Social Icons

Tuesday, 25 April 2017

Korea Kaskazini yatishia kuizamisha meli ya Marekani

Meli ya USS Carl Vinson yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita.

Tokyo (CNN)

KOREA Kaskazini jana Jumapili ilitishia kuizamisha meli ya Marekani ambayo imeanza mazoezi ya pamoja na meli za kivita za Japan katika bahari ya Pasifiki.

Meli ya USS Carl Vinson itaungana na zile za Ashigara na Samidare katika mazoezi ya mbinu katibu na Ufilipono, msemaji wa Jeshi la Wanamaji wa Japan alisema.

Gazeti la serikali la Korea Kaskazini la Rodong Sinmun lilisema katika sehemu ya maoni ya mhariri kwamba nchi hiyo itaonyesha nguvu zake za kijeshi kwa kuizamisha meli hiyo inayoendeshwa na nguvu za kinyuklia kwa shambulizi moja.

Gazeti hilo lilidai kwamba nchi hiyo inazo silaha ambazo “zinaweza kuifikia Marekani na nchi za ukanda wa Asia Pasifiki na ina “silaha kali,” bomu la haidrojeni.

Hata hivyo shirika la utangazaji la CNN halikuweza kuthibitisha madai hayo.

Kutokana na maneno makali kutoka Korea Kaskazini, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kwamba meli zinazoongozwa na Vinson zinapelekwa katika bahari karibu na Peninsula ya Korea.

Mahali ilipo meli ya Vinson imekuwa ni kitu kikubwa katika vyombo vingi vya habari duniani tangu matamshi ya Aprili 12 ya Rais Trump.

Trump alisema kwamba anapeleka msafara wa meli za kivita katika Bahari karibu na Korea ili kukabiliana na tishio linalotoka kwa Korea Kaskazini. Matamshi hayo yalikuja baada ya Pyongyang kutangaza kwamba imefanya majaribio yaliyofanikiwa ya kombora la masafa marefu.

“Tunapeleka msafara wa meli za kivita. Una nguvu sana,” Trump alimwambia mwandishi wa jarida la Fox Business Network Maria Bartiromo. “Tuna manowari nyingi. Zina nguvu sana. Zina nguvu zaidi kuliko meli zinazobeba ndege za kivita. Hilo naweza kukwambia.”

Lakini ilikuja kufahamika baadae kwamba meli hizo hazikuwa zinaelekea katika peninsula ya Korea, bali zinakwenda katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi na jeshi la wanamaji la Australia.

Komandi ya Jeshi la Marekani ya Pasifiki ilisema mapema leo kwamba mazoezi na jeshi la wanamaji la Australia yamekamilika, na kwamba “meli zinazoongozwa na Carl Vinson zinaelekea kaskazini huko Magharibu mwa Pasifiki kama hatua ya tahadhari.”

Msemaji wa wizara ya Ulinzi ya Marekani aliliambia shirika la Utangazaji la CNN kwamba meli hizo zitawasili katika peninsula ya Korea mwisho wa mwezi April.


Mwandishi wa CNN Junko Ogura aliripoti kutoka Tokyo na Susannah Cullinane aliandika kutoka Auckland. Pia waandishi wa CNN Ivan Watson na Zahra Ullah waliripoti kutoka Seoul.

Chanzo Raia Mwema


No comments:

 
 
Blogger Templates