Social Icons

Tuesday, 25 April 2017

Waisrael 6 washitakiwa kwa makosa yanayotokana na chuki, Mpalestina akamatwa kwa kuchoma visu watu

Maafisa wa polisi wa Israeli wakiwa katika eneo lilipotokea shambulizi la visu huko Tel Aviv.

(CNN)

WAISRAELI sita wameshtakiwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi uliochukua takribani miezi sita, na Mpalestina mmoja amekamatwa kutokana na mashambulizi ya visu dhidi ya Waisraeli wanne jana Jumapili mchana, tukio ambalo ni ukumbusho kwamba bado hali si shwari hata pale ambapo kunapoonekana kwamba kuna amani.

Wawili kati ya sita ni wanajeshi

Watu hao sita, wakiwemo wanajeshi wawili na mtoto mmoja, walikamatwa katika mji wa kusini mwa Israel wa Beer Sheva kwa kushukiwa kufanya mashambulizi dhidi ya raia wa Kipalestina wa nchi hiyo ambayo yalianza mwezi Desemba mwaka jana, msemaji wa jeshi la polisi la Israel Micky Rosenfeld alisema.

Wakati wa uchunguzi, polisi walisema waligundua visu, marungu, vyuma ambavyo vilitumika wakati wa mashambulizi ambayo yanachochewa na chuki ya kibaguzi ambayo inalenga kuzuia jitihada za kuwajumuisha pamoja Wayahudi na Waarabu huko Beer Sheva.

Mashtaka dhidi ya kundi hilo yatajumuisha yale yanayohusiana na ugaidi, polisi walisema.

Kulingana na waraka wa mashtaka, mmoja wa waliokamatwa, Raz Ben-Shalom, alitaka kuwadhuru Wapalestina ambao walikuwa wakionekana na wanawake wa Kiyahudi.

Lengo lake, mashtaka hayo yalisema, lilikuwa kujenga hali ya wasiwasi na hofu, na kuzuia mahusiano baina ya wanaume wa Kiarabu na wanawake wa Kiyahudi.

Katika tukio moja mwezi Februari, kulingana na mashtaka hayo, Amitzur alilikaribia gari moja huko Beer Sheva na kugundua kwamba mtu katika gari hilo alikuwa ni Mwarabu na mwanamke alikuwa ni Myahudi. Alitoa kisu na kumchoma mwanaume.

Katika tukio lingine mwezi Machi, mashtaka yanasema, alimwona mwanaume wa Kiarabu na wanawake wawili wa Kiyahudi wakiwa kwenye gari na, alichukua nyundo, akavunja dirisha la gari na kumpiga Mwarabu kichwani.

“Unadhani wewe ni mfalme,” mtuhumiwa alisema, kulingana na mashtaka hayo. “Unatoka na wasichana wa Kiyahudi, wewe Mwarabu mchafu.”

Watatu wachomwa kisu Tel Aviv

Huko Tel Aviv, mwanaume wa Kipalestina aliwachoma kisu Waisraeli watatu siku ya Jumapili mchana, alisema Rosenfeld.

Matukio hayo yalitokea katika mtaa wa HaYarkon, ambao upo katika eneo lenye shughuli nyingi katika jiji hilo.

Picha za video zinaonyesha matukio hayo yakifanyaka ndani ya hoteli moja katika mtaa huo.

Rosenfeld alisema kwamba wahanga walipata majeraha madogo.

Mtuhumiwa, kijana mwenye umri wa miaka 18 kutoka eneo la Nablus katika Ukanda wa Magharibu, alikamatwa katika eneo hilo.

Shin Bet, shirika la usalama la Israel, linatazama shambulizi hili kama tukio la kigaidi.

Matukio haya ni ukumbusho wa matukio ya machafuko ambayo yalisambaa nchini humo, Jerusalem, na katika maeneo yanayokaliwa katika Ukanda wa Magharibi mwisho wa mwaka 2015.


Mwandishi wa CNN Joe Sterling aliripoti na kuandika akiwa Atlanta. Waandishi wengine  Andrew Carey na Oren Liebermann waliripoti kutokea Jerusalem.

Chanzo. Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates