MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, ameeleza namna Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyomshauri asiwanie urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na badala yake akawanie ubunge wa Moshi Vijijini.
Katika mazungumzo yake na Raia Mwema wiki hii, Mrema alisema kimsingi Mwalimu alimuahidi kwamba kama angewania ubunge, alikuwa tayari kwenda kumpigia kampeni ili ashinde nafasi hiyo.
“Nilikutana na Mwalimu kijijini kwake Butiama mwaka 1995. Aliniambia ‘Mrema, kwa nini unataka kuwania urais? Utaundaje Baraza la Mawaziri? Achana na urais. Wania ubunge na mimi nitakuja kukufanyia kampeni ili ushinde’. Hata hivyo sikufuata ushauri wake.
“Nisingewania urais ningewakatisha tamaa mamilioni ya Watanzania waliokuwa wanataka Mrema awe Rais wa Tanzania. Kulikuwa na kauli mbiu maarufu wakati ule iliyokuwa ikisema Piga, ‘Ua Mrema Rais’.
“Sasa ningewezaje kuwaangusha Watanzania wenzangu kwa sababu ya kushawishiwa na Mwalimu? Nilimsikiliza lakini nikamwambia Mwalimu nakuheshimu lakini kwenye hili itabidi niwasikilize Watanzania. Wao ndiyo wanaomtaka Mrema wao,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Vunjo.
Alisema mkutano baina yake na Mwalimu ulifanikishwa na Charles Makongoro Nyerere, mtoto wa Nyerere ambaye wakati huo tayari alikuwa amejiunga na chama alichohamia Mrema cha NCCR-Mageuzi.
Katika mazungumzo yake hayo na gazeti hili, Mrema alieleza kwa kirefu kuhusu namna alivyohama kutoka katika chama hicho na kujiunga NCCR, ingawa baadaye aliondoka na kujiunga na chama alichopo sasa cha Tanzania Labour (TLP).
Mrema alisema sikitiko pekee alilonalo katika maisha yake ya kisiasa ni namna alivyoondoka ndani ya CCM bila ya kuondoka na vigogo wengine japo watano, jambo alilosema lilimfanya aukose urais.
“Sikufanya hesabu zangu sawa sawa wakati nikitoka CCM na kwenda NCCR. Ningejitahidi walau kuondoka na vigogo walau watano hivi kutoka katika chama hicho. Labda na viongozi wa chama wa mikoa na hata mabalozi.
“Sasa mimi niliondoka mwenyewe. Peke yangu. Nilipoona umati wa watu unajaa katika mikutano yangu ya hadhara na wanawake wanatandika khanga kila ninapopita, nikajua nimemaliza kazi.
“Hebu fikiria, mimi peke yangu nilipata kura milioni 1.8 mwaka 1995. Levy Mwanawasa, alipata kura kama hizo kwenye uchaguzi wao nchini Zambia na akapata urais.
“Hivi ningeondoka na watu pale CCM unadhani ningepata kura ngapi? CCM kweli wangeweza muziki wangu? Kwenye siasa zangu, kwa kweli hapo ndiyo mahali pekee nadhani nilifanya makosa.
“Inawezekana wananchi walikuwa wanajiuliza, sawa, Mrema anafaa kuwa Rais lakini je, Waziri Mkuu wake atakuwa nani? Mambo ya Nje? Mambo ya Ndani? Sikuwa na watu wanaofahamika kama viongozi. Kama ningelifanya hilo, pengine ningeweza kuingia Ikulu,” anasema Mrema.
Kuhusu aina ya viongozi wa vyama vya upinzani waliopo sasa ukilinganisha naye, Mrema alisema tatizo lililopo sasa ni kuwa wengi wao hawana uzoefu wowote wa uongozi zaidi ya ule wa kwenye vyama vyao.
“Vyama vingi vya upinzani hapa nchini vina watu ambao hawajulikani uwezo wao. Sasa mtu hajawahi kuwa hata katibu tarafa au mkuu wa wilaya tu angalau halafu anakuja kwa Watanzania na kutaka urais. Sasa huyo mtu atapigiwaje kura? Atashindaje? Atapendwaje kama Mrema?
“Mimi na Maalim Seif tuna nguvu kwa sababu wananchi wetu walituona wakati tulipokuwa madarakani. Wanajua wakituchagua watapata nini. Wapinzani wengine ni majina tu.
Chanzo Raia Mwema

No comments:
Post a Comment