NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 5:
Uoga ukazidi kunijaa kwani mkono wake ulikuwa na ubaridi uliopenya mwilini mwangu.
Nilishindwa kugeuza shingo yangu kumtazama kwani nilijua wazi atakuwa ni yule jamaa wa kwenye ndoto zangu, jamani kwenye matatizo acheni kabisa kwani gafla nilitoa mbio hata nadhani ingekuwa ni mashindano basi lazima mimi ningekuwa mshindi.
Mbio nilizokimbia haikuwahi kutokea maishani mwangu, nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa na kujikuta gafla nishafika kituo cha madaladala huku nikihema juu juu.
Ikatokea daladala mbele yangu na kuisimamisha, iliposimama nikapanda na kukaa kwenye siti. Nikajiinamia chini, sikujielewa kabisa na sikuelewa chochote.
Nilipokaribia na kituo cha nyumbani nikatoa nauli na kumwambia konda ashushe, gari iliposimama nikashuka na kuanza kuondoka mara konda wa daladala akanishika bega na kusema,
"Umesahau chenji yako Sabrina"
Nilihisi kupagawa kwani mkono wa yule konda ulikuwa na ubaridi kama wa yule mtu aliyenishika bega njiani, na je yule konda amejuaje jina langu? Nilihisi kuchanganyikiwa, nilipogeuka kumuangalia yule konda nikamuona akitabasamu kama yule mdoli.
Hapo nilihisi kuwa chizi jamani kwani nilianza kukimbia huku nikipiga makelele ya kuomba msaada, nilikimbia na kituo cha kwanza ilikuwa ni nyumbani kwetu. Nilifika mlangoni na kuanguka na kupoteza fahamu kabisa.
Nilipozinduka nilikuwa mikononi mwa mama, kichwa changu kilikuwa kwenye mapaja yake. Kumtazama usoni alikuwa amejawa na machozi huku dada akiwa pembeni na mama Salome.
Niliinuka ili niweze kukaa, mama akanisaidia kufanya hivyo kisha wakanipa maji niweze kunywa.
Baada ya kutulia, mama akaanza kuniuliza.
"Umepatwa na nini mwanangu? Unajua umenitisha!"
"Mmh hata sijui nimepatwa na nini mama ila viungo vyangu vyote vinauma"
Mama akaniambia kuwa ilibidi wamuite mama Salome ili kunipatia huduma ya kwanza kwani yeye alikuwa ni nesi mzoefu. Na ndiye aliyewapa moyo kuwa nitaamka tu.
Siku hiyo nililala chumbani kwa mama kwani mama alitaka kuangalia hali yangu inaendeleaje kwanza.
Kabla ya kulala nilienda kumuuliza dada maswali mawili matatu wakati anatizama video.
"Eti dada kwa mfano ukahisi mpenzi wako amekusaliti, je kuna haja ya kusikiliza maelezo yake?"
"Sikia mdogo wangu, unapomuhisi mpenzi wako vibaya au unapoona kitu kibaya toka kwake hutakiwi kufanya hasira. Unachotakiwa kufanya ni mambo matatu, kwanza kabisa muulize mpenzi wako kuhusiana na kile unachohisi, kusikia au kuona, pili sikiliza maelezo yake hata kama anakudanganya na tatu kaa chini kutafakari na kuyapima maelezo hayo. Usipende kuchukua maamuzi ya gafla kwani yatakuumiza wewe na umpendae"
Ushauri wa dada ukaniingia na kunikaa sawa, kisha nikaenda kulala huko kwa mama kwani mama alikuwa ameshalala muda huo.
Kesho yake nilikuwa na hali ya kawaida kabisa na kuanza kuongea na kucheka na mama.
"Ila wewe mwanangu ni wa ajabu, sijui ulifukuzwa na wezi jana. Yani umekuja na mbio na kuangukia mlangoni, pochi yako ndogo mkononi na simu ndani ya pochi mmh mi nilijua umevitupa"
Kwanza na mimi nilicheka kwani nikikumbuka jinsi nilivyokimbia halafu bila kutupa ile pochi ni kitu cha ajabu sana.
"Mambo mengine ni maajabu tu mama yangu"
"Ila nini kilikukimbiza haswaa?"
"Kuna mtu alinitisha pale stendi, ndiye aliyefanya hadi nianze kukimbia."
"Una vituko wewe, ulinitisha sana ujue"
Niliongea mambo mengi ya hapa na pale na mama.
Mchana wa siku hiyo Sam alifika nyumbani na kumkuta mama, kiukweli mama yangu alikuwa hampendi Sam ila Sam anapofika na kuniulizia mama lazima ataniita ila atanipa muda wa kuzungumza nae.
Mama akanifata ndani,
"Sabrina, kijamaa chako kipo hapo nje kinakuulizia. Sasa sio ndio unachukua muda wote kuzungumza nae, ongea nae kidogo arudi kwao. Sawa?"
"Sawa mama"
Aliposema tu kijamaa nilijua moja kwa moja anamzungumzia Sam.
Nikatamani kukataa kwenda kuzungumza nae kwa yale ya jana ila pia nilitaka kujua anajipya gani la kujitetea kwani nilifata ushauri ambao dada alinipa.
Nikatoa viti viwili na kukaa nje na Sam, na yeye alikuja kutimiza ile azma yake ya jana kuwa angekuja leo nyumbani kwetu na ndio alikuwa amekuja.
Nilikuwa najiandaa kusikiliza maneno ambayo Sam angeongea kujitetea, hata hivyo nilijua lazima atakachoongea kitakuwa cha uongo tu.
"Sam, hivi unajua jinsi gani nakupenda? Na je unajua ni jinsi gani nimeumizwa na huo uchafu wa kwenye simu yako?"
"Naelewa mpenzi ila unatakiwa kunisikiliza kwanza ili nikwambie ilivyokuwa, na unachofikiria juu yangu si kweli"
"Haya, ongea huo ukweli"
"Siku ile uliyowasiliana nami kwa kutumia ile simu ya rafiki yako, badae alinitafuta na kusema kuwa ananisalimia. Nilishamsahau ila alipojitambulisha ndio nikagundua kuwa ni rafiki yako wa mchana.
Kesho yake akanipigia simu asubuhi na kunisalimia, kisha akauliza kuwa nina mipango gani siku hiyo. Nikamwambia kuwa nimepanga kwenda beach na wewe, akaniambia ni vizuri kisha akapongeza kwa hilo.
Badae akaniuliza kama tumeshaenda huko beach, nikamwambia kuwa wewe umekataa ndio akasema kwamba atajaribu kuzungumza na wewe."
"Kwahiyo zile message alikuwa akikufariji kwavile mimi nimekataa?"
"Bado sijamaliza maelezo mpenzi"
"Haya, malizia basi"
"Badae akanipigia simu na kusema kuwa wewe unaonekana kuna kitu umechukizwa na mimi, hivyo akaniambia kuwa anao ujumbe wa kutosha wa mapenzi unaoweza kukufariji wewe, ndio akaanza kunitumia zile message kuwa niziangalie nikiona inayovutia nikutumie wewe. Ila mi sikuwa nachat nae na wala sikumuomba hizo message"
"Kwahiyo ulitaka mimi nifarijike kwa maneno ya mwanamke mwenzangu? Ulishindwa vipi kumzuia asikutumie? Nadhani ulizipenda ndiomana hukuziondoa kwenye simu yako."
"Si kweli Sabrina, yule ni rafiki yako. Mimi siwezi kukusaliti na kuwa na rafiki yako au kuwa na msichana mwingine, wewe ndiye nikupendae"
"Kweli nimeamini kuwa wanaume ni waongo, yani Sam message inasema nimekumiss sana baby na mwishoni anamalizia na busu mmwaaaaaah halafu unataka kuniambia ni mimi tu unipendaye?"
"Nielewe Sabrina nilichokwambia ni ukweli mtupu, au basi niambie cha kufanya ili upate kuniamini tena. Nakupenda Sabrina"
"Ngoja nifikirie kwanza maelezo uliyonipa kama yana ukweli wowote, ila nisingependa kuona ukiwasiliana tena na Lucy. Nadhani tumeelewana"
Sam alionyesha kujutia sana kile kitendo cha mimi kukuta jumbe za Lucy kwenye simu yake ila ndio hivyo maji yakimwagika hayazoleki.
Nikaagana pale na Sam akaondoka zake tena si kwa kawaida yetu ya kusindikizana, nilimwacha aondoke mwenyewe kama alivyokuja.
Mama akanishangaa kuwa mbona sijamsindikiza Sam.
"Kheee malkia leo umemuacha mfalme wako kaondoka mwenyewe!! Kulikoni??"
"Hakuna kitu mama"
"Mmmh hakuna kitu kweli? Ila kama mmeachana basi ashukuriwe Mungu"
Akainua na mikono juu kuonyesha shukrani hadi nikajisikia kucheka.
"Kwanini mama humpendi Sam?"
"Sio type yako, haendani na wewe kabisa. Wewe mwanangu unatakiwa kupata mwanaume wa ukweli, mwenye kazi ya maana na pesa zake halafu msomi ila sio hao vidampa kama huyo Sam"
"Ila mama mapenzi sio pesa"
"Usibishane na watu tuliotangulia kuliona jua, je utapenda kuona watoto wako wakipata shida au raha?"
"Napenda wanangu wafurahi"
"Basi fata ushauri wangu, olewa na mtu anayejielewa utaona faida yake"
Anavyoongea mama kama vile Sam nae hajielewi wakati Sam ni mwanaume anayejielewa na kujitambua pia.
Dada aliporudi, aliniita chumbani kwake na sikujua ameniitia kitu gani.
Kumbe aliniita kuhusiana na vile vitu ambavyo nilirudisha chumbani kwake.
"Mbona umerudisha maua na mdoli ambaye nilikupa? Nilitaka kukuuliza jana sema ndiovile hukuwa na hali nzuri"
"Me sivitaki tu dada ndiomana nimekurudishia"
"Hadi mdoli Sabrina! Inamaana siku hizi hupendi tena wadoli?"
"Mi sijisikii kuwa navyo tu dada"
"Basi hakuna tatizo vitakaa humu chumbani kwangu"
Sikuweza kumwambia dada ukweli kama yule mdoli alikuwa akitabasamu.
Tulipokaa sebleni dada akamwambia mama kuwa aliniletea zawadi ya mdoli na maua ila nimevirudisha nakudai kuwa sivitaki.
"Ukiona hivyo ujue amekua, maswala ya madoli hayo ni mambo ya kitoto tu. Angekuwa kijijini Sabrina usikute angekuwa na watoto hata watatu sasa hivi"
Dada na mama wakawa wanacheka,
"Nimemshangaa sana leo kukataa mdoli kweli amekua mdogo wangu, eti Sabrina au ndio Sam anataka kukuoa?"
"Atakaemuozesha kwa huyo Sam ni nani? Labda nife ndio aolewe nae"
Kwakweli kauli za mama juu ya Sam hazikuwa nzuri kabisa, ila leo hawakuzungumzia zile stori zao za kutisha angalau nyumba ikawa na amani.
Hata mi mwenyewe, Leo nilikuwa na amani na kwenda kulala chumbani kwangu, kwanza kabisa nilizungumza na Sam kwenye simu kisha nikalala kwa amani kabisa.
Nikawaona Sam na Lucy wakiwa kwenye penzi zito huku mimi roho ya wivu ikiniuma, waliendelea na mapenzi yao na mwisho wa siku wakafunga ndoa.
Nilishtuka sana na jasho jingi likanitoka, yani Sam ananiongopea? Kumbe kweli ana mahusiano na rafiki yangu Lucy hadi watafikia hatua ya kuoana, roho iliniuma sana.
Wakati nawaza hayo, usingizi ukanichukua tena.
Yule mkaka mtanashati akanionyesha nyvmba nzuri sana na kusema kuwa itakuwa mali yangu endapo nitakubali kuwa na yeye, akanyoosha mkono wake ili niambatane nae lakini mimi nilikataa, akawa anafanyakazi ya kunisogelea huku akitabasamu na mimi nikazidi kusogea nyuma, nikafika mahali nikawa nimekwama, kuangalia nyuma kulikuwa na shimo refu lenye wadudu wengi na mbele yangu ni yule mkaka aninisogelea, nilipotaka kuanguka kwenye lile shimo nikashtuka na jasho liliendelea kunitoka tena jingi kushinda la mwanzo. Nikajiuliza kuwa hii ndoto inamaana gani nikakosa jibu.
Nikabanwa na haja ndogo na kuinuka pale kitandani ili niende chooni.
Choo chetu kilikuwa ndani, ila nilipokaribia mlango wa choo nilasikia kama mtu anacheka nikajiuliza ni nani usiku ule wakati mama na dada walikuwa wamelala.
Kufika kwenye mlango wa choo nikamkuta yule mdoli akiwa mlangoni na uso wake ulitazama kwangu huku ukitabasamu, nikaanza kuogopa nikatamani kupiga kelele ila nilishindwa nikaamua kukimbilia chumbani huku nahema juu juu kwani ni mambo ya ajabu ambayo sikuyatarajia kabisa. Nikabamiza mlango kwa uoga.
Nikiwa chumbani kwangu nikaanza kujilaumu kuwa kwanini sikwenda chumbani kwa mama moja kwa moja ila niliogopa kutoka tena.
Nikakaa kitandani kwa uoga, gafla nikashikwa na kitu mgongoni ile kugeuka na kuangalia ni yule mdoli wa chumbani kwa dada, alikuwa akitabasamu kama yule mkaka wa ndotoni.
Hali ilikuwa mbaya zaidi pale nilipotazama mezani na kumuona tena yule mdoli na yale maua.
Hofu ikanitanda, uoga ukajaa nikainuka pale kitandani ili nikafungue mlango nikimbilie chumbani kwa mama.
Nilipoufikia mlango, yule mdoli nae alikuwa mlangoni akitabasamu halafu kwa mbali nilisikia mtu akiita jina langu.
Itaendelea kesho.....!!!
Maoni yako ni ya muhimu sana. Asante.
Kama tuko pamoja
![]()
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:
Post a Comment