Social Icons

Sunday, 18 June 2017

HADITHI: Niliolewa na Jini bila ya kutarajia - 7


NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 7:

Nilikuwa nikitetemeka, kuinua macho na kumtazama ni yule mkaka wa ndotoni.
Nilizidi kutetemeka kwani ubaridi uliotembea mwilini mwangu ulikuwa mkubwa sana.
Akaendelea kunishikiria mkono na kuzungumza.


"Mbona waniogopa sana Sabrina? Mimi sitishi, nipo kawaida kama wengine. Nahitaji kukusaidia."
Sikujibu chochote na kuzidi kutetemeka, akaendelea kuongea.
"Tambua kwamba, huwezi kunikwepa kamwe. Ipo siku utaingia kwenye himaya yangu."
Kizunguzungu cha gafla kikanishika na kuanguka.


Nilipozinduka nilikuwa nyumbani kwenye kochi, nimezungukwa na mama, dada na majirani zetu wawili.
Sikuelewa nini kilitokea hadi mimi kuwa pale, ilibidi niwaulize kwani nini kimetokea ukizingatia wote walikuwa wananipa pole nilivyozinduka.


Dada ndiye aliyenijibu swali nililouliza,
"Nimekukuta stendi pale, wakati nashuka kwenye daladala ulikuwa unatetemeka sana na badae ukaanguka. Ndio nikakuwahi pale na watu wengine walikuwepo stendi pale wakasaidiana nami kukuleta nyumbani. Pole sana mdogo wangu.


Nikawa najiuliza, inamaana dada hakumuona yule mkaka niliyesimama nae? Nikawa na maswali mengi kichwani. Mama akasema nipumzike kwanza na wale majirani wakaaga na kuondoka.

Mama alikuwa karibu sana na mimi.


"Saivi uache safari za jioni mwanangu, nadhani una tatizo wewe"
"Sio unadhani mama, huyu Sabrina atakuwa na tatizo tu"
Mama akaniangalia kwa makini sana,
"Hebu niambie mwanangu, nini tatizo?"
"Hata sielewi mama ila kuna mtu huwa ananitokeaga ndotoni, sasa huyo mtu......"
Nikapaliwa na mate na kuanza kukohoa sana, nilikohoa hadi damu ikabidi mama aanze kunipatia huduma ya kwanza.


Dada akaja na kutoa ushauri,
"Au Sabrina atakuwa na malaria inayopanda kichwani?"
"Eti eeh!"
"Inawezekana mama, angalia mambo anayofanya kama ni ya kawaida"
Nikashindwa kumuelewa dada, kupaliwa na mate kunahusiana nini na malaria inayopanda kichwani? Labda kwavile mi sikuwa daktari.


Wakakubaliana kuwa kesho yake nipelekwe hospitali kwenda kupima hayo malaria.

Usiku nililala tena na mama, nikamuomba asizime taa wakati tumelala kumbe mama alivizia muda ambao usingizi umenipitia haswaa na kuzima ile taa.

Nikashtuka kwenye usingizi, na kumuona mtu amesimama kwenye mlango wa mama nikapiga kelele iliyomuamsha hadi mama.


"Ma.....mamaaaaaaaaaa.........."
Kitu cha kwanza kabisa ni mama kuniuliza kuwa kuna nini, nami nikajibu kwa hofu.
"Kuna mtu mlangoni mama"
Huku nimeziba sura yangu kwenye mwili wa mama.
Mara taa ya chumbani kwa mama ikawashwa, hapo ndipo uoga ulizidi kunikamata kwani nilijua kwa vyovyote vile atakuwa ni yule mtu wa ajabu kwani sikumuona mama akiinuka na kwenda kuwasha taa ila taa iliwashwa nikajua leo lazima mama ataelewa kwanini mimi naonekana kama chizi. Nikaamua kuropoka.


"Si unaona amewasha na taa"
Mara kikasikika kicheko, kusikilizia ni sauti ya dada aliyekuwa akicheka sana hadi anagongagonga mguu chini, akaanza kuongea.
"Kheee malimwengu haya humu ndani, tumeanza kuogopana wenyewe kwa wenyewe?
Mama akamuuliza dada,
"Na wewe vipi mapema hii wakati ni mwisho wa wiki? Unaenda kazini na leo?
"Hapana mama, leo Fatuma kaniomba nimsindikize mahali na inatakiwa tuwahi asubuhi sana. Hivi nimekuja kukudamsha uje kufunga mlango, namshangaa huyo chizi wako anapiga kelele"
Akacheka tena, mama nae akajibu.


"Uliyoyasema jana ni kweli, nadhani Sabrina ana malaria iliyopanda kichwani. Nilitaka leo umpeleke hospitali kumbe na wewe una safari zako loh! Basi tutakuja kuongea vizuri ukirudi."
Kwakweli hata sikuelewa elewa, nilijiuliza maswali mengi sana kuwa kuna kitu dada anakijua ila anaficha. Au la anatumiwa, hata kama mimi muoga ila nakataa kabisa kama aliyesimama pale mlangoni mwanzoni alikuwa ni dada. Nikabaki kama nimepigwa bumbuwazi.


Nilibaki nyumbani na mama aliyekuwa anasisitiza kuwa natakiwa kwenda hospitali ila hakutaka niende mwenyewe.
Nilikuwa nikiongea nae huku akiniuliza maswali ya kupima akili yangu.
"Ila mama, mi dada Penina simuelewi siku hizi sijui na yeye ana matatizo gani?"
"Mwenye matatizo ni wewe Sabrina, yani wewe ukapimwe kabisa hiyo akili yako. Nina uhakika utakuwa na matatizo kichwani.


"Sio matatizo mama, kuna mambo ya ajabu huwa yananitokea ndiomana nakuwa hivi"
"Hayo mambo ya ajabu ni yapi mbona huwa huyataji? Au ile kusema mdoli anakuchekea sijui kila mahali ukienda unamkuta, mara tukilala kama mtu anafungua mlango. Ndio hayo mambo ya ajabu? Mbona wenzako hayatutokei sasa, utakuwa na matatizo wewe sio bure.


"Ila kama huko hospitali mi sitaki kupelekwa na dada Penina
"Sawa hakuna tatizo, nitampigia simu hata kaka yako Deo aje akuchukue akupeleke"
"Hapo sawa"
Mimi sikuwa mgonjwa kama wanavyonifikiria, tatizo lao hawataki kunisikiliza na kunielewa. Aliposema habari za kumpigia kaka Deo simu nikaona itakuwa afadhari pengine yeye ataelewa nitakapomwambia kinachonisumbua.


Mchana wa siku hiyo, mimi na mama tulikaa nje ambako tulitandika mkeka.
Tukashangaa kumuona dada akirudi muda huo maana na yeye kwa kawaida yake kama hajaenda kazini na ametoka tu kwa safari binafsi basi kurudi kwake ni usiku ila siku hiyo alirudi mchana.
Akafika na kumsalimia mama kisha akakaa kwenye mkeka, akaniomba nimpelekee mkoba wake ndani basi nikauchukua na kumpelekea chumbani kwake.


Nikauweka ule mkoba, kuangalia mezani namuona yule mdoli tuliyemchoma moto na yale maua, nilitetemeka sana.
Nikakimbilia nje huku nikihema juu juu na kupiga kelele, mama na dada wakaniuliza kuna nini.
"Yule mdoli tuliyemchoma mama yupo chumbani kwa dada"
Ikabidi mama na dada wainuke na kufatana nami hadi chumbani kwa dada, ni kweli mezani walimkuta mdoli ila sio kama yule.


"Umeamini mama kama mwanao malaria imepanda kichwani??"
"Kweli kabisa mwanangu anaumwa, hebu Penina nenda nae hospitali"
"Hata bila ya kupumzika jamani mama?"
"Mpeleke kwanza utakuja kupumzika ukirudi, mdogo wako ana matatizo huyu, atawehuka bure hapa"
Mimi nikawa nawasikiliza tu wanavyonijadiliana kuhusu mimi kama vile mtoto mdogo wakati ni mtu mzima hadi nayajua mapenzi ni nini.


Ikabidi dada anipeleke hospitali, tukaondoka nyumbani na kufanya safari ya kwenda huko hospitali.
Njiani akakutana na rafiki yake wa kiume na kuanza kuzungumza nae kisha akamwambia kama tunaenda hospitali, yule rafiki akasema tupitie kwanza baa tupate mbili tatu halafu hospitali atatupeleka kwenye zahanati ya rafiki yake na huko tutaenda kutibiwa bure. Kwajinsi dada yangu anavyopenda vitu vya bure akafurahi sana na kukubali, basi tukapitia hapo baa ili wazungumze.


Mimi sikuwa mnywaji wa bia kwahiyo niliagiza soda tu ila dada yangu alikuwa ni mnywaji wa haswaa ila zile bia za bure ndio anazozipendelea sana.
Yule mkaka akaagiza na nyama ya mbuzi aliyekaushwa ambayo ikawa inaliwa na kushushia na vinywaji.


Mara akaja mkaka mwingine ambapo yule rafiki wa dada alimtambulisha yule kaka kama rafiki yake, maongezi yakaendelea.
Kila nikimtazama yule kaka mwingine aliyekuja sura yake inabadilika inakuwa ya yule mkaka wa ndotoni, nikajikuta napiga kelele na kuishtua baa nzima kisha nikaanguka.

Kuja kushtuka nilikuwa hospitali kitandani nikipimwa pimwa kuwa nina tatizo gani, dada akaniambia kuwa nilipoanguka ikabidi waniwaishe hospital.


"Mmh! Sijui una degedege siku hizi mdogo wangu!"
Nilimuangalia sana dada hata sikuelewa urafiki wake na watu wa ajabu ajabu kiasi kile ameanza lini.
Nikahudumiwa kisha nikapewa dawa, daktari akasema kuwa sina tatizo ila nanaanguka sababu ya mshtuko tu ambao hakujua unasababishwa na nini.


Tukaanza safari ya kurudi nyumbani. Dada akaanza kunipa masharti yake njiani,
"Tukifika nyumbani usimwambie mama kama tulipitia bar, sawa?"
"Sawa sitamwambia"
"Basi nitakupa zawadi ya yule mdoli mwingine mdogo wangu."
"Hapana, sitaki zawadi yoyote"
Dada alinishangaa mimi kukataa zawadi.


Kurudi nyumbani, jambo la kwanza mama kuliulizia ni kuwa daktari kasemaje kuhusiana na hali yangu.
Dada akamjibu kuwa daktari amesema kuwa sina ugonjwa wowote.
"Sasa ni kitu gani kina msumbua huyu Sabrina?"
"Amepewa dada atumie halafu tutaangalia hali yake inaendeleaje, ikizidi tutaenda nae tena"
Mama akanigeukia kuniuliza tena.


"Hivi siku ile hadi umepaliwa ulitaka kusema nini?"
"Sio siku ile mama, ni jana tu hapo."
"Haya nieleze basi"
Nikataka kumueleza mama, mara kichwa cha gafla kikaanza kuniuma yani kichwa kiliuma kama vile mtu anagonga na nyundo.


Ikabidi mama anipe dawa kisha akaniambia nipumzike, nililala palepale sebleni kwenye kochi.

Akatokea yule kaka, leo alikuwa na sura ya upole kabisa huku akiongea.
"Nihurumie Sabrina, naomba unikubalie. Nitakupa chochote utakacho kwenye ulimwengu huu na nitakupeleka popote utakapo, naomba unikubalie"
Nikawa natikisa kichwa kwa ishara ya kukataa, yule mkaka aliendelea kuongea.
"Nina vingi vya kukupa ambavyo mwanadamu wa kawaida hawezi kukupatia"
Wazo likanijia kuwa huyu lazima ni jini na ndiomana kajitoa kwenye kundi la binadamu wa kawaida. Nikamuuliza.


"Kumbe wewe ni jini?"
"Mimi ni malaika Sabrina"
Akawa ananisogelea ili anishike huku akinyoosha mkono wake, wazo la Sam likanijia nikakumbuka kuwa nampenda sana Sam wangu, yote hayo yalikuwa yakitembea ndotoni.
Yule mtu akasisitiza nimkubalie, nikaona kama amekuja kwenye maisha ya kawaida na kunishika kisha kunisukuma sukuma kama mtu anayeniamsha, nikashtuka gafla na kupiga kelele kwa nguvu,
"Sitakiiiiiii.............


Kumbe mama ndiye aliyekuwa akiniamsha kuwa ninywe dawa na niende chumbani kulala, jasho lilikuwa linanitoka jingi sana.
Nikanywa dawa na kuelekea moja kwa moja chumbani kwangu kulala nadhani hata mama alishangaa kwa mimi kwenda kulala mwenyewe chumbani kwangu, hata sijui ilikuwaje ila nilijikuta uoga umepotea.


Kulipokucha nilijishangaa sana kulala mwenyewe tena chumbani kwangu wakati nimekuwa nikipaogopa kwa siku hizi za karibuni.
Wazo likanijia kuwa natakiwa kumwambia Sam ukweli ili tujue la kufanya, pengine Sam anaweza kunisaidia kwa majanga haya. Nikachukua simu na kumpigia Sam kuwa badae nitakuwa kwake, nikaona njia rahisi ya kuruhusiwa kutoka pale nyumbani ni kujifanya nimepona na kufanya kazi zote za nyumbani.


Basi nikaamka, nikasafisha nyumba, vyombo na kila kitu. Nikafagia uwanja na kuweka kila kitu sawa, nikabandika na mboga ya mchana kwani chai nilishaiandaa.
Mama na dada walipoamka walishangaa sana, hadi mama akasema.
"Naona Sabrina umepona mwanangu, umerudia kuwa mtoto mzuri tena"
Mchana wake nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea Suzy ila nitawahi kurudi.
"Suzy si alikuwa hapa juzi tu?


"Ndio mama ila nimemkumbuka tu"
Mama aliniruhusu kwani aliamini kuwa nimeshapona.

Safari yangu ilikuwa ni moja kwa moja kwa Sam na lengo la safari yangu ni kumwambia Sam ukweli ili ajaribu kutafuta njia ya kunisidia.


Mwanzoni niliogopa kumwambia ukweli kwa kuhofia kwamba huenda Sam atajisikia vibaya na kuhisi kuna mtu mwingine nampenda, kwahiyo tangia nijue kuwa yule mkaka si binadamu wa kawaida ndio nimeamua kumueleza Sam aweze kunisaidia kwa njia yoyote ile.

Nilimkuta Sam ndani na nikakaa nae kitandani ili niweze kumweleza kuhusiana na mambo yanayonitokea.
Nikaanza kumweleza Sam.


"Unajua mwenzio kuna mambo ya ajabu sana yananitokea siku hizi!!"
"Mambo gani hayo?"
Kwavile nilikuwa naongea huku nimejilaza kitandani, nikajikuta usingizi umenichukua palepale kabla hata sijasema chochote.


Katika ndoto, niliona mimi na Sam tuko mule chumbani tukiongea mara kuna mtu akagonga mlango tena anagonga kwa nguvu sana, Sam akainuka kwenda kufungua.
Yule mtu akaingia moja kwa moja, kumwangalia ni yule mkaka wa ndotoni akaja kunishika mkono na kunivuta kuwa niende nae.


Sam hakuweza kupambana nae kwahiyo akaniachia niende.
Nikashtuka gafla na kusema kwa nguvu "Siendi popote" hadi Sam akanishangaa.
"Una nini Sabrina?"
"Hata sijui"
Mara mlango wa Sam ukaanza kugongwa kwa nguvu sana hadi tukashtuka.

Itaendelea kesho.....!!!!
Asanteni kwa maoni wadau, one 
Kama tuko pamoja   
By, Atuganile Mwakalile.

No comments:

 
 
Blogger Templates