Mbene.

Ushiriki wa Waziri Mbene katika shughuli za maendeleo nyumbani kwao Ileje, ndio uliozusha hisia za yeye kulihitaji jimbo hilo, japo mwenyewe hajawahi kutamka, lakini kwa wananchi wa wilaya hiyo jina lake lipo kwenye vinywa vyao.

Wajuzi wa siasa za Mkoa wa Mbeya wanaitaja sababu kuu ya mama huyo kuhusishwa na siasa za Ileje kuwa ni ombwe la uongozi kwenye jimbo hilo, kwamba Mbunge aliyepo ni baridi mno, hivyo kuwalazimisha wananchi, wakiwemo viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kumkimbilia waziri huyo wakiamini kuwa ni mtoto wao, naye huitikia wito wao, hatua inayowafanya wamtegemee zaidi yeye kuliko mbunge wao.

Juhudi za kumpata Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mbeya, Zambi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ileje zilikwama kutokana na simu za viongozi hao kutopatikana kwa siku mbili.

Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Mohamed Mwala ameushangaa uamuzi wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mbeya kuwaadhibu kibabe bila kuzingatia kanuni na mamlaka ya wananchi wa Ileje.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Siasa, CCM, Mkoa wa Mbeya Mwenyekiti huyo anatakiwa kutofika kwenye ofisi za chama hicho wilayani humo, kutopatikana na kosa lolote wala kugombea nafasi yoyote ndani ya miezi 12 kuanzia tarehe ya kutolewa adhabu hiyo.

Lakini kinachoaminika kwa wengi, Mwenyekiti huyo anaadhibiwa kutokana na imani iliyojengeka kuwa yuko upande wa Naibu Waziri Mbene, madai yanayokanushwa na wadau wa maendeleo wa wilaya hiyo wakisema, anahusishwa kwa sababu ya ushiriki wa waziri kwenye shughuli za maendeleo ya wilaya hiyo, ambazo kimsingi husimamiwa na Halmashauri ya Wilaya.

“Kitaalamu hapa waweza kuona kuwa sisi hatutagombea uongozi katika uchaguzi wa mwakani kwa sababu hatua za msingi zitakuwa zimefanyika tukitumikia adhabu,” anasema Mwala.

Adhabu hiyo dhidi ya Mwenyekiti huyo na wenzake imezidisha hofu miongoni mwa wananchi wa Ileje, wakiamini kuwa kuna njama zinazoratibiwa kutoka nje ya wilaya hiyo kuwapangia safu ya viongozi.

“Mimi ni raia namba moja katika wilaya hii, nilichaguliwa na wananchi na madiwani, unanizuia kuwatumikia watu wangu, umewashirikisha wananchi, hivi wanaijua athari yake,” anasema Mwenyekiti huyo wa Halmashauri akiushangaa uamuzi huo wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mbeya.

Athari inayotahadharishwa na Mwenyekiti huyo ni hisia za wananchi wa wilaya hiyo kutokana na mtazamo walionao sasa kwamba wanadharauliwa na hatua hiyo ni moja ya dharau za viongozi wa chama hicho kwa wananchi hao, kwamba wao hawawezi kuamua jambo wanalolihitaji, bali ni watu wa kuamuliwa na wakubwa kutoka nje ya wilaya yao.

“Ni kutafutiana nafasi, sawa wao wapange, lakini sisi tuna watu,” anatahadharisha Mwala.

Wapo wanaokwenda mbali zaidi katika suala hili, wakibainisha kuwa uamuzi huo umechukuliwa katika mtazamo ule ule wa kuwaona wananchi wa wilaya hiyo kutokuwa na uwezo wa kusimamia mambo yao, kisa ikiwa ni upole wao, lakini katika hili wanasema watakapochachamaa patatikisika.

Ujio wa Janet Mbene katika siasa za Mkoa wa Mbeya unawatisha wengi, wapo wenye kuzusha kuwa anatarajiwa kuwania Jimbo la Mbeya Mjini, na kutokana na uvumi huo baadhi ya wanasiasa mkoani hapa wanatajwa kutumia mgogoro wa Ileje kumbana.

“Watu hawajazoea wanawake majasiri, huyu mama kawatikisa, ni mwanamke mwenye uwezo na msaada mkubwa kwa Mbeya, ninachofahamu mimi anawatumikia kama mtoto wao, mwenyewe husema ni namna ya kuwashukuru wazazi wake waliomleta duniani,” anasema mwanasiasa mmoja mwandamizi mkoani humo.

Mgogoro wa Ileje unatarajiwa kupanuka na kuimega CCM Mkoa wa Mbeya vipande vipande, iwapo tu chama hicho ngazi ya Taifa hakitatumia busara kuutatua, wafuatiliaji wa siasa za mkoa huu wanahofia mitandao ya wasaka urais kuuvuruga tena mkoa huo kutokana na mawakala wake kuandaa safu za viongozi wanaowataka, jambo ambalo tayari limebainika.

Chanzo: Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates