Social Icons

Saturday, 17 June 2017

HADITHI: Niliolewa na Jini bila ya kujitambua - 6


NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 6:

Yule mdoli nae alikuwa mlangoni akitabasamu halafu kwa mbali nilisikia mtu akiita jina langu.
Nilizidi kuchanganyikiwa, nikaamua kupiga kelele kwa nguvu na kwa bahati muda huo sauti ilitoka.
"Mamaaaaaaaaaaaa..............."


Mama na dada walikuja mbio chumbani kwangu.
Walivyofungua mlango wangu, nilichoropoka na kukimbilia sebleni wakanifata na kuniuliza. Nilikuwa natetemeka sana.


"Kuna nini mwanangu? Kuna nini jamani??"
Mama na dada walikuwa wananishangaa, kwani jasho na machozi vilikuwa vyanitoka.
"Mdoli mama mdoli"
Niliamua kusema kilichonisumbua.
"Mdoli kafanyaje?"
"Ananitisha mama kila mahali namuona halafu anatabasamu"
"Yuko wapi sasa huyo mdoli?"


Nikaamua kuongozana nao chumbani ili nikawaonyeshe.
Kuangalia pale mlangoni hayupo, kitandani hayupo, ndipo nikatazama mezani na kumkuta ametulia kabisa kama mdoli wa kawaida.
Nikawa namuonyesha dada,


"Si umemuona yule mdoli, kafikaje pale wakati alikuwa chumbani kwako?"
Dada yangu akacheka sana hadi mama akamuuliza anachochekea.
"Kweli Sabrina ni muoga jamani loh!!"
"Sema basi unachochekea Penina?"
"Mama, yule mdoli kweli Sabrina alikuja na kumrudisha kwangu kuwa hamtaki. Me nikahisi labda kuna kitu kachukia ndomana kamrudisha yule mdoli. Kwa nimjuavyo Sabrina anapenda sana wadoli, sasa mimi nimemfanyia surplise alipokuwa amelala nikamrudisha yule mdoli na kumuweka pale mezani ili akiamka amkute na kufurahia"


Nilimshangaa sana dada, ataniwekeaje kitu ambacho nilishakikataa!
"Ila mimi simtaki huyo mdoli, jana nilishakukatalia dada."
"Penina mwanangu ulichofanya si kizuri, Sabrina mwenyewe ana maruweruwe siku hizi. Akikataa kitu usimuwekee tena, haya mtoe huyo mdoli wako."


Ikabidi dada amtoe yule mdoli, na mimi nikaendelea kuwaeleza.
"Hata hivyo wakati naenda chooni nilisikia mtu anacheka na mlangoni mwa choo ndio akatokea huyo mdoli akitabasamu"
"Maruweruwe hayo mwanangu"
"Hata hivyo niliyekuwa nacheka ni mimi, nilikuwa naongea na simu si unaju kumekucha tayari! Nilikuwa najiandaa kuoga niende kazini"
Nilishangaa sana kwani muda niliodhania mimi kuwa ni usiku wa manane kumbe ilikuwa ni alfajiri, maneno ya mama kuwa nina maruweruwe nikaona huenda yakawa ni kweli ila bado sikuwa na imani na yule mdoli.


Mchana wake wakati tumekaa na mama ikabidi aniulize,
"Hivi ni kweli ulikuwa unatishwa na yule mdoli mwanangu?"
"Ndio mama, tena amenitisha sana tu"
"Kwahiyo unaamuaje maana dadako hayupo saizi tunauwezo wa kufanya chochote"
"Itakuwa vyema kama tukimchoma moto"
"Basi sawa mwanangu"
Mama akanituma nikamchukue yule mdoli ili tumchome moto lakini nilikataa kumfata, hivyo mama akaenda kumchukua mwenyewe.


Akaniita tumchome moto, akammwagia mafuta ya taa na kumuwasha moto.
Wakati yule mdoli anaungua ikatokea harufu kama vile kuna nyama inachomwa hata mama akashangaa.
"Mbona mdoli mwenyewe ana harufu kama ya kiumbe hai?"
"Ndio uone maajabu hayo mama, mi nikisema mnaona ni maruweruwe"
"Itabidi dadako akija nimuulize alipomtoa huyo mdoli"
Wakati tunajadiliana na yule mdoli akizidi kuungua, ikanyesha mvua iliyotuondoa mahali pale kufika ndani ikakatika.


Tukarudi tena kuangalia mdoli alivyoungua, tukakuta vinaungua vitu kama vya plastiki plastiki hivi. Wala haikuonekana dalili ya mdoli, mama akasema labda mdoli alishaungua wote.
"Na hiyo plastiki inayoungua je?"
"Labda wapita njia wameweka"
Nikacheka kweli kwa makisio ya mama.


Tukarudi ndani na kukaa, mara dada akawa amerudi hata tukamshangaa jinsi alivyowahi kurudi siku hiyo.
Ikabidi mama amuulize kuwa mbona amewahi sana.
"Mbona umewahi kurudi leo?"
"Majanga mama"
Halafu akaenda chumbani kwake kuweka mkoba, kisha akarudi tena sebleni na kuniuliza.
"Kheee Sabrina umemchukua tena yule mdoli?"
Kabla sijamjibu, mama akamuuliza tena.


"Niambie Penina, majanga gani hayo?"
"Mwenzangu, (akanigeukia mimi) unakumbuka kuwa nilikwambia kuna kijana kazini kanipa zawadi ndio nikakuletea wewe yale maua na yule mdoli?"
Nikaitikia kwa kichwa huku nikiwa na hamu ya kujua kuwa huyo kijana kafanya nini, kumbe mama nae alikuwa na shauku ya kujua, akauliza haraka haraka,


"Kafanyaje?"
"Kanifata ofisini kuwa ana shida na mimi, akaniombea ruhusa kwa bosi basi nikaondoka nae. Akaniambia kitu ambacho kimenivutia sana na kufanya nifatane nae, nia yetu ilikuwa ni kuja huku nyumbani kumfata yule mdoli. Tukapanda daladala, sijui hata tumechanganyana nae vipi. Yani mi nikashuka kumbe nimemuacha kwenye gari amesinzia, namuangalia chini hayupo na gari imeondoka. Nikajaribu kupanda gari jingine hadi mwisho, nikakuta lile basi lipo kupakia abiria wengine nilipomuuliza konda akasema kuwa yule kijana alivyoshtuka akashuka njiani hata sielewi amepotelea wapi kijana wa watu jamani mweeeh! Hana namba yangu ya simu na hapa hapajui. Ndio nikaamua kurudi nyumbani tu"


"Sasa yeye alikuwa anataka nini haswaaa"
"Mama, yule mdoli kumbe alikuwa wa bosi wake, yeye hakujua. Sasa amegundua kuwa yule mdoli nyuma kwake kule kwenye zipu kuna..... (kisha akanigeukia na kusema), hebu kamlete yule mdoli Sabrina nije kumuangalia mwenyewe"
Mimi na mama tukabaki tunatazamana kwani mdoli tulishamchoma.
Dada alipoona simjibu kitu, akainuka na kwenda chumbani kwangu akapekua na kurudi.
"Umemuweka wapi yule mdoli Sabrina?"
Ikabidi mama aulize tena,


"Kwani ana nini huyo mdoli Penina?"
"Amewekwa pesa kule kwenye zipu mama, tena ni dola za kimarekani nyingi tu."
"Unasema kweli Penina?"
"Ndio mama, mmemuweka wapi sasa?"
Mama akajibu kwa unyonge,


"Tumemchoma"
Dada akawa kama vile mtu ambaye hajasikia vizuri,
"Mmemfanyaje mama?"
Ikabidi mama amueleze dada kuwa mimi na yeye tulikaa na kutafakari kuwa yule mdoli achomwe moto.


Dada alichukia sana, akaenda pale nje kuangalia kisha akarudi chumbani kwake kwa hasira.

Jioni ya leo nilikaa na mama tu sebleni kwani dada alikuwa na hasira na sisi.
Mama akaanza kuniuliza,
"Hivi na sisi tuliingiwa na nini mwanangu hadi kuchoma mdoli asiyetuhusu?"
"Ila mama, yule mdoli alikuwa ananitisha bhana"
"Tungemchunguza kwanza kabla ya kuamua kumchoma, kwakweli tulichukua maamuzi ya haraka sana"


"Ila ishatokea mama haifai kupeana lawama"
"Tumeteketeza pesa mwanangu mmh!"
Hapo nikajua tu kwa tamaa ya mama yangu lazima ashikwe uchungu juu ya hiyo pesa aliyoisikia.

Usiku sikutaka kulala chumbani kwangu, ikabidi nikalale kwa mama ingawa kulikuwa kwa masharti kwani nikilala nae hataki nishike simu kuipokea wala kujibu ujumbe wa aina yoyote ile, ilibidi nikubaliane na vyote tu.


Sam nae akaanza kunipigia simu, nilitamani kupokea ila nilimuhofia mama kuwa atachukia sana nikipokea simu, tena ukizingatia ni ya Sam kijana ambaye hampendi.
Niliiacha iite hadi kukatika sema ilikuwa ikiita kimya kimya, sikutaka kuizima kwani nilijua kuwa nikiizima nitamchukiza Sam ambaye alipiga na kupiga na kupiga bila kupokelewa.
Nikatamani kurudi chumbani kwangu ili niwe huru ila uoga ulinisumbua, nilikaa na mawazo na kupitiwa na usingizi.


Nilishtuka gafla nikiwa na kiu ile kupitiliza, kwavile mama huweka maji mezani mule chumbani kwake kwaajili ya kunywa akishtuka nami nikainuka na kumimina maji kwenye kikombe ili ninywe.
Wakati na kunywa nikahisi kama kuna mtu ameshikilia ile bilauli na kunisukumia maji yote kinywani hadi nikapaliwa, na kuanza kukohoa. Nilikohoa sana hadi mama akaamka hadi na damu zikawa zinanitoka mdomoni, mama akashangaa sana ikabidi anipatie huduma ya kwanza nayo ni kuniweka sehemu yenye hewa zaidi na kuniwashia feni inipepee.


Nilipotulia akaniuliza nini tatizo, nikamueleza mama kuwa nimepaliwa wakati wa kunywa maji na tukarudi kulala.
Nikamuomba mama asizime taa ya mule chumbani kwani kila akizima nilikuwa naona kama kuna mtu anafungua ule mlango wa mama na kuingia.
Ikabidi mama asizime ile taa na kuniona mwanae kuwa nimeanza kuchanganyikiwa, nililala nimemkumbatia mama hadi kunakucha.


Kwakweli kwangu mchana ulikuwa bora kushinda usiku kwani usiku vioja vinakuwa vingi sana.

Kulipokucha mama akaanza kunilalamikia kwa kumlaza na mwanga wakati yeye kazoea kuzima taa.
"Na leo ukalale chumbani kwako, hayo maswala ya kufanya taa ikeshe chumbani kwangu sitaki. Wewe umekuwa mtu wa maruweruwe tu siku hizi hata sijui una nini jamani? Uoga wako umetukosesha mahela toka kwa mdoli."


"Najua tu hilo la mdoli utakuwa unajilaumu siku zote ila sikuwa na la kufanya kwajinsi alivyokuwa akinitisha"
"Unamaajabu sana mwanangu, eti mdoli anatabasamu loh! Na mimi bila hata ya kufikiria mara mbili, eti tumchome mwanangu. Hii ndio haraka haraka haina baraka"
"Basi yaishe mama"
Nilibaki kujisemea kuwa laiti kama yangekuwa yanawatokea kama ambavyo yananitokea mimi labda wangeelewa.


Badae niliwasiliana na Sam ambaye alikuwa amechukizwa sana na kitendo changu cha kupotezea simu zake.

Mchana wake nilitembelewa na rafiki yangu Suzy, nilifurahi sana na kuongea nae mambo mengi kama rafiki.
Nikamueleza Suzy kuhusiana na alichonifanyia Lucy kwa Sam na jinsi Sam alivyonipa maelekezo ya ilivyokuwa.
"Kwahiyo sasa wewe umeamuaje?"


"Kwakweli nilichukizwa sana, nilitamani hata kuachana na Sam kwa usaliti wake"
"Sikia shoga yangu, usithubutu kuachana na Sam kwaajili ya Lucy. Yani Lucy ni gubegube hana mfano, kazi yake ni kuiba mabwana za watu yani hana lolote nakwambia. Usimuachie Lucy"
"Kama wao wamependana je itakuwaje?"


"Hakuna cha kupendana hapo, Lucy namjua vizuri. Usimuachie bwanako, atamuiba kweli. Unamchezea Lucy eeh! Hana masikhara yule mtoto wa pwani"
"Unanitisha sasa Suzy"
"Usiogope, unatakiwa kuwa ngangari. Pigania penzi lako, usikubali mpita njia akakuharibia safari yako."
Maneno ya Suzy yalinitia moyo kwakweli na kujikuta nikipata nguvu mpya juu ya Sam.


Jioni yake Suzy akaaga na nikaamua kumsindikiza stendi ili akapande daladala la kurudi kwao.
Tukasimama pale stendi na kuendelea na maongezi yetu huku tukingoja daladala na kulikuwa na watu wengine pale nao wakingoja usafiri.


Ikaja basi na kusimama mbele yetu, ikashusha abiria kisha Suzy akapanda basi lile na tukaagana. Kwakweli sikumuangalia hata kidogo yule abiria aliyeshuka.
Baada ya lile basi kuondoka, kuja kutahamaki nilibaki mwenyewe pale kituoni hadi nikashangaa wakati mwanzoni walikuwepo watu wengi tu, nikageuka ili nianze safari ya kurudi nyumbani.
Wakati nageuka, nikashangaa kushikwa mkono na mkaka, ule mkono wake ulikuwa na ubaridi sana uliopenya hadi moyoni mwangu, kisha akasema,


"Habari yako Sabrina"
Nilikuwa nikitetemeka, kuinua macho na kumtazama ni yule mkaka wa ndotoni.

Itaendelea kesho.....!!!
Asanteni kwa maoni yenu wadau.
Kama tuko pamoja   
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:

 
 
Blogger Templates