
Waasi wa Libya wakipambana na majeshi ya serikali wakati moshi kutoka kwenye visima vya mafuta vilivyoharibiwa ukitanda angani. Ilikuwa Machi 11, 2011 eneo la Ras Lanuf, Libya.
CNN-London
KUINGIA kwa Uingereza kijeshi nchini Libya kulitokana na taarifa mbaya za kiintelijensia na dhana mbaya. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo ambayo inamlaumu moja kwa moja aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kwa kushindwa kuandaa mkakati unaofaa kuhusu Libya.

Raia wa Libya akichoma moto picha ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Moammar Gadhafi huko Benghazi, Machi 2011.
Uingereza na Ufaransa ziliongoza washirika wa kimataifa kuingilia kati machafuko ya nchini Libya mwaka 2011 kwa nia ya kulinda raia wa nchi hiyo dhidi ya majeshi yaliyokuwa yakimtii Moammar Gadhafi.
Kamati ya Mashauri ya Nje ya Uingereza iligundua kwamba serikali iliyokuwa ikiongozwa na Cameron ilishindwa kugundua kwamba hatari kwa raia wake ilitiwa chumvi na kwamba waasi walihusisha na vikundi vyenye siasa kali za kidini.
Sera ilielekezwa katika kubadili utawala
“Matokeo yamekuwa ni kuanguka kwa mfumo wa kisiasa na kiuchumi, mapigano baina ya vikundi vyenye silaha na mapigano ya kikabila, majanga ya kibinadamu na tatizo la uhamiaji, kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kukua kwa kundi la kigaidi la ISIL huko kaskazini mwa Afrika,” ripoti hiyo ilisema, ikitumia jina jingine la ISIS, ambalo linashikilia baadhi ya sehemu za Libya.

Moammar Gadhafi akiwa Dakar, Senegal mwaka 1985.
“Ripoti hii imebaini kwamba sera ya Uingereza huko Libya kabla na baada ya kuingia kijeshi mwezi Machi 2011 ilitegemea dhana potofu, bila kuifahamu nchi hiyo vizuri kwa kuzingatia hali halisi kwa kipindi hicho,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Mbunge Crispin Blunt, katika taarifa yao.
Akaongeza; “Vitendo vya Uingereza huko Libya vilikuwa ni sehemu ya mpango mbovu wa kuingia Libya, matokea yake yanaonekana hadi leo. Njia nyingine za kisiasa zilikuwepo na zingekuwa na gharama ndogo kwa Libya na Uingereza. Kutoeleweka kwa uwezo wa kitaasisi wa nchi hiyo kulipunguza uwezo wa Libya kuimarisha usalama nchini humu.”
Kamati hiyo imesema kuwa ilizungumza na watu wote muhimu katika uamuzi wa kuingilia kati mgogoro wa Libya isipokuwa Cameron ambaye alikataa kushiriki katika uchunguzi huo akisingizia “kuwa na ratiba ngumu,” akiongeza kuwa maafisa wengine wa serikali walitoa taarifa zilizokuwa zinahitajika.
Dunia imeipa kisogo Libya
Ripoti inasema kwamba Cameron alikuwa anahusika moja kwa moja kwa kushindwa kutengeneza mkakati thabiti wa Libya pamoja na ukweli kwamba alianzisha Baraza la Usalama la Taifa.
Ripoti inasema kwamba wakati Cameron alipoomba na kupewa ruksa ya bunge kuwa aingilie kati kijeshi mgogoro wa Libya aliwahikikishia kuwa kuingilia huko hakukulenga kubadili utawala.
“Mwezi Aprili 2011, hata hivyo, alisema alisaini barua ya pamoja na Rais wa Marekani Barack Obama na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy wakiwa na nia ya pamoja kuhakikisha Libya inabaki bila Gadhafi,” ripoti ilisema.

Majeshi ya serikali yakijiandaa kufanya mashambulizi dhidi ya kundi la ISIS nje ya mji wa Sirte, Libya, Machi 2015.
Uchunguzi huo ulionasa ushahidi kutoka kwa viongozi muhimu – akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Tony Blair, makamanda wa jeshi na wasomi – ulibainisha zaidi kwamba uamuzi wa Uingereza juu ya sera ulifuatia yale yaliyofanywa na Ufaransa ambayo yalisababisha jumuiya ya kimataifa kuunga mkono kuingilia kijeshi Libya, mgogoro ambao Marekani ilihusika kuukuza.
Uingiliaji huo wa kimataifa uliofuatiwa na vuguvugu la Waarabu maarufu kama Arab Spring ulirahisisha kuondolewa kwa Gadhafi ambaye aliuawa pembeni ya barabara na wafuasi wa serikali mpya iliyoingia madarakani.
“Lakini kifo chake kiliruhusu machafuko, yakiwemo mapigano ya kikabila na kulifanya taifa hilo kugawanyika katika tawala za majiji, mengi yakiwa chini ya wanamgambo wanaopingana,” ananukuliwa Mhariri wa Kimataifa wa Kituo cha Televisheni cha CNN, Nic Robertson ambaye anazidi kuweka bayana kwamba; “Lakini hukumu mbaya zaidi ambayo Walibya wanayo kutoka jumuiya ya kimataifa ni kwamba jumuiya hiyo imeigeuka Libya.”
ISIS waalikwa
Machafuko ya kisiasa yalitengeneza uasi ambao makundi ya kigaidi kama ISIS kundi ambalo lilitumia udhaifu wa taasisi za Libya kueneza ushawishi wake katika sehemu nyingine duniani, ikiwamo nchini Syria na Iraq.
Kundi la ISIS limeshikilia mji wa pwani wa Sirte na kuenea kuelekea kusini wakati wakishambuliwa na wanamgambo watiifu kwa serikali ya sasa ya Libya pamoja na Marekani.
Serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa inashindwa kutuliza machafuko na inapata shida kukaa madarakani. Mwaka 2014, wanamgambo wa kiislamu waliilazimisha serikali inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa kukimbia mji mkuu wa Tripoli. Serikali hiyo ipo mashariki mwa nchi.
Nchi hiyo sasa imekuwa kitovu cha wahamiaji wanaotaka kukimbilia Ulaya kutoka nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wamekuwa wakitumia taifa hilo kutoroka kwa kupitia mipaka ambayo iko wazi kufika Bahari ya Mediterranea.
Uzalishaji wa mafuta umeanguka sana tangu taifa hilo kuingiliwa kijeshi huku uchumi ukipata pigo zaidi baada ya bei ya mafuta kuzidi kushuka.
Chanzo. Raia Mwema
No comments:
Post a Comment