TAARIFA kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ana mpango wa kuwania Urais zimezua mambo baada ya shaka kujitokeza kuhusu namna habari hizo zilivyovuja kwenye vyombo vya habari.
Shaka hiyo imekuja wakati wapambe wa watu wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakija juu na kudai kwamba kama kweli Pinda anataka kuwania nafasi hiyo, basi wanachama waliosimamishwa na Kamati Kuu ya chama kwa madai ya kufanya kampeni mapema, walionewa.
Habari za Pinda kutaka kuwania urais ziliibuka Jumapili ya Agosti 24 katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini, vikitokana na safari na mikutano aliyofanya Waziri Mkuu mkoani Mwanza.
Pinda alidaiwa kukutana na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa, ambapo ndipo alipotangaza nia yake hiyo.
Hata hivyo, tangu kutoka kwa taarifa hizo, si Pinda mwenyewe wala ofisi yake iliyotoa taarifa ya kukana wala kukubali kuhusu hilo, lakini Raia Mwema limepata maelezo kuhusu uamuzi huo kutoka katika duru za ofisi yake.
“Pinda ameamua kukaa kimya kwenye suala hilo makusudi tu kwa vile anajua lengo la wanaozusha habari hizo. Kuna namna yake binafsi ambayo anashughulikia suala hilo na umma utajua tu.
“La kwanza linalotia wasiwasi ni kuwa taarifa zile za Pinda zilitoka katika vyombo vya habari kwa wakati mmoja na siku moja. Haiwezekani magazeti matano ya siku moja yakapata stori ya ndani kwa wakati mmoja na tena vilevile kama ilivyoibuka hii.
“Pili, kuna baadhi ya stori za kwenye magaeti zimefanana hadi katika mtindo wa uandishi na upotoshaji. Kwa mfano, chombo zaidi ya kimoja kimeripoti kwamba Pinda alianza kufanya kazi Ikulu mwaka 1974 ilhali wakati huo alikuwa nje ya Dar. Hakunzia kazi hapo.
“Tatu, hakukuwa na juhudi za kumpata Pinda mwenyewe au wasaidizi wake kuthibitisha wala kukanusha kuhusu hili. Inakuaje suala hili linaendelezwa tu bila uhakika wa aina yoyote, alisema mmoja wa maofisa wa ngazi za juu katika Ofisi ya Waziri Mkuu aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa vile si msemaji rasmi wa ofisi hiyo.
Ofisa huyo alisema wanafahamu taarifa hizo zimezushwa kutoka wapi lakini kwa sasa hakuwa tayari kuweka wazi jina la mtu aliyehusika na tukio hilo zaidi ya kusema ni “mtu maarufu.”
Katika hatua nyingine, vyanzo vya gazeti hili vimeeleza pia kushangazwa kwao na namna taarifa hizo za Pinda kutaka kuwania Urais zilivyoeleza kumsifia kwa kuwa mwadilifu na kachero wa muda mrefu, huku zikimhusisha na vitendo vya kutoa rushwa.
“Kama kweli huyu Pinda ni kachero mwandamizi na mahiri, inakuaje akutane na kundi kubwa la watu na aanze kufanya vitendo vya rushwa? Hivi kweli hii inaingia akilini?” kilihoji chanzo kingine cha gazeti hili.
Katika taarifa mbalimbali zilizotoka Agosti 24 mwaka huu, kuna mambo makubwa manne ambayo yalifanana katika baadhi ya taarifa hizo.
Masuala hayo yalihusu kukutana na wajumbe wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, kuifahamu Ikulu fika kwa vile amekaa muda mrefu, kufanya kazi vizuri akiwa chini ya Uwaziri Mkuu wa Edward Lowassa kuliko ilivyo sasa na mapungufu yake kama kiongozi.
Tayari, baadhi ya watu wanaotajwa kutaka kuwania urais wameonyesha kutofurahishwa kwao na uamuzi wa Pinda kutaka kuwania urais.
Katika mahojiano na mojawapo ya magazeti makubwa hapa nchini wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alieleza kutoridhishwa kwake na baadhi ya mambo katika mfumo wa uongozi wa chama chake.
Akitoa mifano pasipo kutaja jina, Membe alisema baadhi ya viongozi walioshiriki katika vikao vilivyowapa adhabu baadhi ya wanachama wanaotajwa kuwania urais, nao wameanza kujitokeza wakitaka kuwania nafasi hizo hizo.
Pinda ni Mjumbe wa Kamati ya Kuu ya CCM na pia Kamati ya Maadili ya chama hicho, kamati zilizoshiriki katika kufikia maamuzi ya kumsimamisha Membe na wanachama wenzake wa CCM kutofanya shughuli za kisiasa kwa muda wa mwaka mmoja.
Wana CCM wengine waliosimamishwa ni Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Steven Wassira, William Ngeleja na January Makamba.
Baadhi ya wapambe wa wanachama hao, wamezungumza na gazeti hili na kudai kwamba kilichofanywa na Pinda ni sawa na kuwafunga spidi gavana wapinzani.
Hapa naona sasa inatakiwa CCM iamue tu kuwafungulia wanachama waliosimamishwa kufanya shughuli hizo za kisiasa. Hakuna sababu za kuwasimamisha wengine na halafu waliofanya uamuzi huo nao wakaanza kufanya yaleyale waliyokataza wenzao.
Hii ni sawa na kuamua kushiriki katika mashindano ya mbio za magari na halafu ukaamua kuwafunga wenzako spidi gavana halafu na wewe ukaingia kwenye mbio hizo ukiwa kamili. Hii si sawa kabisa, alisema mpambe mmoja maarufu wa mmoja wa wanasiasa wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais.
No comments:
Post a Comment