HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, hivi sasa, ipo kwenye mgogoro wa uongozi, chanzo kikielezwa kuwa ni kuingiliwa na uongozi wa mkoa huo.
Madai hayo yanatolewa na baadhi ya viongozi na watendaji wa jiji hilo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo wanaelezea pia kutokubaliana kwao na utaratibu huo.
Mifano inayotolewa na wale wenye kuamini kuwa uongozi wa Mkoa huo wa Mbeya unaingilia utendaji wa kila siku wa jiji hilo, ni pamoja na uamuzi kuhusu Soko la Mwanjelwa ikiwemo uendeshaji wake.
Juma lililopita, wakazi wa jiji hilo wameshuhudia wafanyabiashara wadogo wakijenga vibanda vya mabanzi ndani ya wigo wa soko hilo,hatua inayoelezwa na baadhi ya watendaji na madiwani kuwa inashusha hadhi soko hilo. Inaelezwa kuwa mpango wa awali wa jiji hilo ilikuwa kujenga vibanda vyenye hadhi na kuwakabidhi wafanyabiashara na sio kuwaachia wajenge wapendavyo.
Mambo mengine yanayoelezwa kusimamiwa na uongozi wa mkoa huo ni suala la wafanyabiashara wadogo, maarufu kwa machinga pamoja na waendesha pikipiki ya gurudumu tatu maarufu kwa bajaji.
Chadema wahoji
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Boyd Mwabulanga amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kubainisha kuwa wao kama chama kinachoendesha halmashauri ya jiji hilo hawakubaliani na mwenendo huo.
Jiji la Mbeya linahesabika kuwa moja ya ngome muhimu za Chadema hapa nchini ambapo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana walifanikiwa kushinda nafasi ya ubunge na kuongoza katika nafasi za urais na udiwani kwa kuzoa kata nyingi zaidi hivyo kuongoza Baraza la Madiwani la jiji hilo.
Katika Baraza la Madiwani la jiji hilo, Chadema kinaongoza kikiwa na madiwani 36 dhidi ya 13 wa CCM.
Naibu Meya Jiji la Mbeya, Mchungaji David Ngogo alikiri kuwepo kwa hisia miongoni mwa viongozi, madiwani na wanachama wa Chadema kuhusu uongozi wa mkoa kuingilia uendeshaji wa jiji hilo, zilizojengeka kutokana na matukio hayo ya hivi karibu.
Anasema, maamuzi ya masuala ya soko, machinga na bajaji yanatakiwa kufanywa na mamlaka ya jiji hilo, lakini hatua ya viongozi wa mkoa kusimamia hadi ugawaji maeneo ya biashara kwenye Sokola Mwanjelwa ni kuipora mamlaka ya jiji mamlaka yake.
Hata hivyo, yamekuwepo pia madai ya usaliti miongoni mwa baadhi ya madiwani wa Chadema, wakielezwa kufanya kazi kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kinyume cha msimamo wa chama chao.
Pamoja na usaliti wa baadhi ya madiwani wa chama hicho, naye Meya wa Jiji hilo, David Mwashilindi anashutumiwa na baadhi ya madiwani kwamba ni dhaifu na mwenye kukubali kuingiliwa kirahisi.
Mkurugenzi wa jiji hilo, Nachoa Zakaria alipinga madai hayo ya uongozi wa mkoa kuingilia utendaji wa jiji hilo akisema haoni tatizo kwa sababu serikali kuu ndio wasimamizi wa serikali na pale wanapoona mambo hayaendi ni jukumu lao kuingilia.
“DC na RC ndio wasimamizi wa shughuli zote za serikali, pale wanapoona mambo hayaendi, wanaingilia,” alisema Mkurugenzi huyo katika mahojiano maalumu na Raia Mwema ofisini kwake.
RC Makala anena
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala amekanusha kuingilia utendaji wa Halmashauri ya Jiji hilo na kwamba iwapo yupo mtu yeyote mwenye madai hayo basi atakuwa haelewi kazi za mkuu wa mkoa.
“Kama kuna anayedai hivyo haelewi kazi za Mkuu wa Mkoa kuwa ni kiongozi wa shughuli zote za serikali katika mkoa,” alisema Makala akitoa ufafanuzi kuhusu madai kwamba anaingilia utendaji wa jiji hilo.
Katika maelezo yake kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, Makala anakiri kuingilia kati baadhi ya migogoro ambayo imelikumba jiji hilo lakini wakashindwa kuishughulikia hivyo kumlazimu yeye kuitatua.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, shughuli anazodaiwa kuingilia ni pamoja na Soko la Mwanjelwa ambalo anasema jiji walikaa kimya wakati ufisadi mkubwa wa ujenzi na upangishaji ukifanyika.
“Walikaa kimya, lakini mimi nimeingia mkoa wa Mbeya nimeushughulikia,” anasema Makala.
Katika orodha hiyo anaitaja pia mivutano ya machinga na jiji, ambapo anasema wanazagaa na kukosa msaada na maeneo ya kufanyia kazi. Mkuu huyo wa mkoa anaushutumu uongozi wa jiji hilo kwa kutoumaliza na kusababisha mgogoro kukua hadi alipoingilia kati, ambapo anasema amewasaidia na kumaliza mvutano.
Miongoni mwa usumbufu unaolikabli jiji hilo ni pamoja na kuzagaa kwa malori na bajaji huku magari ya taka nayo yakifanya kazi hiyo pasipo kuzingatia masharti ya usafi hivyo kusababisha kutapakaa kwa uchafu maeneo mbali mbali ya jiji hilo na barabarani.
Pamoja na matatizo hayo, Makala anasema uongozi wa jiji ulikaa kimya hivyo kumlazimu kuingilia kati. Uamuzi mwingine wa mkuu huyo wa mkoa unaoelezwa kuingilia utendaji wa mamlaka hiyo ni hatua ya Makala kuwazuia madiwani wa jiji hilo kuchukua posho kwenye michezo ya timu ya jiji hilo, Mbeya City, akisema ni matumizi mabaya.
Alipokuwa katika ziara yake mkoani Mbeya, mapema Agosti, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimwagiza mkuu wa mkoa huo kushughulikia madai ya kuwepo kwa ufisadi katika mradi wa Soko la Mwanjelwa.
Waziri Mkuu pia alimpa mkuu huyo wa mkoa siku tatu kufuatilia shilingi milioni 489, zikiwa sehemu ya mkopo kwa ajili ya ujenzi wa soko ambazo zinadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, siku saba kuwaondoa wafanya biashara na kuwaingiza machinga kwenye Soko la Mwanjelwa.
Mkuu huyo wa mkoa alipewa pia siku kumi kuwanyang’anya vyumba vya biashara katika soko hilo wasiovitumia.
“Kuthibitiha Waziri Mkuu anayajua majukumu ya mkuu wa mkoa, yote aliniagiza mimi RC, hakumwagiza mkurugenzi wale meya,” anasema Makala.
Hata hivyo, katika suala la shilingi milioni 489, hadi sasa bado kukamilika na ni zaidi ya mwezi sasa tangu agiizo la siku tatu la Waziri Mkuu. Uchunguzi uliofanyika umeonyesha kuwa panahitajika wataalamu wa mifumo toka Benki Kuu kukagua miamala yote ya CRDB inayohusiana na mkopo wa CRDB na taarifa zilizopo zinaeleza kuwa wakati wowote kazi hiyo itaanza.
Chanzo. Raia Mwema

No comments:
Post a Comment